Maalim Seif alitoa kauli hiyo baada ya kuulizwa ni nini hatma ya Zanzibar baada ya uchaguzi wa marudio uliofanyika jana.
“Mimi sijui, waulizeni CCM wao ndiyo wametengeneza hali hii, wao
ndiyo wamekusudia na wanajua wanaipeleka wapi nchi hii, watasema wao,”
alisisitiza Maalim Seif.
Aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari baada
ya kutembelewa na Vijana wa Baraza la Chama cha Demokrasia na Maendeleo
Chadema-Bavicha jijini Dar es Salaam jana kumjulia hali.
Baada ya kufutwa kwa uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka jana, hali ya
kisiasa ya Zanzibar imedaiwa kuwa tete haswa kutokana na CUF kudai
hawatambui kufutwa kwa uchaguzi huo msimamo wao wakitaka mshindi
atangazwe.
Maalim Seif alisema CCM wanafahamu wazi kwamba mshindi aliyeshinda
katika uchaguzi wa wa Okotoba 25, ni nani, lakini wameamua kufanya hivyo
na kuifikisha Zanzibar hapo ilipo sasa.
Alisema miaka mitano iliyopita kulikuwa kumepatikana maridhiano
Zanzibar na walikuwa wameanza kwenda vizuri, lakini kinachoonekana hivi
sasa wameanza kuwarudisha nyuma kwa kuvuruga tena maridhiano hayo na
kuanza kuleta uhasama.
“Hapo nyuma kulikuwa na uhasama wa kisiasa Zanzibar halafu ukaisha,
lakini hivi sasa wanaurudisha, CCM ndiyo wameamua iwe hivyo,” alisema
Maalim Seif.
Kadhalika, Maalim Seif alisema anaamini Mwenyekiti wa Tume ya
Uchaguzi ya Zanzibar (Zec), Jecha Salim Jecha, ametumwa kuitafutia kura
CCM.
“Jecha ametumwa kuitafutia kura CCM, lakini ijulikane kwamba hata
wafanye vyovyote watakavyofanya, Wanzanzibari ndani ya mioyo yao,
wanafahamu Rais wao ni mimi,” alisema Maalim Seif na kuongeza:
“Kinachotokea Zanzibar ni mipango iliyopangwa na CCM ambao pamoja
na kwamba wanamfahamu mshindi ni nani katika uchaguzi wa mwaka jana,
lakini wameamua kufanya hicho wanachofanya hivi sasa.”
Aidha, alisema kwa sasa hataki kusema chochote, isipokuwa anasubiri Rais atangazwe.
Maalim Seif yuko jijini Dar es Saalam kwa mapumziko mafupi baada ya
kuugua na kuruhusiwa kutoka hospitali zaidi ya wiki moja iliyopita. SOURCE:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment