Na Juma Mtanda, Mwananchi.
Umoja wa viongozi wa dini mkoa wa Morogoro umeandaa tamasha la matumini kwa kizazi kipya ikiwa na lengo la kuunganisha nguvu za jamii kupinga matumizi ya madawa ya kulevya huku mbunge wa jimbo la Morogoro mjini, Abdulaziz Abood akitarajia kuwa mgeni rasmi litakalofanyika Desemba 20 mkoani hapa.
Wakizungumza na waandishi wa habari mjini hapa, Mwenyekiti tamasha hilo, Mchungaji Peter Denis alieleza kuwa tamasha hilo lina lengo la kuunganisha nguvu za jamii kupinga matumizi ya madawa ya kulevya na mbunge wa jimbo la Morogoro atakuwa mgeni rasmi.
Denis alisema kuwa umoja wa viongozi wa dini ikishirikaiana na Beula Communications inaandaa tamasha hilo ili kufikisha ujumbe wa kutangaza matumaini kwa walioathirika na dawa za kulevya pamoja na kufanya harambee ya kuchangisha fedha za kujenga kituo cha kuwapokea na kuwashauri watu walioathirika na dawa za kulevya.
“Desemba 20 kutakuwa na tamasha la matumaini kwa kizazi kipya mkoa wa Morogoro na lengo la tamasha hilo kwanza kupata fedha za kuanza ujenzi wa kituo cha kuwapokea na kuwashauri watu walioathirika na dawa za kulevya na tunataka jamii iunganishe nguvu na sisi kupinga matumizi ya dawa za kulevya.”alisema Denis.
Mratibu wa tamasha hilo, Melkezedek Mutta alisema kuwa siku ya tamasha hilo kutakuwa na burudani za aina mbalimbali wakiwemo wasanii wa kizazi kipya Saida Kaloli, Kingwendu, kaswida na kwaya.
Melkezedek alisema kuwa kutakuwa na harambee ya kuchangisha fedha kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho huku wananchi wakiombwa kuungwa mkono kwa kulipia viingio kuanzia kiasi cha sh 10,000 kwa watu wa VIP, watu wa kawaida Sh 5,000 na watoto sh 1,000.
Katibu mkuu wa Bakwata mkoa wa Morogoro, Hamisi Zuberi alitoa ushuhuda namna dawa za kulevya namna zinavyoathiri akili ya mtumiaji, aliwaeleza waandishi wa habari kuwa enzi za ujana wake aliwahi kutumia kilevi lakini athari yake ilikuwa kubwa kutokana na kufanya mambo yanayopingana na jamii.
Zuberi alisema kuwa madawa ya kulevya kimsingi yanapaswa kupigwa vita kwa ngazi zote kuanzia serikali kuu hadi ngazi ya kijiji kwani yamekuwa na athari kubwa katika jamii.
Kwa mujibu wa takwimu za umoja huo, kata zilizokumbwa na vijana wake kujiingiza katika utumiaji wa madawa ya kulevya ndani ya Manispaa ya Morogoro ni pamoja na kata ya Chamwino, Mwembesongo eneo la Msamvu na Manzese kata ya Mafiga.
0 comments:
Post a Comment