Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete na mkewe Mama Salma wakifanya usafi katika soko kuu la Chalinze mkoani Pwani jana.
Alisema jambo hilo halimnyimi usingizi kwa sababu halina ukweli, bali lina lengo la kumchafua.
Kikwete alitoa kauli hiyo jana muda mfupi baada ya kushiriki usafi kwenye maeneo mbalimbali ya mji wa Chalinze, Pwani katika kuitikia wito wa Rais John Magufuli wa kufanya usafi badala ya shamrashamra za miaka 54 ya Uhuru.
Kikwete, ambaye ametoa kauli hiyo kwa mara ya kwanza tangu ang’atuke mwezi uliopita, alidai amekuwa akitajwa na vyombo hivyo kuwa yeye na familia yake walikuwa karibu na baadhi ya wafanyabiashara wakubwa wanaoelezwa kukwepa kodi.
Alisema wale wanaomtuhumu kwa kigezo hicho wanapoteza muda wao bila faida na akasisitiza kuwa ni vyema waendelee kumshutumu yeye, lakini wasimseme Rais Magufuli.
“Sikuwahi kutoa agizo kwa mtu yeyote anayepaswa kulipa kodi eti asilipe, hao wanaosema wanastarehesha baraza, wanapoteza wakati wao.
“Mwingine kasema, ‘hachomoi, mie nimechomeka nini, sijachomeka chochote kwa hiyo sina cha kuchomoa,” alisema Kikwete.
Aliongeza, “kuna wengine wanasema kuwa familia yangu ilihusika, siamini, kama mimi nilihusika, sikuwahi kutoa agizo kuwa mtu asilipe, hata mke wangu (Salma) pia, hawezi na hata mwanangu Ridhiwani, sidhani kama anaweza kufanya hivyo,” alisema.
Alisema, “lakini wale wanaokwepa kodi hawataacha kirahisi. Wataendelea, lakini viongozi wakati wote waendelee kupambana na ndiyo maana mapambano haya lazima yaendelee, tutamuunga mkono Rais (Magufuli) kupambana.”
Alisema katika kuboresha mapato ya Serikali, wakati anaingia madarakani mwaka 2005, mapato yalikuwa Sh177 bilioni na wakati akimaliza utawala wake ilifikia Sh900 bilioni.
0 comments:
Post a Comment