BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

WAZIRI WA NISHATI NA MADINI AELEKEZA BAJETI YOTE YA MWAKA WA FEDHA 2016/2017 KATIKA MIRADI YA UMEME

 
Dodoma. Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo jana aliwasilisha bajeti ya wizara yake akitenga Sh1 trilioni (sawa na asilimia 94 ya bajeti ya wizara yake) kwa ajili ya miradi ya maendeleo, mingi ikiwa ya umeme.

Katika bajeti hiyo ya mwaka wa fedha 2016/17, Profesa Muhongo aliomba kuidhinishiwa Sh1.1 trilioni ambako Sh66.2 bilioni ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida ambayo ni sawa na asilimia sita ya bajeti yote.

“Katika fedha hizo asilimia 98 ya bajeti ya maendeleo imetengwa kwa ajili ya sekta ya nishati,” alisema Profesa Muhongo.

Alisema katika fedha hizo za matumizi ya kawaida, Sh38.8 bilioni ni kwa ajili ya matumizi mengineyo sawa na asilimia 59 na Sh27.3 bilioni sawa na asilimia 41 ni kwa ajili ya mishahara ya watumishi wa wizara na taasisi zake.

Ingawa bajeti za wizara zinaendelea kuwasilishwa, wizara hiyo hadi sasa inaweza kuwa ya pili baada ya ile ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ambayo iliomba Sh4.8 trilioni, kati ya hizo Sh2.2 trilioni kwa ajili ya sekta ya ujenzi, Sh2.5 trilioni kwa ajili ya sekta ya uchukuzi na Sh95.8 bilioni kwa ajili ya sekta ya mawasiliano huku mgawo wa maendeleo ukiwa wa kiwango cha juu. 


Katika sekta ya ujenzi, Sh35.9 bilioni ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida huku Sh2.1 trilioni (asilimia 95.5) zikiwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Kwa upande wa uchukuzi, kati ya Sh2.5 trilioni zilizoombwa, Sh91.5 bilioni ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh2.4 trilioni (asilimia 96) ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Katika sekta ya mawasiliano ambako Sh95.8 bilioni zimeombwa, Sh3 bilioni ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh92.7 bilioni (asilimia 96.8) ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Miradi ya umeme
Alisema baada ya kukamilika kwa mradi wa Kinyerezi I wa megawati 150, Serikali imepanga kuongeza mitambo mingine ya kuzalisha umeme wa Kinyerezi I Extention utakaotoa megawati 185.

“Fedha zilizotengwa kwa ajili ya mradi huu ni Sh119 bilioni na umepangwa kukamilika mwishoni mwa mwaka 2019,” alisema. Profesa Muhongo alisema mradi wa Kinyerezi II wa megawati 240 umeanza na utagharimu Sh564 bilioni.

Akizungumzia Wakala wa Nishati Vijijini (Rea), Profesa Muhongo alisema bajeti yake imeongezwa kutoka Sh357 bilioni mwaka 2015/16 hadi Sh534 bilioni kwa mwaka 2016/17.

“Rea ipo katika utaratibu za ununuzi wa kumpata mkandarasi atakayetekeleza mradi wa kusambaza umeme kwenye vijiji 121 inakopita njia kuu ya umeme ya Iringa hadi Shinyanga,” alisema.

Wizara nyingine

Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji iliomba Sh81.8 bilioni ili kutekeleza majukumu yake, kati ya fedha hizo, Sh41.8 bilioni sawa na asilimia 51 ya bajeti ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh40 bilioni sawa na asilimia 49 ni kwa ajili ya maendeleo.

Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka 2016/17 iliomba Sh275 bilioni kati ya fedha hizo, Sh153.6 bilioni (asilimia 55.9) ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh115.5 bilioni ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo (asilimia 44.1).

Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Mamlaka za Serikali za Mitaa iliomba Sh6 trilioni kati ya fedha hizo Sh3.7 trilioni ni za mishahara, Sh646 bilioni ni matumizi mengineyo na Sh1.6 trilioni ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo.CHANZO:MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: