Mfungaji wa timu ya netiboli ya Polisi Morogoro, Aziza Itonya akikabiliana na upinzani mkali kutoka kwa mlinzi wa timu ya Jiji Arusha, Grace Hija (GK) wakati wa ligi daraja la kwanza netiboli Tanzania bara msimu wa mwaka 2016/2017 katika uwanja wa jamhuri mkoani Morogoro ambapo katika mchezo huo Jiji Arusha walipoteza kwa kufungwa vikapu 45-33, kushoto ni Mwanasha Aly wa Polisi Morogoro, . Picha na Juma Mtanda.
Juma Mtanda, jphtjuma@gmail.com
Michezo ya ligi daraja la kwanza netiboli Tanzania Bara msimu wa 2016/2017 imeendelea kushika kasi huku Polisi Morogoro ikipata ushindi mfululizo sambamba na vigogo wa mchezo huo, Jeshi Stars na mabingwa watetezi timu ya Uhamiaji mkoani Morogoro.
Baada ya timu ya Polisi Morogoro kupata ushindi katika michezo yake miwili mbele ya Kinondoni ya Dar es Salaam kwa vikapu 88-13 na Tanga jiji kwa kuibuka na ushindi wa vikapu 85-12, jana (juzi) iliendelea wimbi la ushindi kwa kuilaza timu ya Jiji Arusha kwa vikapu 45-33.
Katika mchezo huo timu ya Jiji Arusha iliruhusu mashambulizi kutoka kwa wapinzani wao timu ya Polisi Morogoro ambapo katika seti zote nne washindi walikuwa wakiongoza kwa vikapu 11-10 huku seti ya pili ikimalizika kwa Jiji Arusha kufungwa vikapu 23-17 wakati ya tatu iikizidiwa kwa vikapu 35-22 huku mwisho Polisi ikimaliza mchezo kwa vikapu 44-33.
Walinzi wa Jiji Arusha, Grace Hija (GA) na Hawa Abdalla (GD) walishindwa kuwazuia vyema wafugaji wa Polisi Morogoro, Mwanasha Ally (GS) na Aziza Itonya (GA) huku washambuliaji wa Madini Arusha, Agnes Mukasa (GS) na Winfrida Edson (GA) wakipata upinzani mkali kutoka kwa walinzi wa Polisi Morogoro, Amina Jumanne (GA) na Rehema Juma (GD).
Katika mchezo mungine timu ya CMTU ilipoteza mchezo wake dhidi ya Madini Arusha kwa kufungwa vikapu 45-24.
Washindi waliongoza katika seti zote nne 14-6, 24-13, 36-19 na 45-24 huku mabingwa watetezi wa ligi hiyo timu ya Uhamiaji ikiendeleza kasi yake ya kupata ushindi baada ya kuifumua Jiji Tanga vikapu 94-10 baada ya kushinda michezo yake miwili ya awali.
Timu ya Tumbaku ilizinduka katika mchezo wake wa tatu baada ya kufungwa na Uhamiaji vikapu 62-32 kuibuka tena kwa kupata ushindi mbele ya Ras Kagera kwa vikapu 84-23 kufuatia mchezo wa kwanza kupata ushindi kwa kuifunga Kinondoni kwa vikapu 90-17.
Washindi wa tatu wa Afrika Mashariki timu ya Jeshi Stars ni miongoni mwa vigogo vinavyopata ushindi mnono ambapo katika michezo ya awali imeweka kuibuka na ushindi.
Ushindi huo ni kati ya timu ya Ras Kagera waliopata wa vikapu 89-18 huku wakipata ushindi mwingine kwa kuitambia Polisi Arusha kwa kuishushia kipigo cha vikapu 64-38.
Kwa upande wa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Netiboli Tanzania (Chaneta), Zainabu Mbwilo alisema kuwa mashindano ya mwaka huu yalitarajiwa kushirikisha timu 20 lakini kutokana na changamoto mbalimbali ni timu 11 pekee zilizothibitisha ligi hiyo mkoani Morogoro.
Zainabu alitaja baadhi ya changamoto kwa baadhi ya timu kuwa wachezaji kunyima vibali vya kushiriki ligi hiyo, ukosefu wa fedha na watumishi kukosa vibali kazini hali iliyopelekea kuwa na timu chache.Chanzo/MTANDA BLOG
0 comments:
Post a Comment