BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

MBEGU MPYA YA MPUNGA KUONGEZA UZALISHAJI WA MAZAO MOROGORO



WAKULIMA wa zao la mpunga wilayani hapa wanatarajia kuongeza uzalishaji wa zao hilo baada ya kugundulika kwa mbegu mpya ya mpunga ya chotara inayoendelea kufanyiwa utafiti, kuanza kutoa majibu.


Mbegu hiyo iliyofanyiwa utafiti nchini Kenya na Taasisi ya Hybrids East Africa Limited (Heal), imeonyesha ikipandwa kwenye eneo la hekta moja, ina uwezo wa kuzalisha magunia kati ya 100 hadi 120.

Akizungumza katika siku ya maonesho ya kilimo na utoaji elimu kwa wakulima wa zao la mpunga, wilayani hapa, mkulima mtafiti wa majaribio ya mbegu hiyo,Veronica Urio, wameshaifanyia utafiti hapa nchini na kuweza kuzalisha magunia 100 kwa hekta moja.

Alisema utafiti huo umetoa majawabu katika Kijiji cha Mngeta, wilayani Kilombero ambako mbegu hiyo ilifanyiwa majaribio kwa mara ya kwanza, kabla ya majaribio mengine kuendelea kufanyika katika Kijiji cha Dakawa, wilayani Mvomero.

Alisema kabla ya kuanza kutumia mbegu hiyo, alikuwa akitumia aina ya Saro ambayo kwa hekta moja wamekuwa wakivuna magunia ya mpunga kati ya 40 hadi 50 na kuwataka wakulima wenzake kubadilisha maisha kwa kuipokea mbegu hiyo.

“Mimi siwakatazi kutumia mbegu tulizozizoea, lakini hili ni shamba langu nimepanda hii mbegu mpya inayofanyiwa utafiti na shamba lingine nimepanda mbegu ya Saro, tuliozoea wenyewe mnajionea tofauti iliyopo, sasa nawaombeni tuchangamkie hii mbegu inatoa mavuno mengi ili tulime kilimo chenye tija,” alisema.

Ofisa Uhusiano wa Shirika la Kuhudumia Wakulima Afrika, inayofadhili mradi huo,Wandera Ojanji, alisema teknolojia hiyo ya mbegu ni ya kwanza kutolewa katika nchi za Afrika ikiwa na lengo la kuongeza uzalishaji wa mpunga.

Alisema mbegu hiyo inafanyiwa utafiti katika nchi za Tanzania na Kenya, inatarajiwa kuanza kuzalishwa baada taratibu za kufanyiwa uchunguzi kwa nchi hizo kukamilika mwakani na inaonyesha kuleta mapinduzi katika kilimo hicho.

“Tayari hapa nchini mbegu hii imeshapelekwa Wizara ya Kilimo, kwa ajili ya kufanyiwa utafiti wa kina baada kuona jinsi inavyoweza kuzalisha, hivyo tunategemea baada ya kuchunguzwa mwakani, itaanza kuzalishwa na kusambazwa kwa wakulima,” alisema. 


Mmoja wa wakulima wa mpunga katika skimu ya umwagiliaji wa Dakawa, Julius Nshalila, aliitaka serikali kuifanyia utafiti wa haraka mbegu hiyo kama inaleta tija ili ianze kusambazwa kwa wakulima wa mpunga katika Wilaya ya Mvomero waweze kujikwamua kimaisha kupitia kilimo hicho.NIPASHE
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: