BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

MSHAMBULIAJI WA TP MAZENGE MBWANA SAMATTA ANYEMELEA KIATU CHA DHAHABU CHA MFUNGAJI BORA LIGI YA MABINGWA AFRIKA.


Mbwana Samatta kushoto.

By Sauli Giliard
Sasa ni dhahiri kwamba Mtanzania anayechezea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Mbwana Ally Samatta anakaribia kutwaa kiatu cha dhahabu kwa ufungaji bora katika ligi ya Mabingwa Afrika.

Akicheza katika mechi ya mkondo wa kwanza wa fainali za Ligi ya Mabingwa Afrika, katika dakika ya 79 ya mchezo, aliangushwa katika eneo la hatari la wenyeji USM Alger ya Algeria, ndipo mwamuzi alipoamuru ipigwe penalti na bila ajizi Samatta alikwamisha mpira kimiani na kuipatia timu yake bao la pili katika ushindi wa 2-1.

Hilo ni bao lake la saba la msimu huu wa ligi ya mabingwa Afrika, idadi sawa na Bakri Al-Madina wa Al-Mekeikh ya Sudan ambaye timu yake imeshatupwa nje ya mashindano hayo yenye utajiri mkubwa zaidi kwa vilabu vya Afrika. Rainford Kalaba aliifungia TP Mazembe katika dakika ya 45 na kuifanya timu hiyo kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa 1-0.

Hata hivyo, mabingwa hao mara nne wa Afrika walilazimika kucheza pungufu kwa muda mrefu baada ya Kalaba kutolewa nje kwa kadi nyekundu. Katika kipindi cha pili, timu hiyo ya DRC ilifanya kila jitihada kuhakikisha kuwa inapata ushindi wa ugenini ili kurahisisha mechi yao ya marudiano.

Dalili zilianza kuonekana dakika ya 66 baada ya El Orfi wa USM Alger alipopewa kadi nyekundu. Dakika chache baada ya TP Mazembe kukosa penalti, nyota Samatta aliingia kwa kasi ndani ya eneo la hatari na kufanyiwa madhambi dakika ya 79.

Mtanzania huyo alipiga penalti hiyo na kuihakikishia matajiri hao wa DRC ushindi. Wenyeji USM Alger walipata bao la kufutia machozi katika dakika ya 87 baada ya Seguer kupiga shuti kali katikati ya mabeki na kumshinda kipa Robert Kidiaba Muteba.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: