Mgombea wa urais kupitia Chama Cha mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, amesema akiwa rais ataendelea kukamata meli za kigeni zinazovua samaki kwenye bahari ya Tanzania kinyume cha sheria kama alivyowahi kufanya akiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi.
Alisema hatakubali kuona samaki wa Tanzania wanageuzwa shamba la bibi, hivyo samaki watakaokamatwa kwenye meli zinazovua kiholela watagawiwa kwa wananchi kama kitoweo. Dk. Magufuli alisema hayo kwenye mikutano yake ya kampeni katika majimbo ya Mchinga na Kilwa Kusini mkoani Lindi na pia Kibiti mkoani Pwani.
Mgombea huyo alisema kuna watu wanamchonganisha na wavuvi kwa kudai kwamba akiingia madarakani atachoma nyavu zao na hawatakuwa na fursa za kuendesha shughuli zao.
Alisema yeye atakuwa rafiki mkubwa wa wavuvi wadogo na atawawezesha kwa mikopo na zana bora za uvuvi ili wavue kisasa na kuondokana na umaskini. Alisema atapambana na meli kubwa za uvuvi ambazo zimekuwa zikiiba samaki ambao ni mali ya Watanzania.
“Sitaruhusu samaki walio kwenye bahari yetu wawe shamba la bibi. Wanaojijua kuwa wanaiba samaki wetu arobaini zao zimefika, mimi nitakamata na kugawa bure kwa wananchi, maana samaki ni mali yao…. kama niliweza kufanya hivyo nikiwa waziri wa kitoweo, siwezi kushindwa nikiwa rais,” alisema.
Alisema kama makampuni ya nje yatataka kuvua kwenye samaki waingie mkataba na serikali yake ili kuweka maslahi kwa pande zote mbili badala ya kunufaika wao binafsi.
Alisema serikali yake itawapenda wavuvi wadogo tofauti na uzushi unaoenezwa kwamba atawabana na itaanzisha ufugaji wa samaki na kujenga viwanda vingi vya kusindika samaki ili kuongeza nafasi za ajira.
Alisema nchi za China na Vietnam zimekuwa zikiuza nje ya nchi samaki wanaotoka kwenye mabwawa ya ufugaji hivyo haoni kama itashindikana kwa serikali yake kuiga kutoka kwa nchi hizo.
Alisema kukiwa na viwanda vingi wavuvi watauza samaki wao kwenye viwanda kwa bei nzuri, hivyo kuongeza kipato na kuondokana na umaskini.
Dk. Magufuli alisema Tanzania ina rasilimali kama dhahabu, gesi, Tanzanite, wanyama na samaki wa kilo 350, rasilimali ambazo zikitumika zinaweza kuwaondoa Watanzania kwenye lindi la umaskini.
Alisema hakuna sababu ya serikali kupambana na wachuuzi wadogo wadogo kama mamalishe wakati ingeweza kukusanya mapato makubwa kwenye vyanzo mbalimbali vya mapato vinavyoingiza hela nyingi.
Akiwa katika jimbo la Mchinga mkoani Lindi, Dk. Magufuli alisema wilaya hiyo ina historia ya pekee duniani kwani mabaki ya mjusi mkubwa ambayo yamehifadhiwa Ujerumani yalitokea kwenye wilaya hiyo.
Dk. Magufuli alisema akifanikiwa kuwa rais atafuatilia mapato yanapatikana kutokana na kuwapo kwa mabaki hayo nchini humo ili ziwanufaishe pia Watanzania.
Dk. John Magufuli jana aliingia mkoani Pwani kwa kishindo kutokana na mapokezi makubwa ya watu aliyopata kwenye mkutano wake wa kwanza wa kampeni mkoani humo.
APATA MAPOKEZI MAKUBWA
Dk. Magufuli ambaye alikuwa akitokea mkoani Lindi, aliwasili kwenye viwanja vya Mwinyi wilayani hapa saa 11 jioni na kukuta uwanja huo ukiwa umefurika idadi kubwa ya wananchi.
Mgombea huyo alielezea kushangazwa na mapokezi hayo makubwa na kuahidi kuwa akifanikiwa kuingia Ikulu atawakumbuka watu wa Mkuranga kutokana na walivyompokea.
“Kote nilikopita nimepokewa na watu wengi, lakini Mkuranga mmetia fora… hili ni deni kubwa kwangu na nawaahidi kuwatumikia kwa dhati na bila ubaguzi, maana maendeleo hayana vyama... mmenipa raha na hapa nilipo nina furaha sana. Naahidi wilaya yenu nitaiweka kwenye moyo wangu,” alisema Dk. Magufuli huku akishangiliwa na umati uliojitokeza kwenye viwanja hivyo.
Aliwaomba Watanzania wamuombee maana kuna watu aliowaita kuwa ni mafisadi hawampendi kwa kuwa wanajua akishaingia madarakani atafunga mianya yote ya rushwa na ufisadi ambayo wamekuwa wakiitumia kunyonya fedha za Watanzania.
Alimmwagia sifa mgomeba ubunge wa jimbo hilo, Abdalah Ulega, kwamba ni kijana mchapakazi na ambaye wana- Mkuranga walipaswa kuwa naye miaka kumi iliyopita kwa sababu wilaya yao imechelewa kwa maendeleo.
“Huyu kijana nampenda sana na nitambeba ili kuharakisha maendeleo ya wilaya hii, mmechelewa sana kumpata huyu Ulega... mlipaswa kuwa naye zaidi ya miaka kumi iliyopita na huenda mngekuwa mbali sana kimaendeleo,” alisema Magufuli.
Alisema atateua mawaziri wachache, lakini wachapakazi na wale watakaoshindwa kwenda na kasi yake watakimbia ofisini kwa sababu hatawaendekeza watu dhaifu. CHANZO: NIPASHE
MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO
Home / kitaifa /
siasa /
slider
/ MGOMBEA URAIS WA CCM DK JOHN MAGUFULI AZUNGUMZIA SAMAKI KATIKA KAMPENI ZAKE MKOANI LINDI.
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment