JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, limeeleza jinsi majambazi watatu kati ya 14 wanaotuhumiwa kumuua polisi katika eneo la Vikindu, Mkuranga mkoani Pwani, walivyouana wenyewe kwa wenyewe.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro, alisema sambamba na tukio hilo la majambazi hao kuuana Jumamosi iliyopita, pia walikamata bunduki 22 za aina mbalimbali na risasi 835, zilizokuwa zikitumiwa na wahalifu hao.
Akieleza jinsi tukio hilo lilivyotokea, alisema majambazi watatu waliouliwa na wenzao walikamatwa katika maeneo ya Mbagala, Keko na Kawe na walipowahoji walikiri kufanya matukio mbalimbali ya uhalifu kwa kutumia silaha na kutaja silaha walizonazo.
Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (ASP), Thomas Njiku (40), aliuawa kwa kupigwa risasi Agosti 26, mwaka huu kwenye eneo la Vikindu wakati akiongoza kikosi maalum cha kuwasaka watu waliosadikiwa kuwa ni majambazi.
Njiku ambaye alikuwa ndiye kiongozi wa msafara wa kikosi cha polisi, alifariki baada ya kupigwa risasi ambazo zilimpata kichwani na kusababisha kifo chake.
Alikuwa anaongoza operesheni ya kusaka wahalifu kufuatia mauaji ya polisi wanne, Koplo Yahya Malima, Konstebo Tito Mapunda, Konstebo Gaston Lupanga na Koplo Hatibu yaliyotokea eneo Mbande nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam wakati wakikabidhiana, Agosti 23, mwaka huu.
Sirro alisema baada ya mahojiano zaidi majambazi hao walitaja kwamba walikuwa wameficha silaha nyingine Vikindu na ndipo askari waliambatana nao hadi kwenye msitu huko walikozificha.
Alisema wakati majambazi hao wanawapeleka askari kuwaonyesha mahali walipoficha silaha hizo, majambazi walikuwa wameweka mtego ili kuwashambulia, lakini walilibaini hilo na hivyo wakawatanguliza.
Sirro alisema mbinu ya kuwatanguliza majambazi hao ndiyo iliwasaidia askari hao kwa sababu badala ya kuwashambulia askari walianza kushambuliana wenyewe kwa wenyewe.
“Baada ya kukamata majambazi hao na kuwahoji waliwapeleka kwenye nyumba moja ambayo wameikodi kwa ajili ya kufanyia ujambazi iliyopo eneo la Mbezi chini Kinondoni jijini Dar es Salaam, wakafanya msako na kupata silaha mbalimbali, na kukiri kwamba wana mtandao wao kutoka Kenya na nchi nyingine jirani,” alisema Sirro.
“Baada ya kuwahoji walikiri wao ni mtandao wa majambazi walioko Vikindu, na kwamba wana silaha nyingine walizoiba Kituo cha Polisi cha Stakishari na nyingine waliziagiza Afrika Kusini na walikuwa wamezificha katika msitu huo, polisi walikubali kwenda nao kufuata hizo silaha saa sita usiku, lakini kumbe walikuwa wametega mtego kuwashambulia askari, lakini bahati nzuri vijana wetu walikuwa wajanja wakawatanguliza kwa hiyo walivyorusha risasi ikawakuta majambazi, askari wetu wakakwepa mtego wao,” alisema.
Sirro alisema majambazi hao baada ya kupigwa risasi na wenzao, askari waliwachukua na kuwakimbiza katika hospitali ya Taifa Muhimbili lakini walipowafikisha waliambiwa kwamba walikuwa wamefariki.
“Askari wakiwa msituni ghafla walisikia milio ya risasi ikitokea mbele wakalala chini zikisikika sauti ‘mmetuua sisi’ baada ya risasi mfululizo kutulia askari walikuta majambazi hao wakiwa wamejeruhiwa sehemu mbalimbali za kifuani na tumboni huku wakivuja damu baada ya kuwabeba kuwapeleka hospitali wote walikuwa wamefariki,” alisema.
Pia Sirro alisema kati ya majambazi 14 waliohusika katika mauaji ya askari wake Thomas Njuki, huko Vikundu, kati ya hao saba wamekamatwa na wanaendelea kuhojiwa na jeshi hilo.
Alisema mafanikio ya kuwakamata majambazi hao limekuja baada ya jeshi hilo kufanya msako maalum uliofanywa na kikosi maalum cha kupambana na ujambazi wa kutumia silaha kufuatia tukio la wizi lililofanyika Sophia House jijini Dar es Salaam, Septemba 3, mwaka huu, ambapo ziliporwa Sh. milioni 35,000,000 na gari.
SILAHA
Sirro alitaja silaha zilizokamatwa kutoka kwa majambazi hao waliofariki kuwa ni silaha za kijeshi tatu, `magazine’ tupu nane na risasi 120, bunduki aina ya shot gun pumb action tatu na risasi 130, bastola 16, `magazine’ tupu moja na risasi 548, radio call 12, charger tatu za radio call, Bainqcula tatu, risasi baridi za kutishia 37, pingu za plastiki 45, bullet proof tatu na mkasi mmoja wa kukatia vyuma vigumu.
Vingine alivitaja kuwa ni mtalimbo wa mmoja wa kuvunjia milango, `tool box’ moja ya kusafirisha silaha, nyundo kubwa moja, pingu za chuma tatu, CCTV server moja, panga moja, gari mbili aina ya Toyota Noah pamoja na Toyota Alphad.
Sirro alisema majambazi hao walikiri kuhusika na wizi wa mamilioni ya fedha katika benki ya Habib African maeneo ya Kariakoo na Benki ya Stanbic mwaka 2014.
Alisema bado jeshi hilo linaendelea na uchunguzi na baada ya kukamilika watatoa taarifa zaidi.
Wakati huo huo, Sirro alisema Jeshi la Polisi limewakamata watuhumiwa sita wanaodaiwa kuhusika na vitendo vya uvunjaji nyumba usiku na kuiba.
Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Seleman Mohamed mkazi wa Magomeni, Twenye Abdalah (Magomeni Mwembe Chai), James Emmanuel (Magomeni Suma), Bimu Yahaya (Ubungo), Abdallah Mohamed (Mabibo Jitegemee) na Deogratius Oscar (Mabibo).
Pia alisema kuna watuhumiwa wengine wanne waliokamatwa katika tukio jingine la wizi wa magari nane ya jijini Dar es Salaam, ambayo yaliuzwa katika mikoa mbalimbali.
Mbali na matukio hayo, Sirro alisema jeshi hilo limekusanya milioni 920,970,000 ambazo ni tozo za makosa ya usalama barabarani kuanzia Agosti 25 hadi Septemba 4, mwaka huu.
Kuhusu magari yaliyokamatwa kutokana na makosa ya usalama barabarani, alisema yalikuwa 29,293, pikipiki 1406, daladala 8345, pamoja na magari mengine 20,948.NIPASHE
0 comments:
Post a Comment