ASKARI POLISI WATIMUA MBIO BAADA YA KURUSHIWA MISHALE NA WAUZA MADAWA YA KULEVYA
Picha ya maktaba mlenga shabaha akilenga kitu kwa kutumia upinde wenye mshale
ASKARI polisi waliokuwa kwenye kizuizi cha njia za panya maarufu kama ‘Kitobo’ wamenusurika kuuawa kwa mishale na watu wanaodaiwa kufanya biashara ya kusafirisha binadamu, bidhaa za magendo na dawa za kulevya, karibu na mpaka wa Tanzania na Kenya, wilayani Mwanga.
Habari zilizoifikia Nipashe na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Kamishna Mwandamizi Msaidizi wa Polisi, Wilbrod Mutafungwa, watu hao wanadaiwa kusaidiwa na askari mgambo wasio waaminifu.
Kamanda Mutafungwa ingawa hakutaja idadi ya askari walionusurika katika tukio hilo, lakini ni kweli limetokea.
“Ni kweli kuna askari polisi wamenusurika kuchomwa mishale na watu wenye nia ovu baada ya kuimarisha ulinzi kwa kuweka kizuizi kuzuia magendo katika kijiji cha Kileo ambacho kipo mpakani mwa Tanzania na Kenya," alisema.
Juzi Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Kilimanjaro ilizuru eneo hilo na ndipo Kamanda Mutafungwa alipotoboa siri hiyo wakati alipokutana na kuzungumza na wananchi wa kata ya Kileo mbele ya mkuu wa mkoa huo, Saidi Mecki Sadiki.
Akionyesha kushangazwa na tukio hilo, kamanda huyo wa polisi alisema eneo hilo lina mwenyekiti wa serikali ya kijiji ambaye ana jukumu la kuhakikisha ulinzi na usalama unakuwapo muda wote, lakini pia limetokea wakati kijiji hicho kikiwa na askari mgambo zaidi ya 300.
Alisema baadhi ya askari mgambo katika eneo hilo wanatuhumiwa kupewa fedha na kujihusisha na vitendo vya kuwahujumu polisi kwa kutoa taarifa kwa wahalifu wakati wanaposafirisha bidhaa za magendo, mirungi na wahamiaji haramu.
Alisema eneo hilo ambalo zamani lilikuwa na kituo cha polisi lilihujumiwa kwa kituo hicho kuhamishiwa eneo la Kifaru kwa lengo la kudhoofisha ulinzi na usalama ili kufanikisha wafanyabiashara kufanya shughuli zao za kusafirisha bidhaa za magendo bila kizuizi.
Maeneo ya kata hiyo ya Kileo maarufu kama Kitobo, yanasifika kwa usafirishaji wa bidhaa za magendo na wahamiaji haramu kutoka nchi jirani, pamoja na wafanyabiashara wanaokwepa kulipa kodi ya serikali kwa kusafirisha mafuta ya taa na bidhaa za viwandani kwa njia zisizo halali.
0 comments:
Post a Comment