BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

WAFANYABIASHARA WALIOKUBUHU KUUZA MADAWA YA KULEVYA HULISHANA YAMINI ILI ASIWEPO WA KUTOA SIRI ENDAPO MMOJA WAO KUKAMATWA NA POLISI TZ.


Dar es Salaam. Mapambano dhidi ya wafanyabiashara wa dawa za kulevya nchini yanahitaji mbinu na mikakati madhubuti kutokana na watuhumiwa kulishana yamini ili asiwepo yeyote wa kutoa siri wala kuwataja wengine endapo mmoja wao atakamatwa na polisi.

Baadhi ya wafanyabiashara hao huenda mbali zaidi hadi kuchanjiana damu kama ishara ya kula kiapo cha hali ya juu ili kutunza siri hiyo ambayo bosi mkubwa haruhusiwi kutajwa hata ikibidi mtuhumiwa afe.

Siri inayotunzwa ni ya magenge ya watu wanaozalisha, mahali inapozalishwa, usafirishaji na mmiliki wa dawa hizo ambazo zinapigwa vita duniani kote. Usiri huo mkubwa ndiyo sababu ya ugumu wa mapambano dhidi ya biashara hiyo haramu.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili, Kamishna mstaafu wa Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya, George Timbuka alisema hali bado inatisha katika biashara hiyo na inasababisha mamlaka za usalama kuumiza vichwa ili kutafuta mbinu za kung’amua, kukamata na kudhibiti usafirishaji wa dawa hizo ambao huwanufaisha wafanyabiashara wachache huku kundi kubwa hasa la vijana likiteketea.

“Siri ni kubwa sana. Hawa watu wanaapizana mpaka kufikia hatua ya kuchanjia damu ili kutunza siri; ukiwakamata wanaweza kutaja mpaka kiwango fulani lakini wale wamiliki wa mtando huo hawatajwi,” alisema Timbuka ambaye ni kamishna mwanzilishi wa tume hiyo.

Kamishna huyo aliyewahi kushika nafasi mbalimbali katika Jeshi la Polisi ikiwamo ya kuwa Kamanda wa Polisi katika mikoa ya Shinyanga, Mkoa wa Kipolisi wa Tazara na Lindi, anasema hali hiyo ya usiri mkubwa ndiyo inayochangia vita dhidi ya dawa za kulevya kuyumba.

“Hali hii inanikera sana. Hata mimi sijui tufanyeje, lakini inaniudhi sana. Hawa watu ni hatari kuliko hata majambazi; mtandao wao ni hatari na una siri kubwa,” alisisitiza.

Alisema vita dhidi ya dawa za kulevya haifanikiwi kwa kuwa watu wengi ni wabinafsi, si wa kweli huku wengi wa waliopewa majukumu wanaogopa kutimiza majukumu yao.

“Rushwa ipo lakini kama unafanya kazi yako vizuri huwezi kuogopa, lazima ujiamini hawawezi watu kukuletea rushwa kabla ya kukuchunguza wewe ni mtu wa namna gani, wakiona ni legelege na mwenye tamaa utaletewa ... Enzi zangu walikuwa wanajua hawawezi kuniletea rushwa, walikuwa wananiogopa,” anasema Timbuka ambaye alistaafu mwaka 2004.

“Nilikuwa nafanya kazi kwa masilahi ya nchi yangu ndiyo maana mpaka leo mmeweza kuja kwangu na kuona ninavyoishi. Nina amani, nimeridhika na maisha niliyo nayo, sikuona sababu ya kuchukua rushwa na kujilimbikizia mali... Leo hii ningekuwa mgeni wa nani. Je, wanangu ningewapeleka wapi endapo ningetiwa hatiani?”

Kuhusu vitisho na mitego kutoka kwa wafanyabiashara hao, alisema vipo lakini lazima mtu ajitambue anafanya kazi kwa ajili ya masilahi ya nani na kwamba endapo atakuwa na msimamo hawezi kurubuniwa kirahisi.

“Kuna kipindi nilikuwa napata simu za taarifa kuwa kuna dawa za kulevya sehemu wakitaka nifuatilie, lakini nilikuwa natuma vijana wangu, cha ajabu wakienda muda mfupi tu napigiwa tena simu ‘kwa nini hujaja mwenyewe?’ Hali hii ilinitisha sana.


Lakini pia siku moja nikiwa nimeingia baa moja maarufu, alikuja kijana mmoja na kuniambia ‘wewe mzee Timbuka kwa nini unatuzibia tusiwe matajiri?’ Ilibidi niondoke muda uleule, niliona hali sasa ni mbaya,” alieleza.

Alipoulizwa nini kifanyike ili kushinda vita hiyo, Timbuka alisisitiza kwamba watu waache ubinafsi, wawe wa kweli na waliopewa majukumu watimize bila kuogopa na wawe na hofu ya Mungu.

Pia, alisema ili kupambana na dawa hizo, Serikali haina budi kutilia mkazo utoaji elimu kwa kushirikisha viongozi wa dini zote, lakini pia kila Mtanzania kwa nafasi yake atimize wajibu wake.

Alisema licha ya wakati wao kufanya kwa kiwango chao, hadi sasa tatizo bado ni kubwa na tangu aondoke bado mianya ni ileile, hivyo juhudi zaidi zinahitajika katika kukabiliana nalo.

Utendaji kazi wa Tume

Kuhusu utendaji wa Tume, Timbuka aliyefanya kazi katika Serikali ya Awamu ya Tatu chini ya Rais Benjamin Mkapa, amependekeza iongezewe meno kama alivyopendekeza kabla hajastaafu.

“Ningependa kuona Tume ikifanya kazi ya kuchunguza, kukamata na kushtaki mahakamani wahalifu wote wa dawa za kulevya tofauti na sasa inavyotoa taarifa tu,” alisema.

Hata hivyo, alisema marekebisho yaliyofanywa mwaka juzi ya Sheria ya Kuzuia Biashara Haramu ya Dawa za Kulevya ya mwaka 1995 kutokana na upungufu, imesaidia kidogo ingawa jitihada zaidi zinahitajika.

Kwa sasa, Tume inafanya kazi kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani; Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto; Wizara ya Mambo ya nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa na Wizara ya Fedha.

Vigogo wa dawa ni nani?

Alipoulizwa kuhusu vigogo wa biashara hiyo yaani viongozi serikalini au wafanyabiashara wakubwa, Timbuka aliwataka Watanzania kutoichukulia dhana ya ‘kigogo’ kuwa ni viongozi serikalini tu, bali pia watambue kuwa ni wale wenye mitaji mikubwa na wanaosambaza dawa hizo kwa wingi katika nchi mbalimbali huku wakiwa na wafuasi wengi wanaowasaidia kufanya kazi hiyo.

“Hiyo dhana ni potofu, ukichunguza biashara hii inamilikiwa hata na vijana wadogo wenye umri hata wa miaka 20 na nyuma yake akawa na wafuasi wengi wanaomuabudu kama mungu wao,” alifafanua.

Kesi mahakamani

Akifafanua kipengele cha utaifishaji vielelezo vya kesi za dawa za kulevya pindi zifikishwapo mahakamani, alisema hilo bado ni tatizo linalohitaji kutafutiwa njia mbadala ya kulitatua.

Akitolea mfano wa nyumba moja iliyoko eneo la Mbezi Beach jijini Dar es Salaam ambayo ilikutwa na mtambo wa kutengeneza dawa hizo, alisema haikutolewa mahakamani kama kielelezo.

“Licha ya wahusika kuhukumiwa kifungo jela, ilitakiwa hata ile nyumba itaifishwe, lakini ilishindikana kwa kuwa haikutolewa mahakamani kama kielelezo,” alisema Timbuka na akatoa wito kwa wapelelezi wa kesi za dawa za kulevya kuendelea kuisoma vyema sheria, ili wasitoe mwanya kwa wahalifu hao kubakia na mali zinazotokana na uhalifu wao. 


“Mtu akikamatwa na dawa za kulevya hata kama ni kwenye gari, nyumbani hivyo vyote ni vielelezo vinatakiwa vifikishwe mahakamani na Mahakama ndiyo itatoa uamuzi wa kutaifisha ama la kulingana na utetezi utakaotolewa,” alifafanua.MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: