Juma Mtanda, jphtjuma@gmail.com
Wakati timu za netiboli za klabu za majeshi za Uhamiaji na Polisi Morogoro zikitamba kwa kupata ushindi mfululizo ligi daraja la kwanza mchezo wa netiboli Tanzania bara, timu ya Ras Kagera yenyewe imepata radha ya ushindi wake wa kwanza dhidi ya Kinondoni ya Dar es Salaam katika michezo inayoendelea mkoani Morogoro.
Timu ya netiboli ya Ras Kagera inayonolewa na Kocha mkuu, Nora Ichwekeleza ilipata ushindi huo kwa pinde ikiwa ni mchezo wake wa tatu baada ya kupoteza michezo miwili kwa kuambulia vipigo kutoka kwa Tumbaku ya Morogoro kwa vikapu 84-23 huku wakidondokea pua kwa kutandikwa vikapu 89-18 na Jeshi Stars.
Kutokana na matokeo hayo Ras Kagera imejinasua kutoka mkiani mwa msimamo wa ligi hiyo huku Jiji Tanga ikiburuza mkia baada ya kufungwa michezo yake yote miwili huku Kinondoni ya Dar es Salaam ikishika nafasi ya pili kutoka mkiani baada ya kucheza michezo mitatu na kupoteza yote.
Wadada wa Jiji Tanga wameshindwa kufurukuta katika michezo yao miwili baada ya kupigishwa kwata na Polisi Morogoro na kufungwa vikapu 85-12 huku Uhamiaji ikiishindilia kwa vikapu 94-10.
Timu ya Kinondoni iliyoshuka dimbani mara tatu imejikuta ikiambulia vipigo mfululizo na kugawa pointi mbili kutoka kwa wapinzania wao ambapo timu ya Tumbaku Morogoro ilishusha kipigo cha vikapu 90-17 huku wakiadhibiwa na Polisi Morogoro vikapu 88-13 kabla ya jana (Juzi) kukumbana na kipigo kingine cha vikapu 45-38 kutoka kwa Ras Kagera.
Katika michezo ya jana (Juzi), Uhamiaji iliendelea wimbi la ushindi kwa kuishikisha adabu Jiji Arusha kwa vikapu 63-21 huku Tumbaku Morogoro ikipokea kipigo kutoka kwa Polisi Arusha kwa vikapu 59-56 katika mchezo uliokuwa na upinzani mkali.
Jeshi Stars ilikiona cha mtema kuni baada ya kushindwa kuhimilia mchakamchaka wa Polisi Morogoro na kukubali kufungwa vikapu 50-40 ikiwa ni mchezo wake wa kwanza kupoteza katika ligi hiyo iliyojaa upinzani.
Jiji Tanga iliambulia patupu dhidi ya Jiji Arusha kufuatia kupoteza mchezo huo kwa vikapu 70-27 huku Kinondoni ya Dar es Salaam ikishindwa kufurukuta kwa Polisi Arusha kwa kulala kwa vikapu 77-17 wakati Uhamiaji ikipata ushindi kwa kuifunga Madini Arusha vikapu 60-28 na Jeshi Stars iliizimisha ndugu zao CMTU kwa vikapu 54-30.
Michezo hiyo iliendelea (leo) jana kwa Ras Kagera kucheza na Polisi Arusha, Jiji Tanga dhidi ya Madini Arusha, Kinondoni ikishuka kucheza na CMTU huku Uhamiaji ikicheza na Jeshi Stars wakati Tumbaku Morogoro ikionyeshana umwamba na ndugu zao Polisi Morogoro.
Michezo mingine katika mabano Polisi Arusha v/s CMTU, Jiji Arusha v/s Jeshi Stars, Ras Kagera v/s Polisi Morogoro, Jiji Tanga v/s Tumbaku na Kinondoni v/s Uhamiaji.
Katika mchezo huo Jeshi Stars iliongoza katika raundi zote nne kwa vikapu kufunga 13-7 huku raundi ya pili ikipata ushindi wa vikapu 25-16 wakati raundi ya tatu ilishinda 43-20 na raundi ya mwisho ikiibuka na vikapu 45-30 vya ushindi huo.CHANZO/MTANDA BLOG
0 comments:
Post a Comment