Dar es Salaam. Hatua ya Rais John Magufuli kuteua na kuwaapisha mawaziri watatu kabla ya kuapishwa kuwa wabunge, imeibua utata huku wanasheria wakihoji jinsi gani watafanya kazi za Kamati za Bunge kabla ya Februari wakati chombo hicho cha kutunga sheria kitakapoanza shughuli zake.
Kwa mujibu wa ibara ya 66 (1) ya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano, Rais ana mamlaka ya kuteua wabunge wasiozidi kumi ambao anaamini wanaweza kumsaidia katika utekelezaji wa majukumu yake.
Na ibara ya 55 (4) inamuelekeza Rais kuteua mawaziri kutoka miongoni mwa wabunge.
Kwa kutumia mamlaka hayo, Alhamisi iliyopita Rais Magufuli aliwateua makada watatu kuwa wabunge na hapo hapo kutangaza kuwateua kuwa mawaziri na kisha kuwaapisha juzi kutumikia wadhifa huo.
Mawaziri hao ni Profesa Makame Mbarawa ambaye ameteuliwa kuwa Wazira wa Maji na Umwagiliaji, Dk Abdallah Possi (Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu-Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu), na Balozi Augustine Mahiga ambaye anakuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa.
Kuteuliwa kwao kunafanya jumla ya wabunge walioteuliwa na Rais hadi sasa kuwa wanne baada ya kumteua Dk Tulia Ackson mwezi uliopita kabla ya naibu mwanasheria mkuu huyo wa zamani kugombea nafasi ya Naibu Spika wa Bunge.
Hata hivyo, Dk Tulia aliapishwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai kabla ya kugombea nafasi ya unaibu spika na kushinda na kuapishwa kabla ya kuanza kutekeleza majukumu yake.
Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu alisema hapo kuna tatizo la kisheria kwa kuwa mawaziri wote huteuliwa kutokana na nafasi zao za ubunge na kwamba kiapo cha ubunge ndiyo kinamtambulisha mbunge kabla ya kutambuliwa kuwa waziri.
Lissu alisema endapo shughuli za Kamati za Bunge za Kudumu zitaanza vikao vyake siku chache zijazo kabla ya mkutano wa Bunge, waziri anayehusika kwenye kamati yake hatatambuliwa licha ya kuwa kiongozi wa Serikali anayetakiwa kujibu hoja za wizara yake.
“Kwa mfano, Balozi Mahiga atahitajika kuwa mjumbe wa Wizara ya Mambo ya Nje, sasa ataingiaje bila kuwa na kiapo cha kuwa mbunge? Je, hawataenda kushiriki? Kama hawataenda, itakuwaje kwa sababu hata kanuni zinasema huwezi kutambuliwa wala kufanya kazi za kibunge bila kula kiapo,” alisema Lissu.
Kauli ya Lissu iliungwa mkono na mwenyekiti wa zamani wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Jaji Amir Manento kuwa waziri aliyeapishwa bila kula kiapo cha Bunge hawezi kutambuliwa na Bunge hilo.
Jaji Manento alisema Spika hatakuwa na uwezo wa kumpangia kazi zozote za kibunge hadi atakapokula kiapo. Kwa hiyo alisema mawaziri walioapishwa kabla ya kiapo hicho hawatambuliwi na Bunge.
“Inawezekana Rais alishawateua mapema katika kipindi cha ukimya wake wa mwezi mmoja na kuwasiliana na ofisi za Bunge, bila kupata taarifa hiyo, yaani ofisi ya Bunge ikawatambua tu licha ya kutotambuliwa kwa kiapo, lakini bado kuna utata katika suala hilo la kiapo, sawa na mchezo wa yai na kifaranga nani aliyeanza,” alisema Jaji Manento.
Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah alisema mawaziri hao hawawezi kujihusisha na shughuli zozote za Bunge bila kula kiapo.
Alisema mawaziri hao watakuwa na nafasi ya kufanya shughuli zote zinazowahusu kama mawaziri, lakini hawatakuwa na nafasi ya kupewa majukumu ya kibunge kabla ya kula kiapo.
