SABABU YA BALOZI JUMA MWAPACHU KUNG'ATUKA KUJIVUA UANACHAMA WA CHAMA CHA MAPINDUZI CCM WAGUNDULIKA BILA SHAKA YOYOTE.
Balozi Juma Mwapachu (Mwenye sharti ya madoadoa) kulia akisalimiana na Mhe Edward Lowassa enzi hizo wakiwa wote chama cha mapinduzi CCM.
Wimbi la ‘kutimka’ kwa makada katika Chama Cha Mapinduzi (CCM) linazidi kushika kasi baada ya kada mwingine wa chama hicho, Balozi Juma Mwapachu, kutangaza kujivua uanachama wa chama hicho jana.
Uamuzi wa Mwapachu kujitoa CCM, unakuja siku chache baada ya aliyekuwa kada mwenye nambari nane wa CCM, Kingunge Ngombale Mwiru kutangaza kujitoa chama hicho Oktoba 4, mwaka huu.
Katika taarifa yake aliyoitoa jana huku sehemu kubwa akimsifia Lowassa, Mwapachu ambaye hakutaja anajiunga na chama gani, alisema kuanzia kesho (leo) yeye siyo tena mwanachama wa CCM na anatarajia kurudisha kadi yao.
“Nimepata fursa ya kuwa kiongozi ndani ya chama hiki. Lakini kuanzia kesho (leo) mimi si mwanachama wa CCM tena. Na mimi nakubaliana na msimamo wa Lowassa na hao waliomfuata kutoka ndani ya CCM.” alisema Mwapachu.
Alisema alikuwa mwananchama wa CCM tangu mwaka 1967 wakati alipojiunga na Tanu ambacho baadaye kiliungana na ASP na kuzaa CCM .
Alisema tangu alipokuwa mjini Dodoma kwenye mchahakato wa kumpata mgombea wa urais ndani ya CCM alikuwa akimuunga mkono Edward Lowassa ambaye hivi sasa ni mgombea urais wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) anayeungwa mkono pia na vyama vingine vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vya NCCR-Mageuzi, NLD na Chama cha Wananchi (CUF).
Alisema Lowassa ndiye chaguo lake katika kampeni za kumpata Rais mpya wa Tanzania na kueleza kuwa chaguo lake si ndoto wala mlipuko wa mapenzi juu ya Lowassa.
Mwapachu alisema amemfahamu Lowassa tangu miaka ya 90 akiwa kada wa CCM kwa mahusiano katika majukumu ya kichama.
“Kama marehemu Baba wa Taifa alivyowahi kusema, ‘CCM si mama yangu’. Hivyo ndugu zangu, kuanzia kesho (leo) mimi si mwana-CCM tena. Nitarejesha rasmi kadi yangu kupitia ofisi ya CCM ya kata yangu Mikocheni, Dar-es-Salaam. Kwa sasa sijaamua kujiunga na chama kingine. Mwenyezi Mungu anilinde,” alisema Mwapachu.
Alisema Lowassa amejaliwa nuru na uwezo wa kuongoza na kupendwa na watu. Pia ni msikivu na asiyependa ukiritimba na utovu wa nidhamu kazini, iwe ni kwa upande wa watumishi au kwake mwenyewe.
Aliendelea kusema kuwa, Lowassa ni kiongozi ambaye uchamungu wake unamsaidia kuwa na uongozi unaojali na kuheshimu utu, ukweli na uwazi.
Mwapachu ambaye aliwahi kushika nafasi mbalimbali serikalini, ndani ya CCM na pia kuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, alisema kuwa viongozi wanaodhani au kutaharuki kuwa Lowassa ana hulka ya kulipiza kisasi kwa jambo lolote ni waongo.
“Lowassa ni chaguo la wengi na CCM katika busara yake ya kumuengua katika mchakato wa kumpata mgombea wa urais, kimedhihirisha kutokuwa chama kinachoendeshwa kwa misingi ya demokrasia,” alisema Mwapachu.
Alisema dalili za CCM kupoteza lengo la kuwa chama cha watu na kuwa cha viongozi wachache zilianza siku nyingi na hasa katika kipindi cha uongozi wa Rais Jakaya Kikwete.
Alisema CCM kimebadilika na kuwa chama cha makundi na migawanyiko yakupambana si kwa malengo ya itikadi na ujenzi wa chama, bali ya kumalizana na kutaka kufukuzana.
Mwapachu alieleza kuwa Lowassa angeweza kufukuzwa miaka mingi iliyopita ila alishinda vita kutokana na kupendwa na idadi kubwa ya wanachama ndani ya CCM.
Balozi Mwapachu alisema kujivua uanachama kwa Lowassa hivi karibuni ulikuwa ni uamuzi sahihi kwa sababu CCM si chama tena cha watu na kimetekwa.
Kadhalika, alisema aliwahi kuandika makala siku za nyuma akinukuu mshairi kutoka nchini Uingereza aliyeandika 'There comes a time when the door opens and allows the future in'.
Alisema mlango huo sasa umefunguka usoni kwake na uamuzi wake ni kukubali kwamba wakati mpya umewadia ambao ni wakati wa mabadiliko.
Alisema kuendelea kujihisi kwamba bado ni mwana-CCM wa kadi ni kukubali kujidanganya mwenyewe.
MWAPACHU NI NANI?
Mwapachu alizaliwa Septemba 27, 1942 jijini Mwanza, na amewahi kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Machi 24, 2006 na Rais Jakaya Kikwete.
Kabla ya uteuzi huo, aliwahi kuwa Balozi wa kudumu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu (Unesco).
Pia aliwahi kufanya kazi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Balozi wa Tanzania nchini India, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) pamoja na kuwa Kamishna wa Tume ya Kurekebisha Mashirika ya Umma.
Kadhalika, aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Shirikisho la Wenye Viwanda (CTI).CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment