BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

WAVUVI WA DAR ES SALAAM KUANZA KUPATA NEEMA KUTOKA KWA RAIS MAGUFULI, SHEREHE ZA UHURU MIAKA 54 ZAWAPIGA TAFU YA NGUVU.

Askari wa JWTZ katika Chuo cha Mafunzo ya Huduma Pangawe wakifanya usafi eneo linalozunguka hospitali ya mkoa wa Morogoro.Picha na Juma Mtanda

Dar Es Salaam. Rais John Magufuli jana aliwaongoza Watanzania kufanya usafi na kuwataka kujenga utamaduni wa kudumisha utamaduni huo mara kwa mara.

Kufanyika kwa usafi kumetokana na hatua ya Rais Magufuli ya kufuta Maadhimisho ya Sherehe za miaka 54 ya Uhuru wa Tanganyika na badala yake, siku hiyo itumike kufanya usafi kwa lengo la kupiga vita ugonjwa wa kipindupindu ulioikumba baadhi ya mikoa nchini.

Pia, aliagiza Sh4 bilioni zilizokuwa zigharamie maadhimisho hayo, zitumike kwenye upanuzi wa barabara ya Morroco – Mwenge iliyopo Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Katika kusisitiza agizo lake ambalo lilipata mwitikio mkubwa katika maeneo mengi nchini, Magufuli alifanya usafi kwa muda wa dakika 50 katika eneo la Feri lililopo ufukwe wa Bahari ya Hindi jirani na Ikulu kwa kushirikiana na mkewe, Janet, wafanyakazi wa Ikulu na wavuvi.

Wavuvi hao takribani 100 ambao waliwapa wakati mgumu walinzi kutokana kutaka kumshika mkono Rais na kuimba nyimbo mbalimbali za kumsifu, kama ‘tingatinga limeingia’, ‘Hapa Kazi Tu’, ‘mafisadi wamekwisha’, ‘Rais wa wanyonge kaingia’, walilieleza gazeti hili kwamba waliona ajabu Rais kushiriki kufanya usafi na wananchi.

Ilivyokuwa
Huku akiwa amevaa suruali aina ya kadeti, shati la mauamaua, kofia na glovu mkononi, Dk Magufuli alianza kufanya usafi saa 1.30 asubuhi hadi saa 2.20 asubuhi akitumia chepeo na mikono kuzoa uchafu na kuutupia katika ndoo ya taka kisha kupakiwa katika gari la taka lililokuwa eneo hilo.

Baada ya nusu saa, alitembea taratibu kuelekea katika ufukwe wa Bahari ya Hindi, eneo ambalo kulikuwa na wavuvi waliokuwa wakishuhudia wakati akizoa uchafu na kuzungumza nao kwa dakika 10.

Dk Magufuli: Hamjambo?

Wavuvi: Hatujambo
Dk Magufuli: Nani kiongozi wenu?

Wavuvi: Bado hajafika
Dk Magufuli: Nani msaidizi wake|?

Wavuvi: Ali Yusuf
Dk Magufuli: (Huku akikaa juu ya mtumbwi), Yusuf hebu nieleze mna matatizo gani hapa.

Akieleza matatizo yao, Yusuf alisema wanalipa kodi zisizo na kichwa wala miguu, wananyimwa vibali vya uvuvi na Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) kutokana na kukosa zana za uvuvi kwa sababu zinauzwa gharama kubwa.

“Sisi ni wavuvi wadogowadogo, lakini tunatakiwa kuwa na vifaa vya kuzima moto na kisanduku cha dawa, sasa tunapata wapi vitu hivi. Hatupati mikopo ila kwa kuwa ulisema elimu ni bure, walau watoto wetu watasoma hatutalipa ada,” alisema Yusuf.

Baada ya maelezo hayo, Rais Magufuli alinyanyuka na kuwaita wasaidizi wake na kuwataka wachukue namba za simu za wavuvi wawili walioteuliwa na wenzao kuwawakilisha katika mchakato wa kusaidiwa atakaousimamia mwenyewe.

“Nawaomba wavuvi muwe na ushirikiano, naahidi kero zinazowakabili nitaziondoa. Kuweni waaminifu na msivue samaki kwa kutumia sumu, mabomu wala nyavu zilizopigwa marufuku.

“Haya masuala ya kodi, leseni na vifaa mnavyopaswa kuwa navyo wakati mnavua nitazungumza na Sumatra. Nyinyi ni jirani zangu lazima nidumishe ujirani mwema, maana hata nikianguka nyinyi ndiyo mtanibeba. Shida zenu nitazibeba,” alisema Dk Magufuli.

Alipomaliza kuzungumza na wavuvi hao aliondoka huku nao wakimfuata nyuma wakiimba nyimbo za kumsifu Rais na kujumuika naye kumalizia kuzoa lundo la uchafu lililokuwa limebaki.

Kufumba na kufumbua ndani ya dakika 10 uchafu wote ulikuwa umezolewa na kupakiwa kwenye gari la taka.

Akizungumza na waandishi wa habari, Rais Magufuli alisema: “Nawapongeza Watanzania kujitolea kufanya usafi, nina imani wataelewa umuhimu wa kufanya usafi katika maeneo yao kwa sababu ni aibu nchi yetu kuendelea kuwa na kipindupindu.”

Kauli za wavuvi
“Tangu niwe na akili timamu sijawahi kuona Rais akishirikiana na wananchi kufanya usafi wa mazingira. Ni kama siamini ninachokiona kwa kweli ametutia moyo sana,” alisema Moziga Abdallah.
Mwananchi
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: