JESHI LA POLISI LAMPIGA STOP MAMA REGINA LOWASSA KUFANYA MKUTANO DAR ES SALAAM.
Jeshi la Polisi limezuia kufanyika kwa matembezi ya amani na mkutano wa mke wa mgombea urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Mama Regina Lowassa, uliopangwa kufanyika kwenye viwanja vya Tanganyika Packers, Kawe jijini Dar es Salaam jana.
Mbali na kuzuiwa huko, pia wanawake sita kutoka vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), waliokuwa katika mchakato huo wa matembezi ya kuombea amani, walikamatwa kwa madai ya kufanya maandamano bila kibali cha polisi.
Tukio hilo lilitokea majira ya saa nne asubuhi katika eneo la Mlimani City sehemu ambayo wanawake hao walikuwa wamepanga kuanzia matembezi hayo kuelekea Tanganyika Packers kwenye maombezi ya amani yaliokuwa yanajumuisha wanawake wote bila kujali itikadi zao kisiasa.
Katika mkutano huo, mgeni rasmi alikuwa ni mama Lowassa, ambaye alikuwa awahutubie wanawake hao na Watanzania kwa ujumla kuhusu umuhimu wa misingi ya amani kuelekea Uchaguzi Mkuu Oktoba 25, mwaka huu.
Hata hivyo, matembezi hayo yalishindikana kufanyika kutokana na askari kuwazuia na kuanza kuwatawanya na baada ya wanawake hao kuona baadhi yao wamekamatwa, ndipo wengine walipoanza kutimua mbio kuelekea katika maeneo mbalimbali.
Baadhi yao walikwenda kukaa kwenye ofisi za Ukawa za Ngome zilizopo Kawe.
Akizungumzia tukio hilo, Mratibu wa mkutano huo, Susan Lyimo, alisema maandalizi yalianza tangu Jumatau ya wiki hii na ilikuwa ni matembezi ya amani ambayo walimualika mama Lowassa kuzungumza nao.
Alisema Oktoba 7, mwaka huu waliandika barua kwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Sulemain Kova, na waliwasiliana naye hadi juzi asubuhi lakini hawakupewa majibu.
Lyimo alisema ilivyofika majira ya mchana alipigiwa simu akachukue majibu ya barua iliyomjulisha kuwa matembezi hayo hayaruhusiwi na kutakiwa kufanyike mkutano wa ndani.
Alisema sababu zilizotolewa za kuzuiliwa kwa matembezi hayo hayo ni kwamba askari wengi wapo kwenye kampeni hivyo hakuna askari kwa ajili ya kuwapatia ulinzi.
Sababu ya pili walijulishwa kuwa barabara hiyo ambayo walipanga kuitumia itakuwa na msongamano na ya tatu ni sababu za kiitelejensia kwani panaweza kutokea uvunjifu wa amani.
Alisema baada ya kukataliwa waliamua kufanya mkutano bila matembezi lakini alidai cha kushangaza jana saa mbili katika viwanja vya Tanganyika Packers askari walikuwa kwenye viwanja hivyo na kuzuia watu.
Aidha, alisema baada ya kukamatwa kwa wafuasi wao walikwenda Kituo cha Polisi cha Kijitonyama na kutakiwa kuandika maaelezo na baadaye walipatiwa dhamana baada ya baadhi ya viongozi wa Ukawa kufika kituoni hapo na kutimiza masharti.
Alisema polisi wajibu wao ni kulinda amani na walitegemea kupata majibu ndani ya saa 48, lakini matokeo yake wamekaa kimya hadi juzi majira ya saa 10 alasiri ndipo wanaitwa kuchukua barua.
Alieleza kuwa, mkutano huo ulikuwa unawakutanisha wanawake wote kuongea na Mama Regina masuala ya amani na si vinginevyo.
Nipashe lilifanikiwa kuzungumza na mmoja kati ya waliokamatwa, Farida Mapalala, ambaye alisema wakiwa eneo la Mlimani City walifika askari kati ya 15 na 20 wakiwa na gari aina ya Land Rover Defenda ambao waliwazunguka na kuwajulisha kuwa maandamano yamekataliwa.
Alisema walikamatwa watu sita na kupelekwa Kituo cha Polisi cha Mabatini, Kijitonyama.
Farida alisema wamenyanyasika kwani kitendo cha polisi kuzuia mkutano wao huku wengine wakiruhusiwa ni kuonewa.
Alidai kuwa Ukawa wakifanya mkutano mara nyingi wamekuwa wakinyimwa kibali na kujulishwa kuwa sio halali wakati Chama cha Mapinduzi kikiruhusiwa.
Nipashe lilimtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura, kuzungumzia tukio hilo lakini simu yake iliita bila kupokelewa.
Hata hivyo, alipotafutwa Kova alisema anayepaswa kulizungumzia ni Kamanda Wambura na akatoa namba yake nyingine, lakini nayo iliita bila kupokelewa. CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
0 comments:
Post a Comment