BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

UKATILI: WATU WANANE WAKUSANYWA KWA MWENYEKITI WA KITONGOJI NA KUCHINJWA KWA MAPANGA


Tanga. Watu wanane wameuawa na watu wasiojulikana baada ya kuwakusanya sehemu moja nje ya nyumba ya mwenyekiti wa kitongoji na kuwachinja kwa mapanga.

Mauaji hayo yalitokea katika Kitongoji cha Mabatini, Kata ya Mzizima, Wilaya ya Tanga, tukio ambalo limeelezwa na wakazi wa eneo hilo kuwa la kutisha ambalo haliwezi kusahaulika.

Mauaji hayo yamefanyika wakati watu takriban 10 wameripotiwa kuuawa kwa kuchinjwa ndani ya siku 15 katika maeneo mbalimbali, wakiwamo watatu waliochinjwa msikitini jijini Mwanza.

Tukio jingine la mauaji lilitokea Mei 10, saa 7 usiku wakati watu saba wa familia moja walipochinjwa kwa mapanga katika kijiji cha Sima wilayani Sengerema.

Mei 25, mtumishi wa Wizara ya Fedha, Aneth Msuya alichinjwa nyumbani kwake maeneo ya Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Leonard Paulo alisema mauaji hayo yalifanyika saa saba usiku wa kuamkia jana na kundi la watu alilosema wanahofiwa kuwa majambazi lililowateka wakazi hao majumbani mwao na kuwakusanya pamoja kisha kutekeleza unyama huo.

Paulo aliwataja waliochinjwa katika tukio hilo kuwa ni Issa Hussein (50) ambaye ni mjumbe wa Kitongoji cha Kibatini, Mkola Hussein (40), Hamis Issa (20), Mikidadi Hussein (70) na Issa Ramadhani (25).

Wengine ni Mahamoud anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka kati ya 35 na 40 na wengine wawili, Kadiri na Salum ambao walitajwa kwa jina mojamoja.

Mauaji hayo yalifanyika katika eneo lililo jirani na mapango ya Amboni ambako Februari 15 mwaka jana yalitokea mapigano yaliyohusishwa na matukio ya kigaidi, ambayo hata hivyo, Serikali imeendelea kusisitiza kuwa ya ujambazi.

Katika matukio hayo ya mwaka jana, askari mmoja alikufa kwa kupigwa risasi huku wengine wakijeruhiwa na aliyekuwa Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Polisi, Paulo Chagonja aliwaeleza waandishi wa habari kwamba katika operesheni waliwaua tumbili na kukuta vitu kadhaa ikiwamo pikipiki mbovu.

Simulizi ya mauaji
Akisimulia mauaji hayo, mke wa marehemu Mkola, Asha Said ambaye ameachiwa watoto sita, alisema akiwa amelala na mumewe walisikia mlango ukigongwa na walipouliza ni nani anagonga, wakajibiwa kuwa ni askari.

“Mume wangu alipowafungulia alitoka na panga, wakamwambia unatoka na panga wakati sisi tuna bunduki? Kisha wakauliza, ‘watoto wetu mliowapigia simu polisi wawachukue, wako wapi’” alisema Asha.

Alisema watu hao walimtaka mumewe awapeleke kwa Issa ambaye ni kaka yake na mwenyekiti wa kitongoji. Pia, walianza kumpiga na kumkanyaga tumboni kabla ya kwenda kwa Hussein.

“Lililotokea haliwezi kusahaulika maishani mwangu kwani sijawahi kuona watu wakifanyiwa unyama wa aina ile... Nilikuwa nachungulia jinsi walivyokuwa wakimtesa na alipowafikisha nyumbani kwa Hussein wakamtoa nje kwa nguvu, naye wakaanza kumpiga kikatili,” alisema Asha.

Shuhuda mwingine ambaye ni mzee katika kitongoji hicho, Kea Leonard (67) alisema akiwa nyumbani kwake alisikia kelele ndipo akatoka nje na kusimama kwenye kona ya nyumba, akaona kundi la watu wakiwa wamevaa nguo nyeusi wakijifunika vitambaa vyeusi.

Alisema alisikia wakihoji wako wapi watoto waliokamatwa na wanakijiji hao na kuwaripoti polisi kuhusu kuonekana kwao kijijini.

Shuhuda huyo alifafanua kwamba wiki moja iliyopita, muda wa usiku lilipita kundi la watoto wanaokadiriwa kuwa na miaka kati ya 12 hadi 16 kijijini hapo na baada ya kufika kwenye mto, walirejea hapo wakionekana kutojua njia.

Alisema wakazi wa kijiji hicho waliamua kuwazuia na kutoa taarifa kwa mwenyekiti wa kitongoji hicho, Issa Hussein ambaye baadaye alipiga simu polisi ambao walifika na kuwachukua vijana hao wanane na mmoja wao alitoroka.

“Tulipowahoji watoto hao, baadhi walisema wanatoka mjini Tanga na wengine kitongoji cha Amboni na kwamba walikuwa wakitaka kuvuka mto lakini walivyoona maji mengi wakashindwa,” alisema Mzee Kea.

Mkazi mwingine Khalid Issa ambaye ni mjomba wa Mkola alisema mauaji hayo yamesababisha waishi kwa hofu wakihofia kuwa siku zijazo itakuwa zamu ya wengine kijijini hapo.

“Tutaishije hapa tena? Kama wamewaua kinyama vijana ambao walikuwa tegemeo la ulinzi katika kitongoji chetu, kesho si watakuja kutumalizia tuliobaki?” alihoji Khalid.

Diwani wa Mzizima, Fredrick Chiluba alisema wananchi wa eneo hilo wanashindwa kujua nani atawalinda kutokana na tukio la kuchinjwa wenzao.

“Wananchi wapo katika hofu kubwa kwa sababu mwanzo walipovamiwa na ng’ombe, mbuzi na kuku kuchinjwa walihakikishiwa kwamba hayatajirudia tena, sasa leo wamechinjwa watu tena kwa idadi kubwa,” alisema.

Hata hivyo, Kamanda Paulo alisema kwa sasa vyombo vya ulinzi na usalama vinachunguza kubaini sababu za kujirudia matukio hayo.

Alisema katika tukio la jana, ambalo majambazi hao walitokomea kusikojulikana; walipora mchele, biskuti na sukari katika duka dogo la Mikidadi ambaye pia alichinjwa.

“Siwezi kusema mengi, hili jambo ni zito na kubwa, hivyo subirini vyombo vya ulinzi na usalama vifanye kazi zake, tutawaeleza baada ya kuchunguza na kujua,” alisema.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigela alifika eneo la tukio na kusihi wanakijiji kuwa na subira kwa sababu Serikali ina mkono mrefu na kwamba itahakikisha walioshiriki wanakamatwa.

“Huu ni unyama mkubwa, hatuwezi kuuvumilia, Serikali ina mkono mrefu tutahakikisha kila aliyehusika anakamatwa,” alisema Shigela.

Tukio hilo ni mfululizo wa mauaji ya kinyama, ujambazi na uporaji wa kutumia silaha jijini Tanga, matukio ambayo yamezidisha hofu kwa wakazi.

Mwezi uliopita yalifanyika mauaji ya kinyama katika duka la Central Bakery jijini Tanga na watu wanne waliuawa kwa risasi huku majeruhi mmoja akifia Muhimbili, Dar es Salaam alikopelekwa kwa matibabu.

Tume ya haki za binadamu

Wakati hayo yakitokea, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imeitaka Serikali kupitia Jeshi la Polisi kuchukua hatua mahsusi kuhakikisha ulinzi wa wananchi dhidi ya mauaji na vitendo viovu vilivyoshika kasi.

Kauli ya tume hiyo inafuatia kukithiri kwa vitendo vya mauaji ya kutisha, yakiwamo yaliyotokea Mwanza, Mara, Pwani na Dar es Salaam ambayo kuwa ujumla yamegharimu maisha ya wananchi wengi, wakiwamo waliochinjwa.

Mwenyekiti wa Tume hiyo, Bhame Nyandunga alisema jukumu la kwanza la Serikali ni kuhakikisha usalama wa wananchi. Alitaka Polisi kuhakikisha watu wote waliohusika kutekeleza mauaji hayo wanakamatwa ili sheria ichukue mkondo wake. 


Katika tamko lake, mwenyekiti huyo alizishauri mamlaka za Serikali za mitaa katika ngazi zote ziwe na mipango madhubuti ya kuhakikisha ulinzi na usalama katika maeneo yao.CHANZO:MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: