CCM YAZIDIWA UJANJA KATIKA UCHAGUZI WA UBUNGE JIMBO LA ARUSHA MJINI MBELE YA CHADEMA.
Mbunge Mteule wa Arusha Mjini, Godbless Lema
WAKATI Chama Cha Mapinduzi (CCM), kikirejesha kiti chake cha ubunge katika Jimbo la Handeni Mjini mkoani Tanga, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimetetea kiti chake cha Arusha Mjini huku CCM ikilalamika kuwapo kwa hujuma katika jimbo hilo.
Katika Jimbo la Handeni Mjini, mgombea wa CCM, Omari Kigoda alishinda kwa kuwabwaga wapinzani wake wanne kutoka vyama vya siasa vya TLP, CUF, ADC na Chadema, akipata kura 10,315 sawa na asilimia 75.90 ya kura 13,591 zilizopigwa huku kura 214 zikiharibika.
Akitangaza matokeo hayo juzi usiku, Msimamizi wa Uchaguzi huo mdogo, Kenneth Haule alisema wagombea wengine akiwemo Doyo Hassan wa ADC alipata kura 184 (1.35%), Kilo Daudi wa Chadema kura 648 (4.77%), Remmy Shundi wa CUF kura 2,419 (17.80%) na Makame Bakari wa TLP kura 19 (asilimia 0.14).
Mbunge huyo mteule, Kigoda ambaye anarithi mikoba ya baba yake, Dk Abdallah Kigoda aliyeiongoza Handeni kwa miaka 20 kabla ya kifo chake mapema Oktoba na kusababisha uchaguzi wa Oktoba 25, uahirishwe akiwa tayari ameteuliwa na Tume, aliwataka wananchi kumpa ushirikiano wa dhati katika majukumu yake hayo.
Mkoani Arusha, Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Arusha Mjini, Juma Iddy alimtangaza mgombea ubunge wa Chadema, Godbless Lema kuwa mshindi wa kiti hicho, baada ya kupata kura 68,848 (sawa na asilimia 68.54) na kumwangusha vibaya mgombea wa CCM, Philemon Mollel aliyepata kura 35,907 (34.76%).
Mgombea wa ACT Wazalendo, Naravoi Mollel aliambulia kura 342, mgombea wa CUF, Zuberi Zuberi alipata kura 106, huku NRA kupitia Rashid Mkama ikipata kura 43 na kushika mkia katika uchaguzi huo ulioahirishwa kutokana na kifo cha aliyekuwa mgombea wa ACT – Wazalendo, Estomil Mallah.
Akizungumzia matokeo hayo, mgombea wa CCM, Mollel maarufu kwa jina la Monaban alidai matokeo hayo yamechakachukuliwa, huku pia akiwatuhumu baadhi ya viongozi wa CCM wa Jimbo la Arusha kushiriki kumhujumu hatua ambayo imemsikitisha.
Alisema amesikitishwa baadhi ya mawakala wake kufukuzwa katika vituo vya kupiga kura na viongozi wa chama kushindwa kuchukua hatua madhubuti pale matukio ya hujuma yaliyokuwa yakifanyika katika vituo vya kura.
Uchaguzi Mdogo wa Handeni Mjini na Arusha Mjini ni wa tano kufanyika baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu. Tayari umefanyika katika majimbo ya Lushoto, Ulanga Mashariki na Lulindi, na umebaki katika majimbo ya Masasi mkoani Mtwara, Ludewa mkoani Njombe na Kijitoupele mjini Unguja.HABARILEO
0 comments:
Post a Comment