KASHFA YA KUWAHADAA WANAWAKE YAMKOSESHA USINGIZI MGOMBEA URAIS WA MAREKANI DONALD TRUMP
Wanawake wawili wameambia gazeti la New York Times kwamba mgombea urais wa chama cha Republican nchini Marekani Donald Trump aliwashika kimapenzi bila idhini yao.
Mwanamke mmoja amesema mgombea huyo alimshika matiti na kujaribu kuingia mkono wake chini ya sketi yake wakiwa kwenye ndege miongo mitatu iliyopita.
Wa pili anasema Trump alimpiga busu bila yeye kutaka katika jumba la Trump Towers mwaka 2005.
Maafisa wa kampeni wa Trump wamesema "makala hii yote ni hadithi ya kubuni".
Gazeti la New York Times limeanzisha kampeni "ya uongo, na iliyoratibiwa kumharibia jina kabisa", taarifa ya maafisa wa Trump imesema.
Jessica Leeds, 74, kutoka Manhattan, ameambia gazeti hilo kwamba alikuwa ameketi karibu na Trump sehemu ya abiria wa hadhi ya juu kwenye ndege wakielekea New York pale alipoinua sehemu ya kupumzishia mkono kitini na akaanza kumshika.
Mwanamke huyo alikuwa na umri wa miaka 38 wakati huo.
"Alikuwa kama pweza .... mikono yake ilinishika kila pahali," anasema. "Ulikuwa ni unyanyasaji."
Rachel Crooks alikuwa mpokezi wa wageni katika kampuni ya kuuza ardhi ya nyumba katika jumba la Trump Tower, wakati huo akiwa na miaka 22.
Anasema alipigwa busu la lazima na Trump nje ya lifti ya jengo hilo.
"Ilikuwa vibaya sana," Bi Crooks ameambia New York Times.
"Niliudhika sana kwamba alidhani nilikuwa sina maana kiasi kwamba angefanya hivyo (bila hiari yangu)."
Wawili hao hata hivyo hawakuripoti visa hivyo kwa maafisa wa serikali.
Hata hivyo, wanasema waliwaambia marafiki na jamaa zao yaliyojiri.
Bi Leeds anasema alikasirika sana na alitatizika kimawazo baada ya Trump kumgusa.
Anasema mara moja aliondoka eneo la abiria wa hadhi na kwenda kuketi eneo la abiria wa kawaida.
Maafisa wa kampeni wa Clinton wamesema simulizi hizo za kuogofya kwenye New York Times zinatilia mkazo "kila kitu ambacho tunajua kuhusu jinsi Donald Trump huwachukulia wanawake".
'Kumshika makalio'
Hayo yakijiri, Mindy McGillivray naye ameambia gazeti la Palm Beach Post kwamba akiwa na miaka 23 , Bw Trump alimshika makalio katika kilabu chake cha Mar-a-Lago club jimbo la Florida mwaka 2003.
Anasema alikuwa amesimama karibu na mchumba wake wa wakati huo Melania Knauss.
Bi McGillivray, ambaye kwa sasa ana miaka 36, anasema hakuripoti kisa hicho kwa polisi.
Lakini mwenzake, mpiga picha Ken Davidoff, aliambia gazeti hilo kwamba mwanamke huyo alimwita kando siku hiyo na kumwambia: "Donald amenishika makalio sasa hivi".
Maafisa wa Trump wanasema madai ya Bi McGillivray hayana ukweli wowote.
Wanawake wote watatu wamesema wanaunga mkono Bi Clinton.
Ijumaa wiki jana, video iliyopigwa mwaka 2005 ilitokea na kumuonyesha Trump akinena maneno ya kuwadhalilisha wanawake na kuongea kuhusu kuwapapasa wanawake.
Aliomba radhi kuhusu matamshi hayo, lakini akasema yalikuwa mazungumzo ya mzaha faraghani.
Viongozi wengi wakuu wa Republican, akiwemo Spika Paul Ryan, wameshutumu matamshi hayo. Ryan alisema hatamtetea tena Trump.BBC
0 comments:
Post a Comment