SIRI YA USHINDI WA URAIS KWA DK MAGUFULI ZILIFICHULIWA MAPEMA, EDWARD LOWASSA AMEKUWA DARAJA NA KIVUKO KWA CCM KUTAWA KWA MIAKA MITANO 2015-2020.
Rais Mteule wa Tanzania, Dk John Joseph Pombe Magufuli
By Julius Mathias, Mwananchi
Oktoba ni mwezi wa kihistoria kwa Watanzania katika mwaka 2015 kutokana na ukweli kwamba watanzania wamepiga kura kuchagua rais, wabunge na madiwani.
Uchaguzi umefanyika Jumapili iliyopita ukiwa wa tano tangu kufanyika wa kwanza mwaka 1995 katika mfumo wa vyama vingi uliorejeshwa nchini mwaka 1992.
Bila shaka ni uchaguzi uliokuwa na mvutano mkubwa zaidi tangu mwaka 1995, hasa kutokana na ushindani uliopo baina ya vyama vya siasa hasa CCM kinachotawala na Muungano wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) unaojumuisha vyama vya Chadema, CUF, NLD na NCCR-Mageuzi.
Kutokana na ukweli huo, baadhi ya wachambuzi na wanasiasa waliamini safari hii upinzani ungekuwa na nafasi kubwa ya kuing’oa CCM, chama kinachotajwa kuwa kikubwa zaidi, chenye nguvu na mpangilio mzuri barani Afrika.
Hilo limeufanya uchaguzi wa Oktoba 25 kuvuta hisia za wengi hata mataifa ya kigeni lakini Ukawa wakadondokea pua. Mjumbe wa timu ya kampeni za CCM, January Makamba
Hata hivyo, mjumbe wa timu ya kampeni za CCM, January Makamba alisema kuwa kwa matokeo ya tafiti zisizo na shaka na mbinu za kimataifa za kampeni zilizotumiwa na chama chake mwaka huu, isingewezekana matokeo kuwa tofauti, zaidi ya Dk John Magufuli kuchaguliwa kura rais wa tano wa Tanzania.
Kabla ya Uchaguzi.
Kupitia mtandao wa Mail & Guardian Africa wa nchini Zambia juma lililopita, Makamba aliandika sababu 10 zinazomhakikishia Magufuli kuibuka na ushindi wa urais katika uchaguzi huo.
Zifuatavyo ni sababu nane zilizoainishwa na Makamba ambaye pia ni msemaji wa timu hiyo ya kampeni za urais za CCM kama anavyokaririwa na mwandishi wa gazeti hili.
1. Kasoro za Edward Lowassa
Anasema licha ya kushinda kwenye chaguzi zote za vyama vingi tangu mwaka 1995, uchaguzi wa mwaka huu ulionekana kuwa mgumu kwa CCM kutokana na mgombea wa awali wa upinzani.
“Lakini upepo wa ushindi uligeukia upande wa CCM baada ya upinzani kumtangaza Edward Lowassa kuwa mgombea wao mwezi Agosti, bila kupigiwa kura ndani ya vikao vya chama.
“Alionekana maarufu akiwa mmoja wa waliotajwa kuweza kupenya kwenye uteuzi wa CCM kuwania urais kabla kushindwa kwenye uchaguzi ndani ya chama, huku ni kutoaminika na huu ndiyo ukweli.
Ni rahisi kwa CCM kushinda dhidi ya Lowassa kuliko ingekuwa dhidi ya Dk Wilbrod Slaa aliyetarajiwa kuwania mwaka huu lakini akawekwa kando na Lowassa kupewa nafasi hiyo,” anasema Makamba.
Anaeleza kwamba Slaa anaheshimika na kukubalika kwa uaminifu wake na kwa sababu hiyo hoja anazowasilisha huwa na nguvu, lakini Lowassa hana uwezo huo na ndiyo sababu CCM haikumteua kuwania urais kwani hawezi kuleta mabadiliko kutokana na historia yake.
“Wapo wanaoamini uchaguzi huu ni mgumu kwa CCM kwa sababu Lowassa anagombea kupitia upinzani. Tunaamini uchaguzi ungekuwa mgumu kwetu kama Lowassa angekuwa mgombea wetu,” anasema.
2. Upinzani kuitupa hoja ya ufisadi
Akifafanua hoja hiyo, Makamba anasema miaka 10 iliyopita kulikuwa na matukio mengi ya rushwa na ufisadi yaliyofikishwa mahakamani, kutangazwa na vyombo vya habari, asasi za kiraia hata Bunge kupambana nayo kuyafichua huku Rais Jakaya Kikwete akiweka historia ya kupambana na hali hiyo kwa kumuagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuwa wazi kwa jamii na kujadiliwa na Bunge.
Anasema katika kipindi hicho pia Lowassa alilazimishwa kujiuzulu uwaziri mkuu kwa sababu ya kashfa ya rushwa na iliyogonga mijadala ya Bunge wakati huo pia vyombo vya habari na wananchi wameamka kwani rushwa haikubaliki.
