MAMBO MATANO YA MATESO ANAYOKUMBANA NAYO MTOTO WA KIKE AKIZALIWA MKOA WA MARA TANZANIA
Picha ya maktaba ikimuonyesha, Catherine Benedicto wa kijiji cha Buhundwe wilayani Rorya mkoani Mara akiwa amevimba uso kwa madai ya kupigwa na mwanaume.
BAADHI ya makabila nchini yana mila ambazo kwa namna moja ama nyingine, zinakandamiza watoto ama wanawake.
Kwa kiasi kikubwa, mila hizo zinatofautiana kutoka kabila moja na jingine ama mkoa mmoja na mwingine, lakini Mara ni mkoa pekee ambao tafiti zinaonyesha, mtoto wa kike akizaliwa huko anapata majanga yote matano ya ukandamizaji wa haki zake.
Tofauti na mikoa mingine nchini, mtoto wa kike anayezaliwa Mara hujikuta katika nafasi kubwa ya kupokea vipigo kutoka kwa mume, kuolewa nyumba ndogo, kukeketwa au kubakwa, na kuolewa na kaburi.
Majanga hayo matano ni nje ya kifo ambacho kinaweza kuwa matokeo ya kipigo, kukeketwa au kubakwa.
Hii ni kwa sababu mkoani Mara, masuala ya ukatili kwa wanawake, ukeketaji, ubakaji, nyumba ndogo na binti kuolewa na kaburi ni mambo yanayotendeka licha ya juhudi za serikali, wadau na wanaharakati wa haki za binadamu kupiga vita mila za aina hiyo.
Kwa mujibu wa ripoti ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kuhusu hali ya haki za binadamu kwa kipindi cha Januari hadi Juni mwaka jana, ya mapema mwaka huu, kuna matukio ya ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu hususan kwa wanawake.
Ripoti hiyo inasema kuna matukio mengi ya unyanyasaji kwa wanawake pamoja na watoto, ambao wanafanyiwa ukatili wa kingono na kijinsia ikiwamo ukeketwaji.
Aidha, Mkurugenzi Mtendaji wa kituo hicho, Dk. Hellen Kijo-Bisimba, akizungumza na Nipashe wiki hii, alisema wanawake wa mkoani Mara wanakabiliwa na changamoto kubwa kutokana na kuendelea kudumishwa kwa mila potofu.
Alisema wakati juhudi za kukomesha mila hizo zikiendelea, matukio ya ukatili wa kijinsia ikiwamo, ukeketaji, ubakaji, vipigo, mwanamke kuolewa na kaburi na mengineyo yanaendelea mkoani humo.
KUPIGWA HADHARANI
Ukatili umekuwa ukifanyika hadharani, alisema Dk. Kijo-Bisimba, pale mwanamke atakapokuwa amefanya kosa fulani na wakati mwingine ikibainikia amefanya mapenzi nje ya ndoa huadhibiwa hadharani mwanamke huyo.
Dk. Kijo-Bisimba anasema ukatili katika mkoa huo huonekana kama matendo ya kawaida kwa kuwa huonekana adhabu inayotolewa ni ya kawaida.
“Kuna matukio mengi kama ya mtu kupigwa hadharani, kukatizwa uhai wake huku baadhi wakishuhudia, kuna matukio mengi ya ukatili,” alisema.
KABURI LA KIJANA
Dk. Kijo-Bisimba alisema ni jambo la kawaida mkoani Mara kwa binti kuozeshwa kaburi la kijana ambaye alifariki bila ya kupata mtoto.
Baada ya kuozeshwa huko, anasema, watoto ambao watazaliwa na binti huyo watatambulika kama ni wa marehemu, licha ya kuwa kiuhalisia amezaa na mtu mwingine ambaye yupo hai.
“Kimila wanasema kijana kufa bila kuacha mtoto haiwezekani, hivyo watoto watakaozaliwa watatambulika ni wa marehemu,” alisema.
MWANAMKE MWENZAKE
Dk. Kijo-Bisimba alisema mwanamke ambaye hajawahi kuzaa na umri wake ukawa umepita kumudu tendo hilo la kiafya, lakini ambaye ana uwezo kiuchumi, kimila huweza kutafuta mwanamke mwenzake na kumuoa.
Alisema mahari hutolewa na kupokelewa na familia ya binti huyo ambaye atatafutiwa mwanaume wa kuzaa naye, japokuwa watoto wanatambulika ni wa mwanamke huyo mtu mzima.
“Mwanamke kama hajazaa kwa wenzetu, anaonekana kama hana thamani hivyo anaamua kuoa binti na kumtolea mahari kama kawaida, ingawaje hafanyi kitendo chochote cha kuingilia ila anakuwa na mamlaka kama baba mwenye familia aliyeoa,” alisema.
VYOMBO VYA DOLA
Mkoa wa Mara, Dk. Kijo-Bisimba alisema, pia ni kati ya mikoa mitano inayoongoza kwa ukeketaji mabinti wadogo, na unaonekana ni ngumu kuachana na mila hiyo.
Alisema kuna msimu wa ukeketaji ambao unafahamika na vyombo vya dola, lakini vinaogopa kuzuia matukio ya ukeketaji.
“Ukeketaji unafanyika hadharani, hata polisi wanashuhudia mabinti wanapitishwa mbele yao," alisema Dk. Kijo-Bisimba. "Suala la kukomesha ukeketaji linaonekana ni changamoto kubwa.”
HANA SAUTI
Alisema unyanyasaji kwa wanawake ni moja ya matukio yanayoripotiwa mara kwa mara mkoani humo kutokana na mwanamke kuonekana ni mtu ambaye hana sauti ndani ya jamii.
“Kuna matukio ya ubakaji kwa watoto, mabinti wadogo, vitendo ambavyo vinaripotiwa kila wakati katika vyombo vya habari, vituo vya polisi," alisema Dk. Kijo-Bisimba. "Huu ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.”
Kutokana na kukithiri kwa matukio hayo, Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), ulifungua vituo vya taarifa kwa baadhi ya kata ili kuishawishi jamii kutoa taarifa kuhusu matukio ya ukatili yanayotokea.
Ofisa Programu Mwandamizi wa Ushawishi na Utetezi TGNP, Anna Sangai alisema vituo hivyo vimefunguliwa katika kata ya Nyakonga na Regicheri wilayani Tarime.
Alisema vituo hivyo vya taarifa vilifunguliwa ili ifikapo msimu wa ukeketaji taarifa zitolewe kuhusu matukio hayo pamoja na mengine ya ukatili wa kijinsia.
“Matukio ya ukatili wa kijinsia yanafanyika katika baadhi ya mikoa na maeneo ya kanda ya ziwa, ikiwamo mkoani Mara," alisema Sangai.
"Tukaona vituo vya taarifa ni muhimu ndani ya jamii ili wafikishe taarifa mapema.”
TAKWIMU
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Hamisi Kigwangalla, Februari mwaka huu, alisema asilimia 15 ya wanawake nchini, wamegundulika kuwa wameshakeketwa na kwamba takwimu hizo zinaonyesha, ukeketaji huo umekithiri katika mikoa nane, ikiwamo Mara.
“Utafiti wa kidemografia na Afya Tanzania (Tanzania Demographic and Health Survey) wa mwaka 2010 unaonyesha asilimia 15 ya wanawake wamekeketwa, takwimu hizo zipo zaidi mikoa ya kanda ya ziwa,” alisema.
Kaimu Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Halmshauri ya mji wa Tarime, Adventina Mjemla alisema kuwa idadi ya wasichana waliokeketwa mwaka 2013 ilikuwa 427 na kwa mwaka 2014 ni 351.
Alisema sababu za ukeketaji ni kuendelezwa kwa mila na desturi ikiaminiwa kuwa kunampunguzia msichana ambaye hajaolewa hamu ya kujamiiana. Aidha, inaaminika mwanamke aliyekeketwa akiolewa atatulia na mwanaume mmoja.
Novemba mwaka jana, Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania–TAMWA, kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu Duniani (UNFPA), kilifanya utafiti wa kihabari wenye lengo la kutathmini hali ya ukatili wa kijinsia.
TAMWA iliangalia zaidi ndoa za utotoni na ukeketaji kutoka mikoa 13 ya Bara na Zanzibar.
Utafiti huo ulibainisha katika wilaya ya Tarime kesi 118 za ubakaji ziliripotiwa Mahakamani mwaka huo.
0 comments:
Post a Comment