Kikosi cha timu ya Polisi Moro SC katika picha ya Maktaba.
Na Juma Mtanda, Morogoro.
Klabu ya Polisi Moro SC imeiomba TFF kutumia darubini za ziada katika michezo ya ligi daraja la kwanza Tanzania bara msimu wa mwaka 2015/2016 baada ya klabu hiyo kukumbana na fitina kubwa na za kiwango cha juu wakati wa mchezo wao na wenyeji Lipuli FC licha ya kupata ushindi wa bao 2-0 katika uwanja wa Samora mkoani Iringa.
Akizungumza na mwanaspoti mjini hapa, Meneja wa klabu hiyo Fikiri Hussein (Mmachinga) alisema kuwa TFF inabidi zitumie darubini za ziada kwa kuangalia michezo ya ligi daraja la kwanza hasa kwa kuwalenga baadhi ya waamuzi wamekuwa na tabia ya kuungana na timu wenyeji kwa lengo la kuwasaidia uwanjani ili kuibuka na ushindi.
Hussein alisema kuwa katika mchezo huo mwamuzi, Riziki Mwakyami kutoka Pwani alitoa kadi nne nyekundu kwa wachezaji wa Polisi Moro SC na Lipuli FC.
“Ligi daraja la kwanza hawa TFF wanapaswa kuwa na darubini ya ziada ya kuwamulika waamuzi wanaochezesha michezo hii kwani wengi wao wanaingia uwanjani wakiwa na lengo la kuegemea upande wa timu mwenyeji jambo ambalo sio sahihi kabisa.”alisema Hussein.
Waliopewa kadi nyekundu kwa upande wa Polisi Moro SC ni pamoja na mlinda mlango wao tegemeo, Elias Sospeter na mlinzi Nahoda Bakari wakati Lipuli FC ni Tony Manyiro na Danny Mrwanda.
Polisi Moro SC tayari imeshuka dimbani mara tatu na kuzoa pointi sita baada ya kupata ushindi mbele ya Burkina FC na Mji na Lipuli FC huku ikipoteza mchezo kwa Mji Njombe FC.
Katika kundi hilo JKT Mlale FC ya Songea na Mji Njombe FC ndiyo zenye pointi saba kila mmoja huku JKT Mlale ikiongoza kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.
0 comments:
Post a Comment