“Jambo la pili, mawaziri hao wanaweza kuwa na nafasi ya kushiriki kwenye Kamati za Bunge lakini hawatakuwa na nafasi ya kupiga kura kama kanuni za Bunge zinavyobainisha. Anaweza kuingia na kusikiliza au kufuatilia mjadala tu kwenye kamati hizo,” alisema huku akitoa mfano kuwa jambo hilo si mara ya kwanza kutokea.
“Profesa (Sospeter) Muhongo aliteuliwa kuwa mbunge na kuapishwa waziri wakati Kamati za Bunge zikianza vikao vyake, lakini hakuwa ameapa kuwa mbunge kwa hivyo aliingia na kufuatilia vikao, lakini hakuwa na haki ya kupiga kura.”
Katika ufafanuzi huo, Dk Kashililah alisema mawaziri hao hawataweza kushiriki mjadala ya miswada au hoja zilizowasilishwa ndani ya kamati hizo.
“Na ndiyo maana Bunge litakapoanza tu, wanaanza kula kiapo kwanza kwa sababu kanuni za Bunge zinaagiza hivyo,” alisema.
Ibara ya 56 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano inaongeza utata zaidi katika suala hilo kutokana na kumzuia mtu yeyote anayeteuliwa kuwa waziri, kutekeleza majukumu yake kabla ya kula viapo vyote vilivyopo kisheria.
Ibara hiyo inasema: “Waziri au naibu waziri hatashika madaraka yake ila mpaka awe ameapa kwanza mbele ya Rais kiapo cha uaminifu na pia kiapo kingine chochote kinachohusika na utendaji wa kazi yake kitakachowekwa kwa mujibu wa Sheria iliyotungwa na Bunge.”
Mara baada ya kuapishwa Desemba 12, Dk Mahiga alielekea moja kwa moja ofisi za wizara yake kuanza rasmi kazi.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue hawakupatikana jana kuzungumzia suala hilo.
Kafulila amvaa Muhongo
Wakati huohuo, aliyekuwa mbunge Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila amesema uteuzi wa Profesa Muhongo umedhihirisha kuwa Serikali ya Awamu ya Tano haina nia ya dhati ya kupambana na ufisadi.
“Rais Magufuli alisema Serikali yake ni ya kutumbua majipu, lakini ni jambo la kushangaza kuona anaingiza mengine kwenye baraza lake, haeleweki,” alisema Kafulila alipozungumza na Mwananchi jana kuhusu uteuzi huo.
Kafulila, ambaye alikuwa kinara wa sakata hilo, alisema Profesa Muhongo ambaye alikuwa Waziri wa Madini na Nishati wakati fedha hizo zikichotwa, aliisababishia Serikali hasara ya mabilioni ya fedha.
“Nimeshangaa kuona mtu kama Profesa Muhongo aliyevunja Sheria ya Fedha ya mwaka 2012, Kifungu cha 29 na kusabisha hasara kubwa ameteuliwa kuwa waziri, tena wa wizara ile ile,” alisema.
Alisema asilimia 70 ya Sakata la Escrow bado haijaisha. Alidai kuwa Benki ya Stanbic ambayo ilishiriki kupokea na kutakatisha fedha zilizotolewa kutoka akaunti hiyo bado mambo hayajamalizika, hata maazimio yaliyofikiwa na Bunge la 10 Novemba mwaka jana kuhusu sakata hilo bado hayajatekelezwa yote.
Moja ya maazimio hayo ni mamlaka husika kutengua uteuzi wa mawaziri walioguswa na sakata hilo, akiwamo Profesa Muhongo ambaye alitangaza kujiuzulu mapema mwaka jana.
Hata hivyo, Katibu wa Bunge Dk Thomas Kashililla alisema baada ya Bunge la 10 kuvunjwa, shughuli zote za Bunge hilo zilikoma.
“Kama kuna hoja yoyote ya kuibua hoja za Bunge lililopita, zinatakiwa zianze upya kwa kufuata taratibu wa Bunge jipya la 11,” alisema Dk Kashililla.
Hata hivyo, Ikulu ilitangaza Mei mwaka jana kuwa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma imebaini kuwa Profesa Muungo hakufanya vitendo vyovyote vya ukiukwaji wa maadili katika sakata hilo. BBC
MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO
Home / magazeti /
slider
/ MAWAZIRI WATATU WA RAIS MAGUFULI WAZUA UTATA KUTOKANA NA KUSHINDWA KUPITIA BUNGENI
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment