BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

KADA WA CCM ISAKA AGONGWA NA GARI BAADA YA KUTOKEA VURUGU BAINA YA WAFUASI WA CHAMA HICHO NA CHADEMA MKUTANO WA KAMPENI WA MGOMBEA MWENZA DODOMA


Dodoma. Kada wa CCM, Fatuma Isaka anayedaiwa kugongwa na gari kwenye vurugu zilizotokea juzi baada ya wafuasi wa chama hicho kuvamia mkutano wa kampeni wa mgombea mwenza wa Chadema, Juma Duni Haji, amefariki dunia.

Tukio hilo lilitokea saa tisa alasiri katika Viwanja vya Shule ya Msingi Chang’ombe A kabla ya Duni kuwasili kuhutubia mkutano wa kampeni.

Inadaiwa Fatuma aligongwa na gari la CCM baada ya kuteleza wakati likiondoka kwenye uwanja huo.

Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Jenifa John alisema wakiwa katika viwanja hivyo, walifika makada sita wa CCM na kuwaamuru wanachama wa Chadema kuondoka kwa madai kuwa ratiba ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ilionyesha hawakupangiwa kufanya mkutano kwenye eneo hilo kwa siku hiyo.

“Walituambia Serikali ni yao na shule ni yao, kwa hiyo hakuna chama chochote kinachoweza kuwazuia kufanya kampeni mahali hapo na kututaka tuondoke,” alidai Jenifa.

Alisema baada ya mabishano hayo, makada hao wa CCM waliokuwa na gari, waliamua kuondoka.

Alisema wakati gari linaondoka, kada mmoja wa chama hicho (hakumtaja jina) alikuwa hajapanda, hivyo alivyokuwa akitaka kulirukia kwa bahati mbaya aliteleza, akaanguka na kukanyagwa na magurudumu ya nyuma.

“Wenzake waliondoka na kumuacha majeruhi huyo akiwa chini. Wakazi wa eneo hili walikodi gari na kumpeleka hospitali,” alidai Jenifa.

Akizungumzia tukio hilo, Katibu wa Chadema Mkoa wa Dodoma, Kennedy Kimario alisema CCM ilifanya makusudi kuvamia mkutano huo. “Walifanya fujo bila sababu, walikuwa wanajua kuwa anapokuja mgombea urais au mgombea mwenza kisheria mikutano yote midogo ya kampeni inapaswa kusimama,” alisema Kimario.

Katibu Msaidizi wa CCM Mkoa wa Dodoma, Othman Dunga alivilaumu vyombo vya dola kwa madai kuwa vilishindwa kuchukua hatua mapema. “Sisi tulikuwa na barua halali kutoka kwa msimamizi wa uchaguzi ya kufanya mkutano mahali hapo, lakini walipokuja polisi waliwaruhusu Chadema waendelee na mkutano wao wa kampeni,” alidai Dunga.

Hata hivyo, Dunga alidai kuwa kada huyo aligongwa na gari la Chadema na kuchomwa mwilini na vitu vyenye ncha kali.

Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Dodoma, David Mnyambuga alithibitisha kutokea kwa mgongano wa ratiba kati ya vyama hivyo na kumalizwa na msimamizi wa uchaguzi wa Manispaa ya Dodoma Mjini.

“Ratiba ilileta shida baada ya kufanyiwa marekebisho kwa sababu siku hiyo aliyekuwa ahutubie mkutano ule wa kampeni alikuwa mgombea mwenza wa Chadema, kwa mujibu wa utaratibu, ililazimu kupangua ratiba suala hilo lilimalizwa na mkurugenzi ambaye ni msimamizi wa Uchaguzi wa Manispaa ya Dodoma Mjini),” alisema.MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: