Mhe Edward Lowassa.
Fidelis Butahe, Mwananchi
Dar es Salaam. Mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowassa na Frederick Sumaye jana walikuwa miongoni mwa makada wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ambao hawakuhudhuria sherehe za kuapishwa kwa Rais John Magufuli.
Ni kawaida kwa mawaziri wakuu wa zamani kuwa sehemu ya wageni rasmi kwenye sherehe hiyo ya kihistoria, lakini jana wawili hao, ambao walitangaza kuihama CCM mwezi Julai na kuhamia kambi ya upinzani, hawakuwamo kwenye jukwaa la wageni rasmi.
Juzi mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema vyama vinavyounda Ukawa havitahudhuria sherehe hizo kwa kuwa vinapinga jinsi uchaguzi ulivyoendeshwa na kuwataka wananchi wapenda mabadiliko na wapenda haki, viongozi na wabunge wa chama hicho kutohudhuria shughuli hiyo.
Ukawa ilimsimamisha Lowassa kugombea urais na kwa mara kwanza mgombea wa upinzani alipata kura milioni 6.07, ambazo ni karibu ya mara tatu ya kura alizopata Dk Willibrod Slaa mwaka 2010.
Hata hivyo, viongozi wa Ukawa walipinga matokeo yaliyokuwa yakitangazwa, wakisema ni tofauti na yale yaliyokusanywa na mawakala wao na kuitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kusitisha utangazaji.
Lowassa, ambaye alikuwa akipeperusha bendera ya Chadema, alikuwa akiungwa mkono na NLD, NCCR-Mageuzi na CUF ambavyo vinaunda Ukawa.
Lowassa alihamia Chadema baada ya CCM kutompitisha kuwa mgombea wa urais, baadaye kundi la makada kutoka CCM lilimfuata, akiwamo Sumaye, Dk Makongoro Mahanga, aliyekuwa Waziri wa Kazi na Ajira, na Kingunge Ngombare-Mwiru, mwanasiasa mkongwe na waziri wa zamani.
Mbowe alisema juzi kuwa sababu kubwa ya Ukawa kususia sherehe hizo ni kutaka kuonyesha nchi na dunia nzima kuwa hawakubaliani na mchakato wa uchaguzi, hasa matokeo ya urais ambayo kwa mujibu wa Katiba ya nchi, mwenyekiti wa NEC akishayatangaza, hakuna mahali pa kuyapinga.
“Watawala wamechezea haki ya Watanzania ya kupiga kura. Kura zimehesabiwa kama karatasi za kawaida tu. Matokeo ya wagombea wetu yamehujumiwa waziwazi.
“Safari hii hujuma hazikuwa kificho. Kila mtu amejionea matokeo yaliyokuwa yanatangazwa na Jaji Lubuva si yale ambayo yalikuwa yamebandikwa vituoni,” alisema Mbowe juzi.
Ukawa pia ililalamikia kile walichoita “mchezo mchafu” waliofanyiwa wagombea wao wa ubunge katika majimbo mbalimbali, ikieleza kuwa walitangazwa washindi ambao hawastahili. Hata hivyo, juzi jioni Naibu Katibu Mkuu wa CUF-Bara, Magdalena Sakaya aliwaeleza wanahabari kuwa hawakuwa wamepata mwaliko wowote wa kuhudhuria sherehe hizo.
Katika hotuba yake fupi ya shukrani, Dk Magufuli aliwashukuru wagombea wenzake wa urais, akisema wamempa changamoto kubwa na amejifunza mengi kutoka kwao na kuwataka wapinzani washirikiane katika kazi ya kuwaletea wananchi maendeleo.
MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment