MGOMBEA URAIS WA CCM AANZA KUUNDA JOPO MAALUMU LA WATAALAMU KWA SERIKALI YAKE MPYA.
Mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk John Pombe Magufuli
By Matern Kayera, Mwananchi Digital
Mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk John Pombe Magufuli ameunda jopo maalumu la wanataaluma na wataalamu kutoka kada mbali mbali ikiwa ni maandalizi ya uundaji wa serikali yake endapo atashinda urais.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa CCM, January Makamba alisema kuwa jopo hilo la wanataaluma na wataalamu wa uchumi, biashara, utawala na sheria, kutoka kwenye taasisi za elimu ya juu, asasi zisizo za kiraia, na sekta binafsi, wamepewa majukumu maalumu ya kufanya mabadiliko makubwa serikalini kuanzia siku ya kwanza ambayo Magufuli atakuwa madarakani.
Makamba ameyataja baadhi ya majukumu hayo kuwa ni kuchunguza na kupendekeza maeneo ambayo Serikali itabana matumizi, ikiwemo manunuzi ya umma, posho za vikao na matumizi ya magari, ili Magufuli aweze kufanya maamuzi ya haraka kuyatatua matatizo hayo.
Majukumu mengine ambayo jopo hilo limepewa ni pamoja na kuchunguza na kupendekeza maeneo ambayo Serikali itaongeza mapato mara moja bila hatua za kibajeti, kuchunguza na kupendekeza maboresho makubwa katika mfumo wa utendaji na utumishi na ufanisi katika Serikali.
“Kupitia kodi na ushuru wenye usumbufu kwa wafanyabiashara wa ngazi zote, wakulima, wafugaji na wavuvi iwapo unaweza kurekebishwa bila kuathiri bajeti ya Serikali inayotekelezwa sasa, kupitia sheria zote za nchi na kuorodhesha Sheria ambazo zinapaswa kubadilishwa haraka ili kuharakisha mabadiliko ya kweli na ya haraka ambayo ameyaahidi kwa Watanzania,” alisema Makamba.
Kupitia na kuorodhesha masuala yote na kero zote zinazosubiri maamuzi ya Serikali ili atoe maamuzi kuanzia siku ya kwanza atakapoapishwa.
Kwa mujibu wa Makamba, Dk Magufuli ameazimia kuanza kazi kwa bidii na maarifa, ndiyo maana ameunda jopo hilo. Alisema jopo hilo linapaswa pia kupendekeza miundo na idadi ya Wizara na kutengeneza rasimu za mikataba ya kazi kwa Mawaziri, Makatibu Wakuu na watendaji wengine wakuu atakaowateua mara baada ya kuapishwa kuwa rais wa Tanzania.MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment