BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

MKURUGENZI NA KATIBU TAWALA WAPIMA UKALI WA RAIS WA AWAMU YA TANO JOHN MAGUFULI

RAIS John Magufuli amewatumbua Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba.

Wamechukuliwa hatua hiyo baada ya viongozi hao, kubainika kufungua akaunti nyingine inayofanana na ya Ofisi ya Waziri Mkuu ya Maafa ya Kagera kwa ajili ya kujipatia fedha.

Ameagiza vyombo vya dola, vichukue hatua kwa kila aliyehusika. Sambamba na hilo, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi Mhasibu Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Simbaufoo Swai kutokana na kuhusika katika njama hizo.

Viongozi waliotumbuliwa na Rais Magufuli ni Katibu Tawala, Amantius Msole na Mkurugenzi Steven Makonda ambao wanadaiwa kufungua akaunti yenye jina linalofanana na akaunti rasmi ya kuchangia maafa iitwayo “Kamati Maafa Kagera” kwa lengo la kujipatia fedha.

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa, kwa vyombo vya habari jana ilieleza hayo.

Msigwa asema pia kuwa kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na ofisi ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, pamoja na kutengua uteuzi huo, Rais Magufuli ameagiza vyombo vya dola vichukue hatua dhidi ya wote waliohusika katika njama za kufungua akaunti hiyo.

Taarifa hiyo ya Ofisi ya Waziri Mkuu ilieleza kuwa Majaliwa amemsimamisha kazi Mhasibu Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Swai kutokana na kuhusika katika njama hizo.

Hata hivyo, Majaliwa ametoa mwito kwa wananchi na taasisi mbalimbali, kuendelea kuchangia misaada kwa ajili ya walioathirika kwa kutumia akaunti rasmi ya “Kamati Maafa Kagera” ambayo imetangazwa na Serikali.

Wakati huo huo, Dk Magufuli amepokea msaada wa Sh milioni 545 kutoka kwa Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi kwa ajili ya kusaidia wananchi wa mkoa wa Kagera waliopatwa na maafa ya tetemeko la ardhi lililotokea Septemba 10, mwaka huu.

Rais John Magufuli na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa (kushoto) wakiangalia mfano wa hundi yenye thamani ya Sh milioni 545 iliyokabidhiwa kwao jana na Balozi wa India nchini, Sandeep Arya kwa ajili ya kusaidia waathirika wa tetemeko la ardhi mkoani Kagera. (Picha na Ikulu)


Hundi ya fedha hizo imekabidhiwa jana Ikulu jijini Dar es Salaam na Balozi wa India nchini, Sandeep Arya na baadaye Rais Magufuli akaikabidhi kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa. Katika barua yake kwa Rais Magufuli iliyosomwa na Balozi Arya, Modi alisema Serikali na wananchi wa India, wamepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kutokea kwa maafa hayo, yaliyosababisha vifo vya watu na uharibifu wa mali.

“Tunaziombea amani na uvumilivu familia zote zilizopatwa na madhara na pia tunapenda kuwahakikishia kuwa tupo pamoja na marafiki zetu Serikali ya Tanzania katika kipindi hiki kigumu” alisema.

Kwa upande wake, Dk Magufuli alimshukuru waziri huyo na Serikali yake kwa kutoa mchango huo na kutuma salamu za rambirambi, na kuongeza kuwa Serikali ya Tanzania imeguswa na moyo wa upendo ulioneshwa na wananchi wa India.

“Naomba unifikishie shukrani zangu za dhati kwa Waziri Mkuu Modi, mwambie kwa niaba ya Serikali yangu tunamshukuru sana kwa kutoa msaada huu muhimu kwa ajili ya watanzania wenzetu waliopatwa na maafa kule Kagera…,” “…Mwambie ameonesha moyo wa upendo na ushirikiano kwetu na tumefarijika kwamba marafiki zetu mmeguswa kwa namna ya kipekee na tatizo lililoipata nchi yetu” alisisitiza Rais Magufuli.

Kutoka Kigoma, Fadhili Abdallah anaripoti kuwa, wakati tathmini ya athari ya tetemeko la ardhi lililotokea mkoani Kagera, ikitarajiwa kuhitimishwa Januari mwaka ujao, mikoa mingine mitatu imeongezwa katika tathmini hiyo.

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo akizungumza mwishoni mwa ziara yake ya siku tano mkoani Kigoma, ameitaja mikoa hiyo kuwa ni Kigoma, Tabora na Dodoma.

Alisema kuwa tathmini ya awali, inaonesha kuwa mikoa hiyo imeathiriwa kutokana na tetemeko hilo na kwamba tathmini ya kina lazima ifanywe na wataalamu kujua ukubwa wa mipasuko ya miamba chini ya ardhi ili kuweza kuchukua hatua za kukabiliana na hali hiyo.

Muhongo alisema kuwa wataalamu wa miamba (Jiolojia), wanaendelea na kazi ya kufanya tathmini ya kujua hali halisi ya mipasuko mkoani Kagera, ambako kwa kiasi kikubwa ambako mkoa huo uliathirika na tetemeko.

Hata hivyo timu ya tathmini ilikuwa ikikabiliwa na upatikanaji wa vifaa, ambavyo vinaweza kuonesha mipasuko hadi kufikia kilometa 15 chini ya ardhi na kwamba tayari vifaa hivyo vimeshaagizwa.

Akielezea tahadhari za matetemeko, alisema kuwa hadi sasa hakuna utaalamu unaoweza kubaini dalili za kutokea kwa matetemeko na kwamba itachukua miaka mingi, kuweka kupata utaalam wa kuweka vifaa chini ya ardhi, kutambua jambo hilo na kwamba utafiti kuhusiana na jambo hilo bado zinaendelea.

Pamoja na hivyo, alisema kuwa serikali inaendelea kuratibu upokeaji wa misaada mbali mbali chini ya uratibu wa mkuu wa mkoa Kagera na kwamba waathirika watasaidiwa kulingana na taratibu ambazo kamati ya maafa inasimamia hilo.HABARILEO
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: