BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

RAIS KIKWETE AWATAKA WATANZANIA KUCHAGUA RAIS ASIYE NA KIGUGUMIZI OKTOBA 25.

Rais Jakaya Kikwete akivalishwa skafu baada ya kuwasili Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma kuongoza maadhimisho ya kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru na kumbukumbu ya miaka 16 ya kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Kushoto ni Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk Fenella Mukangara.(Picha na Freddy Maro).
RAIS Jakaya Kikwete amesisitiza wapiga kura katika uchaguzi mkuu, kuchagua mgombea urais asiye na kigugumizi kwenye kukemea rushwa.

Aidha, Rais Kikwete amesisitiza Oktoba 25, watu wenye sifa wakishakamilisha kupiga kura, warudi nyumbani kwa kuwa jukumu la kulinda kura vituoni si lao, bali ni la mawakala wa vyama vya siasa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Akizungumza jana mjini hapa kwenye kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru sambamba na kumbukumbu ya miaka 16 ya kifo cha Mwalimu Julius Nyerere, yaliyofanyika mjini Dodoma, Rais Kikwete alisema baadhi ya viongozi kwenye vinywa vyao, wana vigugumizi vya kutaja neno rushwa na wanapata tabu nalo.

“Tunataka viongozi wasio na vigugumizi kusema rushwa ni mbaya,” alisema.

Alisema kumchagua kingozi mwenye kigugumizi na rushwa ni kutafuta majanga na watanzania wanatakiwa kufanya maamuzi ya kuwakataa, wasichaguliwe kuwa viongozi.

Pia aliwataka wananchi kufuata maagizo yote ya NEC .

“Vyama vya siasa vina wajibu wa kufuata agizo la NEC, uchaguzi unafanywa kwa mujibu wa Katiba na unasimamiwa na NEC, wananchi mliojiandikisha pigeni kura kwenye vituo mlivyojiandikisha kisha rudini nyumbani na siyo kulinda kura”,alisisitiza Rais Kikwete.

Alisema NEC imeelekeza vizuri utaratibu wa kulinda kura kwenye vituo vya kupigia kura kwamba inafanya kwa kushirikiana na mawakala wa vyama vya siasa.

Aliwataka mawakala wasikubali kuchuuzwa na viongozi wao.

Wakaidi kukiona

“Msikubali kuchuuzwa na viongozi wenu, hizo ni vurugu, tunaomba agizo la NEC liheshimiwe, atakayekaidi hatutamvumilia, na msilazimishe serikali kufanya yasiyopenda, lisilobudi lisifanywe”alisisitiza Rais Kikwete.

Akisisitiza hilo, Rais Kikwete alisema wenye nia ovu, wana hiari ya kutii au kukaidi agizo hilo. Hata hivyo, alisema serikali itatumia nguvu ile ile itakayotumika kwa wakaidi, kwa kuwa wana nia ya kuleta ruvugu na kuvunja amani nchini.

“Hivi unapoambiwa usiondoke ubaki kituoni kulinda kura, mantiki yake ni rahisi wewe uko nje ya kituo cha kura, huwezi kulinda kura, ila walio ndani ndio wanaolinda na hao ni mawakala, sasa nyie wengine uko nje ni kuleta vurugu”,alisema Rais Kikwete.

Alisisitiza wananchi waliojiandikisha kujitokeza kupiga kura kwa kutokubali kuhadaiwa kuuza vitambulisho vya kupigia kura, kwani kufanya hivyo ni kuuza haki yao ya msingi.

“Nasikitishwa na watu wanaouza vitambulisho vya kupigia kura na pia wanaonunua, huku ni kupoteza haki yenu ya msingi, hivi mnaonunua ndiyo demokrasia ya ushindi?, nasisitiza vyombo vya dola fuatulieni na wanaobainika kuuza na kununua wote sheria iwabane,” alisisitiza Rais Kikwete.

Rais Jakaya Kikwete aliwataka Watanzania kuwakataa kwenye masanduku kura wanaotaka kuingia Ikulu kwa kutumia madhehebu ili taifa lisijute baadaye kwa kuchagua viongozi wasio na sifa.

“Oktoba 25, tuwakatae watu hao kwa kuepusha nchi na balaa na majanga, mgombea anakuwa na kigugumizi kutaja neno rushwa tangu kuteuliwa na chama chake yuko kimya hataji kabisa rushwa,” alisema.HABARILEO
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: