DK MAGUFULI AAPISHWA RASMI KUONGOZA TANZANIA KWA AWAMU YA TANO, RAIS MSTAAFU JAKAYA KIKWETE AAGWA NA KUPIGIWA MIZINGA 21 NA VIKOSI VYA ULINZI NA USALAMA DAR ES SALAAM.
Rais John Magufuli akiwa amenyanyua juu mkuki na ngao muda mfupi baada ya kuapishwa kuwa Rais wa awamu ya tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam leo.Picha na Emmanuel Herman
By Louis Kolumbia, Mwananchi Digital
Dar es Salaam. Rais Mteule John Magufuli leo ameapishwa kuwa rais awamu ya tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kusema anafahamu majukumu makubwa aliyonayo kutekeleza ahadi alizozitoa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu.
Magufuli ameyasema hayo kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam katika salamu zake za shukrani kwa Watanzania baada ya kuapishwa kushika wadhifa huo mkubwa nchini.
Ameahidi kufanyakazi kwa bidii ili kukidhi matarajio ya Watanzania waliomchagua kwa kura nyingi, akisema mchakato wa uchaguzi umekwisha na sasa wananchi na wote alioshindana nao kuwania nafasi hiyo waungane katika kuijenga nchi.
“Tanzania ni kubwa kuliko matamanio ya mtu mmojammoja.
Niwaambie wagombea wenzangu, sasa uchaguzi umekwisha tuungane kuijenga nchi yetu. Hakuna matamanio yatakayozidi ukubwa wa nchi yetu” amesema Dk Magufuli katika hotuba yake hiyo fupi.
Rais Magufuli na Makamu wake Samia Suluhu Hassan wamekula viapo vyao mbele ya jopo la majaji lililokuwa chini ya Jaji Mkuu, Mohamed Othman Chande baada ya kuibuka washindi katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka huu.
Rais huyo wa awamu ya tano ameapa kulinda katiba, kuwatumikia Watanzania kwa uadilifu, bidii, juhudi na maarifa, haki na usawa pasipo ubaguzi wa aina yoyote.
Sherehe hizo zilizohudhuriwa na wakuu wanane wa nchi za Afrika, watu wengine mashuhuri toka sehemu mbalimbali duniani zilitanguliwa na kuagwa rasmi kwa Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete kwa kupigiwa mizinga 21 na vikosi vya ulinzi na usalama.
0 comments:
Post a Comment