BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

PROF LIPUMBA AMUONYESHA JULIUS MTATIRO JELA


MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, aliyerejeshwa madarakani na ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa,

Ametishia kuwafikisha mahakamani viongozi wote wanaodai ni wa Kamati Tendaji ya chama hicho iliyoundwa Baraza Kuu la Uongozi Taifa ikiwa wataendelea kung'ang'ania madaraka na ofisi za chama hicho.

Prof. Lipumba alitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam jana alipokutana na waandishi wa habari kwenye ofisi za chama hicho zilizopo eneo la Buguruni.

Alisema kuwa kutokana na onyo la Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Fransis Mutungi, ni vema viongozi hao wakaepuka kung`ang`ania madaraka hayo na kujifanya ni viongozi wa chama hicho.

“Msajili kamueleza (Julius) Mtatiro kwamba asiendelee kujifanya kuwa ni kiongozi wa kitaifa wa chama kwa kuwa akifanya hivyo ni kosa la jinai, anaweza kufikishwa mahakamani na akipatikana na hatia, yeye na wenzake wanaweza kupigwa faini si chini ya Sh. milioni moja ama kifungo cha miezi sita jela,” alisema Prof. Lipumba.

“Mtatiro ni mwanachama wa kawaida na mimi ndiye niliyemteua kuwa mjumbe wa mkutano mkuu na hakugombea nafasi ya kuingia katika Baraza Kuu na Katiba yetu haina utaratibu wa kamati ya uongozi kwa hiyo ni mwanachama wa kawaida afanye adabu awe na heshima na tutaendelea kumtazama kama mwanachama wa kawaida.”

Agosti 28, mwaka huu, Baraza Kuu la Uongozi la CUF lililoketi katika kikao chake cha dharura mjini Unguja, lilimteua Mtatiro kuwa mwenyekiti wa kamati ya kamati ya muda ya uongozi hadi utakapoitishwa mkutano mkuu maalumu mwingine baada ya ule wa awali kuvunjika jijini Dar es Salaam kutokana na vurugu.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari jana, Prof. Lipumba pia alisema kwa sasa anaona changamoto iliyopo katika kujenga upya chama hicho, lakini anachotaka ni kujenga upya umoja ndani ya chama hicho na kumaliza mpasuko ambao unaonekana kwa sasa.

“Kazi niliyonayo sasa ni kujenga umoja wa chama na kuusimamia kujenga umoja huo katika pande mbili za Bara na Zanzibar, (chama) chenye nguvu ili kuleta mabadiliko ya kweli, na natarajia kwamba Katibu Mkuu (Maalim Seif Sharif Hamad) ambaye yuko safari, akirejea tuendelee kufanya kazi, tuko tayari kuwaleta pamoja viongozi ili tufanye kazi na kujenga chama kimoja na nikiri kwamba kufanya kazi kwa sasa katika hali hii itakuwa ni changamoto,” alisema.

Aliongeza kuwa kama ilivyo katika chama chochote cha siasa, kinachosimamia haki, kuwa na migongano ni jambo ambalo ni la kawaida na hawawezi kuifanya kama uadui huku akitolea mfano Rais wa sasa Marekani, Baraka Obama ambaye alikwa na uadui mkubwa na Hillary Clinton wakati wanapambana kugombea nafasi ya hiyo ndani ya chama chake.

Kuhusu kikao cha Baraza Kuu la Uongozi Taifa kilichopangwa kufanyika visiwani Zanzibar leo, Prof. Lipumba alisema ni batili na hakitambui.

“Mimi ndiye mwenyekiti wa chama hiki na ndiye mwenye mamlaka ya kuandaa kikao hicho, kama sipo Katibu Mkuu ndiye anaweza kuitisha na ambaye mimi nafahamu hayupo, kwa hiyo kwa vyovyote vile, Naibu Katibu Mkuu ambaye ni Magdalena Sakaya, alipaswa kufahamu lakini na yeye hafahamu," alisema na kufafanua zaidi:

"Kwa hiyo, niseme kifupi kwamba kikao hicho hakipo na hao walioitisha hawana mamlaka hayo."

