Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan.
SIKU moja baada ya Ofisi ya Makamu wa Rais kutoa taarifa ya kukanusha taarifa iliyokuwa ikisambazwa kwenye mitandao ya kijamii juzi kuwa Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, ameomba kujiuzulu nafasi yake, vyombo vya usalama vimeanza uchunguzi wa kumpata mzushi wa taarifa hiyo ya uongo.
Habari za kuaminika kutoka ndani ya Jeshi la Polisi ziliiambia Nipashe jana kuwa kazi ya kumsaka mtu aliyeanzisha uzushi huo ilianza mara moja baada ya taarifa hizo kuanza kusambaa juzi.
Mtoa taarifa wetu hakuweza kueleza kwa kina hatua ambayo upelelezi huo umefikia kwa hofu ya kuharibu uchunguzi huo, hata hivyo.
Alieleza kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi ya aliyehusika kwa kuwa alitoa taarifa za kuupotosha umma kinyume cha sheria.
Awali Msemaji wa Jeshi la Polisi, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Advera Bulimba alimtaka mwandishi atafute taarifa hizo kwenye wizara husika kwanza, alipoulizwa na Nipashe kuhusu hatua zilizochukuliwa na Jeshi hilo kwa chanzo cha kusambaa kwa habari hizo za uzushi.
Alisema ni vyema mwandishi akapata taarifa ya hatua zilizochukuliwa kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais ndipo arudi kwa Jeshi la Polisi kuuliza.
“Kwa nini usiiulize Ofisi ya Makamu wa Rais wanachukua hatua gani kwanza," alisema Bulimba. "Waulize kwanza wao wanachukua hatua gani, ndipo uniuliuze na mimi.”
Alipoulizwa kama majibu ya ofisi ya Makamu wa Rais na majibu ya Jeshi la Polisi yana uwiano wa aina tofauti, alimtaka mwandishi aulize ndipo naye atoe taarifa.
Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu, aliiambia Nipashe kwa njia ya simu kuwa taarifa hizo hajazipata. Aliomba kutojibu swali hadi hapo atakapopata taarifa kamili.
“Hizo taarifa zijazipata, naomba unipe muda nizisome kwanza,” alisema Mangu.
Taarifa kwa umma iliyotolewa juzi na Ofisi ya Makamu wa Rais Dar es Salaam, ilisema taarifa zinazosambazwa zikisema makamu huyo wa Rais ameomba kujiuzulu nafasi yake ni uzushi na uongo.
Kwa mujibu wa taarifa zilizokuwa zikisambazwa kwenye mitandao ya kijamii, zilidai makamu huyo wa rais ameamua kujiuzulu.
Kufuatia habari hiyo kusambaa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii, taarifa hiyo ya Ofisi ya Makamu wa Rais ilisema
“taarifa hiyo ni ya uchochezi inayolenga kuliweka Taifa kwenye taharuki.
“Mhe. Makamu wa Rais yuko bega kwa bega na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kufanya kazi zao kwa mujibu wa Katiba ya nchi ili kuwaletea wananchi maendeleo.
“Ofisi ya Makamu wa Rais inawataka wananchi na Watanzania kwa ujumla kupuuza taarifa hiyo ambayo inalenga kupotosha umma kuhusu ushirikiano mzuri uliopo baina ya Viongozi wetu.
“Mwisho, Ofisi ya Makamu wa Rais inawasihi Watanzania kufanya kazi kwa bidii na wajiepushe na vitendo vinavyolenga kuvuruga amani na utulivu nchini,” ilisema taarifa hiyo.NIPASHE
0 comments:
Post a Comment