Dar es Salaam. Mfanyabiashara, Yeriko Yohanesy Nyerere amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akikabiliwa na mashtaka matano ya kutoa taarifa za upotoshaji kupitia mtandao wa Facebook.
Wakisoma hati ya mashtaka kwa kubadilishana mawakili wa Serikali, Simon Wankyo na Paul Kadushi jana mbele ya Hakimu Mfawidhi, Cyprian Mkeha walidai kuwa mshtakiwa huyo alifanya makosa hayo kinyume na kifungu cha 16 cha Sheria ya Mtandao namba 14 ya 2015. Wankyo alidai kuwa Oktoba 25, 2015 katika eneo lisilojulikana Nyerere alichapisha taarifa za upotoshaji kupitia mtandao wa Facebook kuwa ‘piga kura leo huku ukikumbuka kifo cha Mwangosi, Mateso ya Ulimboka na Kibanda, mateso ya kijana wetu wa JKT. Ukikumbuka hayo fanya uamuzi sahihi bila ushabiki.’
Wakili huyo wa Serikali alidai kuwa Oktoba 24, 2015 katika eneo lisilojulikana jijini Dar es Salaam mshtakiwa huyo alichapisha taarifa za upotoshaji kupitia mtandao wa Facebook, kuwa Taifa la Tanzania kuanzia leo (yaani Oktoba 24) halihitaji amani, linahitaji haki tu.
Alidai kuwa Oktoba 24, 2015 mshtakiwa huyo alichapisha taarifa za uongo kupitia Facebook kuwa siku ya leo (Oktoba 24) mpaka siku ya kuapishwa Lowassa, taifa hili halihitaji amani bali taifa hili linahitaji haki tu, amani ilishatoweka siku nyingi, kilichosalia ni uvumilivu tu.
Mbali na hayo pia alichapisha taarifa za uongo kuwa, njia sahihi ya kulitibu taifa hili ni kwa dola dhalimu kutenda haki hata kama itawauma.
“Uchaguzi huu ni vita, anayedhani ni demokrasia apimwe akili. Hii ni vita kati ya umma na dola, ni vita kati ya wema na ubaya, ni vita kati ya shibe na njaa , ni vita kati ya masikini na matajiri, CCM siyo chama cha siasa kwa sasa, ni muungano wa kihalifu unaolindwa na baadhi ya watumishi wa vyombo vya dola .
“Umma umekosa amani na furaha , fursa pekee waliyoipata Watanzania wanamjua rais wao wanayekwenda kumchagua kesho (Oktoba 25), jaribio lolote litakalofanywa na CCM na vibaraka wao la kukwamisha matakwa ya umma litaondoa hata ule uvumilivu kidogo walionao Watanzania na kisha vitazaliwa vichaa chongo ambavyo hata risasi na mabomu hayatakizima.
“Kwa siku ya leo (Oktoba 24) mpaka siku ya kuapishwa Lowassa, taifa hili halihitaji amani, bali taifa hili linahitaji haki tu,” yalinukuliwa mahakamani maneno yanayodaiwa ya Yeriko.
Mshtakiwa huyo anadaiwa kuwa Agosti 24, 2015 alichapisha taarifa nyingine ya upotoshaji kupitia mtandao huo wa Facebook akidai, “mipango ya hujuma ya JK toka Ngurdoto Arusha muda huu.
Kikwete yupo Ngurdoto Arusha na wakuu wote wa mikoa na wilaya Tanzania nzima pia wakuu wa vyombo vya dola na wanadhimu mbalimbali,” yalinukuliwa maneno yanayodaiwa ya Yeriko.
“Wakuu wa mkoa wanaelezwa kwanza kuwa NEC kwa kushirikiana na CCM tayari wameshatengeneza kura bandia kwa kutumia mfumo wa kalamu za kichina.
“Pia wanaamuliwa kuhakikisha wanahujumu kampeni za Ukawa kwa kutumia vyombo vya dola, wanaagizwa kuhakikisha kamatakamata ya vijana wa bodaboda wiki moja kabla ya uchaguzi na zaidi ni wakuu hao wa mikoa wanaagizwa wakawaagize ma-DC kote nchini kuhakikisha wanalinda masilahi ya CCM walipo siku ya uchaguzi,” yalinukuliwa maneno yanayodaiwa ya Yeriko.
Yeriko anadaiwa kuwa Septemba 3, 2015 katika eneo lisilojulikana alichapisha taarifa za upotoshaji kupitia mtandao wa Facebook kuhusu uwepo wa akaunti ya benki ya kughushi inayomilikiwa na Mtanzania katika benki ya HSBC tawi la North London ikionesha CCM imemuwekea Dk Slaa E 1.5 milioni kupitia kwa mchumba wake Josephine Mshumbusi ikiwa ni rushwa ili kushinda uchaguzi 2015.
Mawakili hao wa Serikali walidai kuwa mshtakiwa huyo alichapisha taarifa hizo za upotoshaji akiwa na lengo la kupotosha umma katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, mshtakiwa alikana na Hakimu Mkeha alimtaka mshtakiwa huyo kuwa na mdhamini mmoja ambaye atasaini bondi ya Sh5 milioni.
Upande wa mashtaka ulidai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na mshtakiwa alikamilisha masharti hayo ya dhamana na kesi imeahirishwa hadi Desemba Mosi, 2015.MWANANCHI
MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO
Home / kitaifa /
siasa /
slider
/ FACEBOOK YAMPONZA YERIKO NYERERE KWA KUPANDISHWA MAHAKAMA YA KISUTU KWA TAARIFA ZA UPOTOSHAJI DHIDI YA UCHAGUZI MKUU 2015.
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment