Mbali na kuburudisha jamii, kazi nyingine kubwa ya sanaa ni kuelimisha.
Tofauti na zamani, wasanii wa kiume walilazimika kuigiza sauti za kike kutokana uhaba wa wasanii hao, lakini sasa idadi ya wanawake kwenye sanaa imeongezeka.
Wengi sasa wanafanya vizuri na bila kumung’unya maneno, nipongeze hatua ambayo muziki wetu umefanikiwa kufikia.
Pamoja na pongezi zangu, kuna jambo ambalo huwa linausumbua moyo wangu kwa kukosa majibu ya maswali mengi ambayo huwa najiuliza.
Jambo hili linahusu mavazi ya wasanii wetu hususan wa kike na zaidi kwenye muziki wa kizazi kipya na filamu.
Kama ambavyo baadhi ya wasanii wamekuwa wakisema hawaishi kwa kutegemea ‘kiki’ ili kazi zao za muziki na filamu ziweze kuuzika, baadhi yao huamini kuvaa nusu uchi ni kujiongeza mashabiki.
Wao wenyewe wanaamini wanapendeza kwa kuvaa mavazi yanayoonyesha maungo ya miili yao. Kinachonishangaza, mavazi yao huwa ni tofauti kabisa na wasanii wa kiume ambayo, hujisitiri vilivyo.
Mara kadhaa nimejikuta nikizima luninga au kubadilisha chaneli pale ninapokutana na muziki au filamu yenye wasanii waliovalia mavazi ya nusu uchi.
Nikiwa mdau, huwa nakerwa na mavazi ya baadhi ya wasanii wetu wa kike ambayo badala ya kuongeza heshima kwa jamii, yanadhalilisha utu wa mwanamke.
Hakuna utafiti wowote uliowahi kufanywa ukaonyesha kuwa, mavazi ya nusu uchi yanasaidia kuongeza umaarufu wa wasanii wa kike.
Wahenga walisema chema chajiuza kibaya chajitembeza, kazi nzuri na ubunifu wa msanii ndiyo vitamuweka mwanamke katika nafasi nzuri na siyo mavazi ya aibu na yaliyokosa heshima.
Uvaaji wao una tafsiri nyingine kabisa, kwamba baadhi ya wasanii wa kike ‘wanajiuza’ na hili hawawezi kukataa kwa sababu ukweli ni kwamba hawawezi kuendelea kujipitisha kwenye mitandao kwa mavazi yanayodhalilisha, kisa wanatafuta umaarufu.
Huenda wanasahau kwamba wao ni kioo cha jamii, tabia na mienendo yao vinapaswa kufundisha na siyo kuifanya jamii ipate walakini.
Kuvaa mavazi yanayoacha wazi maungo ambayo yanapaswa kusitiriwa siyo dawa wala ushujaa, kupata umaarufu au kuonyekana kama unaweza sanaa.
Mavazi hayo huonyesha aliyevaa ni chombo dhaifu, hana anachotegemea zaidi ya maungo yake ni sio uwezo wa kazi.
Ni ukweli usiofichika kwamba wasanii hawa wanapaswa kujitafakari juu ya mienendo ya maisha yao hususan upande wa mavazi.
Mwanamke anapaswa kujisitiri vilivyo. Mbona kipindi cha mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani, wasanii hawahawa wa kike wamekuwa wakitupia picha ambazo wamevaa mavazi ya kusitiri miili yao na kuonekana wakiwa nadhifu?
Kwa kweli hakuna sababu kwa wasanii wetu kuacha wazi maungo yao kwa kudhani kwamba, kufanya hivyo kunawaweka kwenye nafasi nzuri kisanii.
Wapo wasanii wachache ambao hujiheshimu na ni maarufu akiwamo Judith Wambura ‘Jay dee’.
Kama muziki wako ni mzuri, utapata mashabiki wengi na kazi yako itauzika ndani na nje ya nchi na si kwa kuvaa mavazi yanayoweza kukutafsiri tofauti.
Mara kadhaa nimesikia wasanii wa kike wakilalamika kuwa nyuma zaidi ya wasanii wa kiume, wanadhulumiwa haki zao na wakati mwingine, kuonewa kwa kutolipwa stahiki zao wanapoalikwa kwenye matamasha mbalimbali.Mwananchi
Uonevu huo hautakoma kama watajilegeza kwa kuvaa mavazi ambayo wataendelea kuonekana viumbe dhaifu wasio na uwezo zaidi ya kutegemea, kuwatega mashabiki wao ili wapate umaarufu. Muda bado upo na nina imani kubwa kwamba, wasanii wetu wanaweza kubadilika.
0 comments:
Post a Comment