Akifafanua zaidi kuhusu uamuzi uliotolewa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Prof. Lipumba alisema anampongeza kwa kuonyesha weledi katika kutoa msimamo na mwongozo wake kuhusu mgogoro wa chama hicho kwa kuzingatia Katiba ya chama hicho.

Alisema anamshangaa Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Self kutokutambua uamuzi wa Msajili ilhali awali alionyesha kumpongeza kwa barua Msajili huyo kwa hatua anazozionyesha katika kushughulikia mgogoro huo.

“Namshangaa Katibu Mkuu baada ya Msajili kutoa uamuzi ameanza kukosoa uamuzi huo wakati kipindi ambacho mgogoro unashughulikiwa na ofisi hiyo aliandika barua ya kupongeza lakini leo hii yuleyule aliyepongeza leo anakosoa na anamuona yule aliyemuamini hafai tena,” alisema.

KUSHIRIKIANA NA CHADEMA
Alipoulizwa kuhusu msimamo wake juu ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Prof. Lipumba hakuweka wazi kama ataendelea kushirikiana, lakini akadai ataendelea kushirikiana na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) pale atakapoona kuna umuhimu wa kufanya hivyo.

Alisema msimamo wa Ukawa ulikuwa ni kuunga mkono maadili ya rasimu ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya Jaji Joseph Warioba ambayo msomi huyo alidai Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa hakuwa miongoni mwa waasisi wa umoja huo, lakini baadae viongozi wa vyama hivyo akiwamo Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif waliamua kumsimamisha Lowassa kuwa mgombea wa urais kupitia Ukawa, jambo ambalo hakukubaliana nalo.

Katika hatua nyingine, Prof. Lipumba alidai kuwa baada ya kuwasili katika ofisi hizo, hakukuta baadhi ya mali za ofisi yakiwamo magari, kompyuta za ofisi pamoja vifaa vingine.

Msomi huyo aliwaomba wanachama wa CUF waliochukua mali hizo kuzirejesha mara moja.

Kabla ya kufanyika kwa mkutano huo na waandishi wa habari, Nipashe lilishuhudia gari la polisi likiwa linazunguka katika barabara ya kuingilia katika ofisi hizo huku kukiwa hakuna makundi ya watu kama ilivyozoelea katika siku za nyuma.

Kwenye geti la ofisi hizo, ulinzi pia uliimarishwa, huku walinzi wakiwauliza maswali kila aliyekuwa anataka kuingia katika ofisi hizo kabla ya kutoa idhini ya kuingia.

Baadhi ya viongozi ambao walikuwa wanaonekana katika ofisi hizo baada ya kuteuliwa kwa Kamati Tendaji inayoongozwa na Mtatiro walionekana nje ya ofisi hizo na hata walipofuatwa kuulizwa kwa nini wako nje walisema wanasoma mazingira kuona kama ofisi hizo zinaingilika ilhali wanaona timu wa Prof. Lipumba ndiyo iko ndani.

BARAZA KUU
Wakati Lipumba akidai kikao cha Baraza Kuu la Uongozi Taifa kilichoitishwa ni batili, Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Uhusiano ya Umma wa CUF, Salum Bimani, alisema jana kuwa baraza hilo linakutana leo kwenye ofisi za makao makuu ya chama hicho zilizopo eneo la Mtendeni mjini Unguja.

Alisema kikao hicho kiliitishwa na Kamati ya Utendaji ya Taifa kutokana na kikao chake cha dharura kilichofanyika visiwani Zanzibar Septemba 24, mwaka huu.

Alisema kikao hicho cha Baraza Kuu la Uongozi Taifa kitapokea na kujadili ajenda iliyowasilishwa na Kamati ya Utendaji ya kumfikisha mbele ya baraza hilo mwanachama wake aliyesimamishwa, Prof. Lipumba ili kujieleza na kujitetea kutokana na matendo yake anayoendelea kuyafanya dhidi ya chama hicho.


“Tumeshuhudia uharibifu mkubwa katika chama na baadhi ya Wananchi wanaongozwa na Profesa Lipumba kufanya hujuma za kuvunja ofisi, kupiga na kujeruhi walinzi wa chama katika Afisi Kuu ya CUF Buguruni Dar es Salaam siku ya Jumamosi tarehe 24 Septemba 2016," alisema Bimani.nipashe
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: