KASHFA ZA RUSHWA NA WIZI ZAWAFUKUZISHA KAZI KAZI MAOFISA WAANDAMIZI SABA WA SHIRIKA LA UMEME TANZANIA (TENESCO)
Siku chache baada ya moto wa Serikali ya Awamu ya Tano, Rais Dk. John Magufuli kuwachukulia hatua wabadhilifu wa mali za umma wa Bandarini na TRA, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), limewafukuza kazi maofisa waandamizi saba kwa kashfa mbalimbali za rushwa, wizi na ubadhirifu wa mali za shirika hilo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Felchesmi Mramba, jana jijini Dar es Salaam aliweka wazi hatua zilizochukuliwa na shirika hilo baada ya uchunguzi kukamilika na kubaini uhusika wao kwa namna moja au nyingine na baadhi wameshapandishwa mahakamani.
Mramba alisema watumishi hao wamefukuzwa kazi kwa kipindi cha miezi miwili kutokana na makosa mbalimbali ikiwamo wizi na ubadhirifu na wamo waliofikishwa mahakamani mkoani Kagera juzi.
Alitaja vyeo vya walioachishwa kazi kuwa ni mameneja wa mikoa, wahandisi na wahasibu wa mikoa ya Kagera, Katavi, Ilala, Shinyanga na Kinondoni Kaskazini. “Ukiacha kero zinazosababishwa na miundombinu, Tanesco inachukua hatua madhubuti za kuwaadabisha wafanyakazi wake wanaotoa huduma mbaya na kuwa kero kwa wateja.
Baadhi ya kero kudaiwa rushwa kabla ya kupewa huduma, kucheleweshewa huduma na ubadhirifu,” alisema Mramba. Aidha, alisema shirika hilo litaimarisha hatua hizo ili mfanyakazi yeyote atakayebainika analaghai, anadai rushwa, anatoa lugha chafu au huduma mbovu, atawajibishwa mara moja na pale atakapobainika ataachishwa kazi.
KUDHIBITI WIZI WA UMEME
Mkurugenzi huyo alisema Shirika linaendelea na kampeni maalum katika mikoa yote ya kuwakamata wezi wa umeme na kuwachukulia hatua kali pamoja na hatua nyingine kubwa na wezi wa umeme kutangazwa hadharani na kufunguliwa mashitaka.
“Ni rai yangu kwa yeyote anayejihusisha na wizi wa umeme ajisalimishe kwa kwenda kwa meneja wa mkoa na kama hawatajisalimisha kwa hiari, hatua zilizokusudiwa dhidi yao zitachukuliwa pasipo huruma yoyote,” alisisitiza.
Aidha, Tanesco imetoa siku saba kwa wateja wanaojua kwamba mita zao zimechezewa kujisalimisha na ikiwa kinyume shirika lisilaumiwe kwa hatua zitakazochukuliwa.
MIUNDOMBINU
Mramba alithibitisha kuwapo kwa kero ya kukatika umeme mara kwa mara ambako kunasababishwa na uchakavu wa miundombinu kwa kuwa baadhi ni ya siku nyingi wakati matumizi ya umeme yameendelea kuongezeka kwa kasi.
Alisema vituo vingi vya umeme vilijengwa katika miaka ya 80 na 90 wakati wakazi wa Jiji la Dar es Salaam walikuwa chini ya milioni tatu na sasa ni zaidi ya milioni tano, hivyo miundombinu iliyopo imeelemewa.
Mramba alisema jitihada za kurekebisha hali hiyo zinaendelea kwa kuwa na miradi mikubwa inayoendelea na utapunguza tatizo hilo.
Alitaja baadhi ya miradi hiyo inayotekelezwa kuwa ni pamoja na wa Kusini mwa Dar es Salaam kwa ufadhili wa Benki ya Dunia utakaoboresha umeme maeneo ya Kigamboni, Kurasini, Mbagala, Mkuranga, Kisarawe, Gongo la Mboto, Ukonga, Kitunda, Vingunguti na Tabata.
Alitaja miradi mingine inayotekelezwa kwa ufadhili wa Serikali ya Japan itakayosaidia kuondoa tatizo la umeme katika maeneo ya Muhimbili na Upanga, Mwananyamala na Kinondoni, Oysterbay na Masaki, Jangwani, Bahari Beach na Mbezi Beach.
Mingine ni unaotekelezwa kwa mkopo kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (ABD) unaoendelea katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Shinyanga na Geita.
Mwingine ni unaofadhiliwa na Serikali ya Finland ambao utasaidia kuimarisha umeme katikati ya Jiji la Dar es Salaam na kusaidia kuimarisha umeme kwenye maeneo yenye majengo marefu ya Samora, Azikiwe, Kariakoo na Sea View.
Aidha, alibainisha mradi mkubwa wa kupeleka umeme wa kilovoti 400 kutoka Iringa kupitia Mtera, Dodoma, Singida hadi Shinyanga uko kwenye hatua za mwisho za kukamilika na hivyo kuwa na umeme wa uhakika Kanda ya Ziwa. Mramba alisema kazi ya kuunga Songea kwenye Gridi ya Taifa kutokea Makambako kwa kilovoti 220, inaendelea na mkandarasi yuko kazini.
Pia alisema kazi ya kuunga Tanzania na Kenya kwa umeme wa kilovoti 400 inatarajiwa kuanza hivi karibuni kwani zabuni za kumpata mkandarasi ziko katika hatua za mwisho na ujenzi utaanza mwakani. Mramba alitaja miradi mingine ambayo itaanza hivi karibuni kuwa ni Dar es Salaam –Somanga wa kilovoti 400 na Bulyankhulu-Geita-Nyakanazi-Rusumo wa kilovoti 220.
“Miradi hii ikikamilika, itasaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la kukatika kwa umeme kutokana na mfumo wa usambazaji,” alifafanua. CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment