BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA LATIKISIKA BAADA YA WABUNGE WATATU WA CCM KULITIKISA
Dar es Salaam. Hakuna shaka kuwa Bunge la Jamhuri ya Muungano linapitia kwenye kipindi kigumu baada ya wabunge watatu kupandishwa kizimbani jana, ikiwa ni ndani ya wiki mbili tangu kuibuke tuhuma za rushwa, mabadiliko yaliyoondoa wenyeviti watano.
Katika kipindi hicho, wabunge ambao wako jijini Dar es Salaam kuendelea na shughuli za Bunge wamediriki hata kukataa chai wanazoandaliwa kwenye mashirika na taasisi wanazoongoza, kwa hofu kuwa ukarimu huo unaweza kugeuzwa kuwa tuhuma za rushwa.
Pia, Spika Job Ndugai alifanya mabadiliko wa wajumbe 27 wa kamati za Bunge, akiwahamisha wenyeviti watatu na makamu wawili, uhamisho uliomaanisha wamepoteza nafasi zao, mmoja akipoteza nafasi ya Mwenyekiti wa Bunge, ambayo hushikiliwa na wabunge watatu ambao ni lazima wawe viongozi wa kamati.
Hata hivyo, Ndugai alisema mabadiliko yake ni ya kawaida na hayahusiani na tuhuma za rushwa zilizoandikwa na baadhi ya vyombo vya habari.
Wakati Ndugai akikana kuhusisha mabadiliko yake na tuhuma za rushwa, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Valentino Mlowola alisema taasisi yake imepokea tuhuma hizo na imeshaanza kuzifanyia kazi.
Pia, wabunge wawili, Zitto Kabwe (Kigoma Mjini, ACT Wazalendo) na Hussein Bashe (Nzega, CCM) walimuandikia barua Spika wakieleza uamuzi wao wa kujivua ujumbe kwenye kamati zao, kushinikiza kufanyika kwa uchunguzi ili watuhumiwa wachukuliwe hatua.
Jana, waliofikishwa mahakamani kwa tuhuma za kuomba rushwa ni Mbunge Mvomero (CCM), Suleiman Saddiq, Kangi Lugola (Mwibara,CCM) na Victor Mwambalaswa (Lupa, CCM), ambao walikuwa wajumbe wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC).
Takukuru iliwafikisha wabunge hao Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa shtaka hilo na wakili wa taasisi hiyo ya kuzuia na kupambana na rushwa, Maghela Ndimbo ikiwa ni mara ya pili kwa wajumbe wa LAAC kushtakiwa kwa tuhuma za rushwa.
Hata hivyo, washtakiwa hao wote walikana shtaka hilo na Lugola alisema baada ya kesi kuahirishwa kuwa hiyo “ni vita ya kisiasa” ambayo haitawazuia kuendelea kutumbua majipu.
CCM yatoa tamko
Saa chache baada ya tukio hilo, CCM ilitoa taarifa kuhusu kitendo hicho ikieleza kusikitishwa na tuhuma dhidi ya wabunge na kutaka uchunguzi ufanyike ili watakaobainika wachukuliwe hatua.
“Chama cha Mapinduzi kinasikitishwa sana na tuhuma hizo hasa pale zinapowahusu wabunge ambao ni wawakilishi wa wananchi na kinaunga mkono jitihada za vyombo vya dola katika kutafuta ukweli wa tuhuma hizo,” inasema taarifa ya CCM iliyosainiwa na msemaji wake, Christopher Ole Sendeka.
“Lazima ifahamike kuwa vitendo vya rushwa havina itikadi, dini wala ukabila na kwamba havikubaliki kwa namna yoyote kwa kuwa vina madhara makubwa kwa Taifa.”
CCM imesema haitasita kuwachukulia hatua za kinidhamu wabunge wake wote watakaobainika kuhusika kwenye vitendo hivyo.
Mahakamani
Jana, Wakili Ndimbo alisema washtakiwa hao walitenda kosa hilo Machi 15, kinyume cha kifungu cha 15 (2) cha Sheria ya Takukuru.
Wakili Ndimbo alisema siku ya tukio washtakiwa hao kwa nafasi zao za ujumbe wa Kamati ya Bunge ya LAAC, waliomba rushwa ya Sh30 milioni kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Gairo mkoani Morogoro, Mbwana Magote.
Wakili Ndimbo alibainisha kuwa washtakiwa hao walitenda kosa hilo wakiwa Hoteli ya Golden Tulip, iliyoko Masaki wilayani Kinondoni, Dar es Salaam na kwamba waliomba rushwa hiyo ili waweze kutoa mapendekezo mazuri ya taarifa ya hesabu za halmashauri hiyo za mwaka 2015/2016.
Hata hivyo, Wakili Ndimbo aliieleza Mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika hivyo akaiomba ipange tarehe nyingine ya kuitaja.
Pia, Wakili Ndimbo alisema upande wa mashtaka hauna pingamizi dhidi ya dhamana ya washtakiwa hao iwapo watakamilisha masharti.
Hakimu anayesikiliza kesi hiyo, Thomas Simba aliwataka kutekeleza masharti ya dhamana ambayo ni kuwa na mdhamini mmoja ambaye atasaini dhamana ya Sh5 milioni na ambaye atawajibika kuwafikisha mahakamani hapo kwa tarehe na saa itakayopangwa.
Washtakiwa wote walikuwa na wadhamini na Mahakama iliridhishwa na hati za utambulisho wa wadhamini hao na kuwaachia.
Hakimu Simba aliahirisha kesi hiyo hadi Aprili 14 itakapotajwa tena mahakamani hapo huku akiutaka upande wa mashtaka kukamilisha mapema upelelezi ili kesi hiyo ianze kusikilizwa mapema. Baada ya hakimu kutoka nje ya Mahakama, washtakiwa hao wakiwa kizimbani, walifurahia huku Saddiq na Lugola wakishangilia kwa kunyanyua juu mikono yote miwili wakionyesha ishara ya ushindi.
Sambamba na kushangilia huko, Lugola pia aliwashukuru waandishi wa habari, lakini akadai kuwa kesi hiyo ni vita ya kisiasa tu ambayo haitawakatisha tamaa wale walio tayari kutumbua majipu kuendelea kufanya hivyo.
“Nawashukru sana waandishi wa habari kwa ‘coverage’ yenu. Licha ya vita hii ya kisiasa, wale tulio tayari kutumbua majipu tutaendelea kutumbua majipu,” alisema Lugola ambaye amekuwa akijinasibu kupambana na ufisadi.
Lugola, mmoja wa wazungumzaji wakubwa kwenye Bunge la Kumi aliwahi kutinga bungeni na bango lililoandikwa “Maadui wakubwa wa bajeti ni bajeti mchepuko, rushwa, matumizi makubwa, misamaha ya kodi, deni la taifa, ufisadi na bajeti tegemezi” wakati akichagia hotuba ya bajeti.
Wabunge hao watatu waliingia mahakamani saa 5.28 asubuhi na kuketi kwenye mabenchi wakisubiri kupandishwa kizimbani kusomewa shtaka linalowakabili.
Saddiq alivalia shati lenye rangi nyeupe likiwa na michirizi ya rangi nyekundu na nyeusi, suruali nyeusi na viatu vyeusi.
Lugola alivalia shati la kitenge lenye rangi nyeusi na mabaka yenye rangi mchanganyiko wa nyekundu, nyeusi na nyeupe, suruali ya rangi ya kijani mpauko na viatu vyeusi, wakati Mwambalaswa alivalia shati jeusi lenye madoa meupe, suruali ya kijivu na makobazi.
Muda wote kabla ya kupandishwa kizimbani, washtakiwa hao walikuwa wakipekuapekua simu zao hadi hakimu alipoingia mahakamani.
Hakimu Simba aliingia mahakamani saa 5.52 asubuhi na baada ya kukaa kwenye kiti chake, wakili Ndimbo aliwaelekeza washtakiwa hao wapande kizimbani na kuwasomea mashtaka na washtakiwa wote walikana kutenda makosa hayo.
Mwaka 2012, Takukuru ilimfikisha mahakamani hapo Mbunge wa Bahi (CCM), Omary Badwell ikimshtaki kwa tuhuma za kushawishi na kupokea rushwa ya Sh1 milioni kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Mkuranga. Mbunge huyo alishinda kesi hiyo.MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment