KUFUNGA kwa kuacha kula na kunywa kwa saa au siku kadhaa ni jambo kongwe na linafanywa na waumini wa dini mbalimbali na hata makundi mengine ya watu kwa sababu tofauti.
Waumini wa dini ya Kikristo huwa wanafunga kipindi cha Kwaresma au siku nyingine kulingana na imani yao.
Waislamu wanafunga Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kama lazima katika dini na siku nyingine za hiari (Sunna).
Watu wanaofunga kwa kuacha kula na kunywa, ratiba yao ya chakula inabadilika .Kwa upande wa Waislamu, hua miilo mikuu miwili, mlo wa futari na ule wa usiku wa manane (Daku).
Futari ni mlo ambao mfungaji anautumia ili kufungua kinywa mara tu jua linapozama, Kwa kuwa mtu amekaa muda mrefu bila kula chakula ni vema futari yake iwe mlo laini ambao ni rahisi kusagwa tumboni.
Pia,Vyakula hivyo viwe vitamu kutokana na sukari iliyomo katika vyakula vyenyewe, Ndizi zilizoiva na kupikwa,viazi vitamu, Maharage, Mihogo, Magimbi, Uji, Maziwa, juisi ya asili na vingine mithili ya hivyo ni mfano wa vyakula laini.
Zaidi ya hayo, mlo wa futari lazima uwe mlo kamili, wenye mafungu yote ya vyakula kama vile wanga, mafuta, protini, madinivitamini, maji ya kunywa na nyuzi lishe (Dietary fibre).
Kwa hiyo, futari ya mihogo, tambi, magimbi na viazi lazima iwe na maharage ,nyama, samaki au dagaa,Vile vile, lazima futari hiyo iwe na matunda na mboga za majani za kutosha.
Kwa mujibu wa kanuni za ulaji bora, mtu mmoja anatakiwa ale matunda vikombe vidogo vitatu na mboga za majani vikombe viwili mpaka vitatu kwa siku.Kwa watu wanaofunga wanatakiwa wapange ratiba zao ili kutimiza hesabu hiyo usiku wa mfungo.
Vilevile,vyakula vya futari visiwekwe sukari,chumvi wala mafuta mengi.Watu watumie mafuta yanayotokana na mimea na kwa kiasi kidogo.
Mafuta ya Mizaituni, Alizeti, Ufuta na kiini cha Mahindi ni miongoni mwa mafuta bora kabisa kwa afya ya mlaji yanayopatikana hapa Tanzania.
Vinywaji aina ya Koka,Chai na Kahawa viepukwe au vitumiwe kwa kiasi kidogo usiku wa mfungo.Hii ni kwa sababu vyakula na vimywaji hivyo vikiliwa karibu na Alfajiri humfanya mfumgaji kupoteza maji mengi panapokucha kwa njia ya mkojo.Hali hiyo ni hatari kwa afya.
Dini ya Kiislamu inawahimiza wafungaji kutumia Tende,maji au maziwa kama kifungua kinywa wanapoanza kufuturu .Tende ina asilimia 60 mpaka 70 ya sukari ya asili aina ya glucose na fructose.
Mtu akila Tende aina hii ya Sukari inanyonywa na utumbo na kuunguzwa na seli na hatimaye inatoa nguvu kwa haraka inayompa mfungaji furaha na kutuliza akili yake kwa haraka.
Tende pia ina vitamin za aina mbalimbali,protini asilimia 2.5 na madini asilimia 2.1.Pia Tende ina mafuta kidogo kiasi cha asilimia 0.4 ili kukidhi haja ya mwili na haina aina mbaya ya mafuta.
Zaidi ya hayo,Tende ina nyuzi lishe asilimia 3.9 ambazo zinasaidia kunyonya sumu tumboni na kumwezesha mlaji kupata haja kubwa mara kwa mara.Wali,Ndizi au ugali ni vyakula vizuri kwa daku.MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment