TUTAMCHANGUA HIVYO HIVYO EDWARD LOWASSA HATA KAMA NI MGONJWA ILI AWE RAIS WA TANO WA TANZANIA.
Mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa akihutubia mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye Uwanja wa Sabasaba, Tarime Mjini, mkoani Mara jana. Picha na Othman Michuzi Serengeti.
Mwenyekiti wa Chadema Musoma Mjini, Vicent Nyerere amesema Mkoa wa Mara utamchagua Edward Lowassa kuwa rais licha ya madai kwamba ni mgonjwa ili aweze kushughulikia masuala ya hospitali na kumwambia mgombea huyo kuwa:
“Wanasema wewe mwizi, sisi huku tumesema tutamchagua mwizi na kumfungia Ikulu miaka 10 atumikie wananchi.”
Nyerere alisema hayo katika mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye Uwanja wa Sokoine, Serengeti mkoani Mara.
“Lowassa wamekutukana sana na wengine wanasema wewe mgonjwa, sasa sisi tumesema Mkoa wa Mara tunamchagua mgonjwa ili ashughulikie masuala ya hospitali zetu kwa kuwa hilo ndilo tatizo kubwa.
“Rais ambaye akiweka sahihi mtu ananyongwa, sahihi yake inaruhusu nchi kuingia vitani, anazungumza kuwa atajenga Mahakama za kufunga wezi na mafisadi, wakati ukienda magereza waliojaa ni walala hoi… sisi watu wa Mkoa wa Mara tunasema hatuhitaji mahakama za mafisadi, tunahitaji hospitali bora,” alisema Nyerere.
Huku akishangiliwa na umati wa waliofika kumsikiliza, Nyerere alisema pia kuwa baba yake mkubwa, hayati Mwalimu Julius Nyerere alitawala kwa miaka 23 lakini hakuwahi kutoa kauli za kibabe.
Lowassa
Akihutubia mkutano huo wa kampeni, Lowassa aliahidi kujenga barabara ya lami kuanzia Makutano hadi Mto wa Mbu kupitia Mugumu iwapo atachaguliwa na kusema anakusudia kumaliza matatizo yanayoisumbua wilaya hiyo ikiwamo barabara, chujio la maji, migogoro ya wanyama na wananchi na hospitali ili kuhakikisha wananchi wa wilaya hiyo wanafaidi matunda ya nchi.
“Wingi wenu ni ishara kubwa kuwa mnataka mabadiliko ya kweli, natambua mnayo matatizo mengi hapa, ninaombeni mtumie wingi wenu huu kunipigia kura, mbunge na madiwani ili tuweze kuleta mabadiliko, nasisitiza nipeni mgombea ubunge ili tushirikiane kukamilisha matatizo hayo ikiwamo barabara,” alisema.
Hivi karibuni, akiwahutubia wakazi wa Mji wa Mugumu, mgombea mwenza wa CCM, Samia Suluhu Hassan alisema wakichaguliwa, watahakikisha barabara hiyo inajengwa kwa kiwango cha lami.
Lowassa alisema anakerwa na mfumo ambao umeanza kujengeka wa wanyama kuthaminiwa kuliko wananchi, pamoja na kurejea kauli yake kuwa serikali yake itachunguza upya suala la Operesheni Tokomeza ili waliopata madhara wafidiwe huku akisisitiza kurudisha heshima ya wananchi kuthaminiwa badala ya wanyama.
Kuhusu bodaboda, aliahidi kuwa serikali atakayounda itawatafutia benki ili wakopeshwe.
“Katika nchi zilizoendelea kundi kama hili la bodaboda, serikali inawajibika kuwalipa kwa kuwa hawana ajira… hapa pamoja na kushindwa kuwatafutia mitaji, wamebaki kuwafukuza na kuwapiga, lazima hayo yakomeshwe na watakuwa marafiki zangu,” alisema.
Akimnadi mgombea ubunge jimbo hilo, Marwa Ryoba na madiwani wa kata 30, Lowassa aliwataka wananchi kutobweteka, bali wahakikishe wanajitokeza kwa wingi kwenda kupiga kura na kwamba hiyo ndiyo itakuwa silaha pekee ya kuiondoa CCM na kuiweka ya Ukawa ili iwaletee mabadiliko ambayo yameshindikana kwa muda mrefu.
Sumaye
Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye aliwataka wananchi wasimchague mgombea wa urais wa CCM kwa kuwa hana sifa za kuwa kiongozi mkuu, haambiliki na hapokei ushauri wa wengine.
“Nimekuwa Waziri Mkuu kwa miaka 10, Lowassa na Magufuli walikuwa mawaziri chini yangu, najua utendaji wao, Lowassa ni mtu wa kutafakari kwanza kabla ya kuchukua hatua, lakini huyu Magufuli anahitaji kuwa chini ya mtu... kauli zake za sasa hata ninyi mmesikia huyu alipaswa kuwa waziri chini ya mtu,” alisema.
Sumaye alisema wananchi wanatakiwa kumpima kwa kauli zake ambazo anatoa kwa sasa ikiwa ni pamoja na kushughulikia mafisadi na wala rushwa ndani ya Serikali ya sasa ambayo na yeye ni miongoni mwao.
“Wao wanapita na kututukana lakini sisi tunaeleza ukweli mtupu, kama ufisadi umemshinda ndani ya wizara yake anawezaje ngazi ya urais? Amelazimisha kununua meli mbovu iliyotumika kwa zaidi ya miaka 30 ambayo walitarajia iwe inafanya safari zake kwenda Bagamoyo, sasa wameipeleka Kusini, nawaambia Watanzania mtajuta,” alisema.
Alisema miongoni mwa matatizo yatakayoikuta serikali itakayoundwa na Lowassa endapo atachaguliwa ni kulipa madeni makubwa ya nje ambayo yamefikia zaidi ya Sh35trilioni. Alisema wakati hali ya maisha inazidi kuwa ngumu kutokana na matumizi mabaya ya CCM ikiwamo safari zaidi ya 412 za Rais zilizotumia zaidi ya Sh4trilioni kwa kipindi cha miaka 10, Dk Magufuli amezisifia kuwa zimetusaidia na kuongeza kuwa hiyo inaashiria kuwa wakimchagua huenda akatembea zaidi ya mtangulizi wake.
Alibainisha kuwa mfumo ndani ya CCM ni mbovu ndiyo maana watu wengi wanakimbia, kwa kuwa fedha za umma zinachotwa na watu na kuanzisha kampuni kubwa ambazo huandika majina ya watoto wadogo hata wa miaka mitatu, huku watoto wengine wakikosa madawati na dawa hospitalini hakuna.
Kabla ya mkutano
Shughuli nyingi mjini Mugumu zilisimama na watu walijaa uwanjani hapo kuanzia saa mbili asubuhi, eneo hilo likipambwa kwa bendera na mabango ya mgombea huyo. Aliwasili saa sita mchana na kuhutubia na baadaye kuelekea Nyamongo wilayani Tarime.
0 comments:
Post a Comment