Hali hiyo ilisababisha Lowassa kutokubalika kwa wananchi huku wapinzani wakitumia jina lake katika mapambano ya ufisadi wakimtaja kama mtuhumiwa.
Anasema katika orodha ya mafisadi iliyotolewa na upinzani mwaka 2007, Lowassa alikuwa mmoja wa waliotajwa vinara.
3. Mabadiliko
Makamba anasema hija hiyo ilianzia CCM na kwenda nje ya chama hicho hata kubebwa upinzani kwa kasi na kishindo.
Anasema kuwaona Lowassa na Frederick Sumaye ni kitu kikubwa katika siasa za Tanzania wakiwa upande wa upinzani kwani kabla ya Agosti walikuwa ndani ya CCM na walichukua fomu za kuomba kugombea urais. Hata hivyo, wakiwa ndiyo wasemaji wakuu kwenye kampeni za upinzani kwa sasa ni vigumu kuwaaminisha watu wale wale kwamba yale mema waliyohubiri juu ya CCM siku chache zilizopita yalikuwa ni uongo.
“Hayawezi yakabadilika ndani ya muda mfupi wa kuondoka kwao,” anasema.
4.Kutoafikiana ndani ya Ukawa
Anasema licha ya makubaliano ya kusimamisha mgombea mmoja kuanzia urais mpaka udiwani, bado vyama vyote vinne vilishindwa kuafikiana juu ya majimbo 12 na baadhi ya kata. Kwenye baadhi ya majimbo wagombea wote waliojitokeza walilazimika kupanda jukwaani na kupigiwa kura na mgombea urais ili kutoa nafasi kwa wananchi kuamua nani wanamtaka. “Hii ni fursa kwa CCM kutetea majimbo hayo.” anasema Makamba.
Anasema mpango wa kuwa na mgombea mmoja wa urais ulikuwa na dhamira nzuri kabla Lowassa hajajiunga Ukawa, lakini kuja kwake na kuondoka kwa Dk Wilbrod Slaa na Profesa Ibrahimu Lipumba ni kete ambayo itasaidia kuivusha CCM.
5. Matumizi ya chopa
Makamba anataja kujaza watu wengi kwenye kampeni zake hasa maeneo ya mjini ambako ndiko mara nyingi hufanyika, matumizi ya helikopta (chopa) hivi karibuni vinaweza kupunguza nafasi ya Lowassa kupata kura nyingi.
Anasema hiyo inatokana na ukweli kwamba wananchi wengi hawapati nafasi ya kukutana naye tofauti na mpinzani wake mkuu, Dk Magufuli ambaye aligoma kufanya hivyo aliposhauriwa.
“Kwa haraka haraka, Lowassa anakubalika sana kwenye miji mingi mikubwa ambako amefika, lakini takwimu za nchi hii zinaonyesha wananchi wengi wanaishi vijijini. Hii inaweza ikamaanisha kwamba mgombea huyu anaweza akapata ushindi mjini na akashindwa vibaya vijijini,”anasema.
6. Siasa za kujuana
Anasema CCM inajivunia uwezo wake wa kuwa na siaa za kimtandao ambao unazingatia kwa kiwango kikubwa kujuana miongoni mwa makada wake. Pamoja na ukweli kwamba Lowassa anajaza watu wengi kwenye mikutano yake, wajuzi wa mambo wanasema hiyo si hoja ya msingi.
Makamba anabainisha, idadi ya wanachama wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) ndani ya CCM pekee ni kubwa kuliko Wanachadema wote nchini na kwamba mara nyingi chama chake kinafanya mambo nje ya macho ya vyombo vya habari tofauti na wapinzani.
Anasema hilo linadhihirishwa na uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambao CCM ilishinda kwa asilimia 80 licha ya Ukawa ulioonekana kuwa na nguvu kubwa wakati huo.
7. Magufuli
Makamba anasema kuanzia kuchukua fomu mpaka kupitishwa ndani ya chama hakuna aliyemtegemea kushinda tiketi hiyo. Ni waziri asiye na historia kubwa kuwazidi baadhi ya makada aliokuwa anashindana nao ndani ya chama.
Anasema kabla hajapitishwa hakuna mchambuzi yeyote wa ndani na hata kimataifa aliyempa kipaumbele. “Ni kama ilivyokuwa kwa Benjamin Mkapa mwaka 1995 ambaye baada ya kupitishwa alishinda Uchaguzi Mkuu.
Magufuli alishindana na mawaziri wakuu wastaafu wote wawili’; Lowassa na Sumaye ndani ya CCM, na kuibuka kidedea. Haitakuwa ajabu endapo hilo litaendelea kwenye Uchaguzi Mkuu,” anasema.
8. Tafiti
Anasema tafiti mbili zimeibeba CCM. Twaweza na Ipsos-Synovate wamesema chama hicho kitashinda kwa zaidi ya asilimia 62.
“Ingawa baadhi ya watu wanabeza matokeo ya tafiti hizo, wataalamu wanasema utafiti hupingwa na utafiti mwingine. Matokeo yanaweza yakaendelea kubaki kama yalivyo,” anasema.
0 comments:
Post a Comment