MBUNGE WA JIMBO LA UBUNGO SAID KUBENEA AONJA JOTO YA KIBURI, BAADA YA KUMUITA MKUU WA WILAYA WA KINONDONI KIBAKA,
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda (mwenye fulana ya mistari) akimsikiliza mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea (wa kwanza kulia) wakati walipokuwa kiwanda cha nguo cha Tanzania Tooku kujaribu kutatua mgogoro wa wafanyakazi kabla ya kutofautiana na Makonda kuamuru mbunge huyo kukamatwa na polisi jana. Picha na Venance Nestory
Dar es Salaam. Mbunge wa Ubungo (Chadema), Said Kubenea amekamatwa na polisi kwa amri ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni mkoani Dar es Salam, Paul Makonda baada ya kudaiwa kurushiana maneno wakati wakitatua mgogoro wa wafanyakazi wa Kiwanda cha ushonaji na usafirishaji wa nguo, Tooku.
Viongozi hao walitofautiana kauli baada ya Makonda kudaiwa kumkatalia Kubenea kuzungumza na wafanyakazi hao.
Akizungumza na gazeti hili akiwa Kituo cha Polisi Magomeni ambako alikuwa akishikiliwa, Kubenea alisema alikuwa wa kwanza kufika kiwandani hapo na kuzungumza na wafanyakzi hao na baadaye uongozi na wakati wako katika majadiliano, Makonda aliingia.
“Nilimwelezea tulipofikia na baadaye akasema anataka kuzungumza na wafanyakazi, lakini alitaka kumaliza mkutano bila kunipa nafasi. Nilimuuliza, mbona hunipi nafasi, akasema mimi ni nani, yeye ndiyo mkuu wa wilaya, tukabishana na mimi nikamwambia ‘wewe ni kibaka tu,” alidai Kubenea.
kizungumzia suala hilo, Makonda alidai kuwa mbunge huyo alionekana kutofahamu taratibu za kutatua migogoro na nguvu aliyonayo mkuu wa wilaya kutokana na ugeni wa kazi ya ubunge.A
Makonda alisema alipofika alifanya kikao cha ndani na uongozi wa kiwanda na kuhudhuriwa na Kubenea ambaye baadaye alizungumza na wafanyakazi hao.
“Lakini wakati nawasikiliza wafanyakazi, Kubenea alitaka naye kuongea, ile haikuwa nafasi yake kwa kuwa alishawasikiliza, lakini aling’ang’ania kutaka kuzungumza,” alidai Makonda.
Alidai baada ya Kubenea kuona hajapatiwa nafasi ya kuzungumza, alianza kumrushia matusi jambo ambalo halikumfurahisha, hivyo kuamuru polisi kumkamata na kumhoji kwa matusi hayo.
Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Camilius Wambura alipoulizwa kuhusiana na suala hilo, alisema walikuwa wanaendelea kumhoji mbunge huyo pamoja na watu wengine.
Hii ni mara ya pili kwa Makonda kuamuru kuswekwa rumande kwa viongozi baada ya baadhi ya maofisa wa ardhi wa Manispaa ya Kinondoni kuchelewa kufika kwenye utatuzi wa mgogoro wa ardhi Kata ya Wazo.MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment