Mwenyekiti wa chama cha soka mkoa wa Lindi, Francis Kumbandulane (wa pili kutoka kushoto) akinyanyua kofia juu sambamba na wahitimu wenzake mara baada ya kutunukiwa shahada ya uzamili katika sayansi ya uhasibu na fedha wakati wa mahafali ya 14 ya chuo kikuu cha Mzumbe yaliyofanyika chuoni hapo mwishoni mwa juma mkoani Morogoro.
Na Juma Mtanda, Mwananchi.
Mwenyekiti wa chama soka mkoa wa Lindi, Francis Kumbandulane amefichua mipango ya klabu ya Kariakoo Sport Club inayoshiriki ligi daraja la pili na kuwa klabu hiyo itakuwa miongoni mwa timu zitakazopanda daraja na kucheza ligi daraja la kwanza msimu ujao.
Akizungumza na gazeti hili mara baada ya kutunukiwa shahada ya uzamili katika sayansi ya uhasibu na fedha katika mahafali ya 14 ya chuo kikuu cha Mzumbe mkoani hapa, Kumbandulane alisema kuwa klabu ya Kariakoo Lindi imeweka mipango kabambe ya kuwepo kati ya moja ya timu nne zitakazofuzu na kuingia ligi daraja la kwanza msimu ujao.
Kumbandulane alifichua mipango hiyo kuwa, wanajivunia kuwa na kikosi bora ligi daraja la pili kinachowapa imani kufanya vizuri na kuwepo kati ya timu nne zitakazofuzu kutinga ligi daraja la kwanza na umoja, mshikamano kuanzia uongozi wa serikali ya mkoa na wilaya.
“Nikueleze tu mwandishi, Kariakoo ya Lindi itafanikiwa kucheza ligi daraja la kwanza msimu ujao kwani nina imani kubwa ya kuwepo kati ya timu nne za juu zitakazotinga ligi daraja la kwanza msimu ujao.”alisema Kumbandulane.
Kariakoo Lindi tayari imecheza michezo miwili katika ligi daraja la pili na kupata pointi mbili baada ya sare mbili.
Kumbandulane ambaye ni Mhasibu wa wakala wa barabara mkoa wa Lindi (Tanroad) alisema kuwa timu ya Kariakoo ya msimu huu inataka kurejesha makali ya mwaka 2003 na mwaka 2010 wakati wa utawala wa mkoa huo Abubakari Mgumila.
Mwaka 2003 timu ya Kariakoo Lindi ilifanikiwa kucheza fainali za kombe la afrika mashariki la Hedex Cup lakini walipoteza mchezo huo kwa kufungwa na Express ya Uganda kwa kufungwa na kuishia nafasi ya pili.
“Kariakoo hii tunataka kuirejesha makali yake ya mwaka 2003 tulipoishia nafasi ya pili baada ya kufungwa na Express ya Uganda katika fainali ya Hedex Cup lakini mwaka 2010 nusura tutwae kombe la taifa Cup kama sio mizengwe ya soka kwa kufungwa na Singida kwa bao 3-1 katika mchezo wa fainali”alisema Kumbandulane.
Mwenyekiti huyo aliwataka wadau wa soka mkoa wa Lindi kuisaidia kwa hali na mali timu ya Kariakoo Lindi ili kufanikisha malengo yake kwani upande wa serikali umeonyesha kuiunga mkono timu hiyo.
0 comments:
Post a Comment