Dar es Salaam. Mahakama Kuu imebariki maombi ya CUF ya kumfungulia kesi Msajili wa Vyama vya Siasa pamoja na Profesa Ibrahim Lipumba na watu wengine waliosimamishwa uanachama wa chama hicho cha kisiasa.
Wakati Mahakama Kuu ikikubali maombi hayo, Profesa Lipumba amesema hakukuwa na haja ya kupeleka mahakamani suala hilo kwa kuwa litapoteza muda.
Uamuzi huo ulitolewa jana na Jaji Ama - Isario Munisi baada ya Bodi ya Wadhamini ya CUF kuwasilisha maombi ya kufungua kesi mahakamani hapo dhidi ya Profesa Lipumba, aliyejiuzulu uenyekiti wa chama hicho na baadaye kuvuliwa uanachama lakini hatambui uamuzi huo.
Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi ameingia kwenye orodha hiyo baada ya kutangaza msimamo wa ofisi yake wa kumtambua Profesa Lipumba kuwa mwenyekiti licha ya mkutano mkuu kuridhia barua yake ya kujiuzulu.
Katika maombi hayo namba 75 ya mwaka 2016, bodi hiyo inataka kumshtaki Msajili Mutungi, Profesa Lipumba na wanachama wengine, pamoja na mambo mengine, kupinga uamuzi wa kumtambua msomi huyo kuwa mwenyekiti halali wa CUF.
Wakili wa bodi hiyo, Juma Nassoro aliieleza Mahakama jana kuwa kuna barua ya Msajili wa Vyama vya Siasa ambayo inamtambua Profesa Lipumba kama mwenyekiti wa Taifa wa CUF, na kwamba kitendo hicho ni kutengua uamuzi wa vikao vya chama wa kukubali uamuzi wa Profesa Lipumba kujiuzulu uenyekiti, kusimamishwa kwake na hatimaye kuvuliwa uanachama.
Alisema kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa na kanuni zake, msajili hana mamlaka na kwa sababu hiyo, wanaomba kibali cha kuwasilisha maombi ya kuiomba Mahakama hiyo itengue barua hiyo.
Pia Wakili Nassoro aliwasilisha vielelezo mbalimbali, ikiwamo barua hiyo ya msajili na nakala za uamuzi wa chama hicho dhidi ya Profesa Lipumba na wenzake.
Akitoa uamuzi wake, Jaji Munisi alisema baada ya kusikiliza hoja hizo na kupitia vielelezo vilivyowasilishwa, amejiridhisha kuwa maombi hayo yanakidhi vigezo vyote vya kupata kibali kilichoombwa.
Hivyo, Jaji Munisi ameiagiza CUF ndani ya siku 14 kama sheria inavyoelekeza, kuwasilisha maombi yake hayo ya kuomba Mahakama itengue barua ya Msajili wa Vyama vya Siasa inayomtambua Profesa Lipumba.
Akizungumza baada ya uamuzi huo, Wakili Nassoro alisema wanajipanga kuwasilisha maombi hayo ndani ya siku saba na kwamba wataiomba mahakama imzuie msajili kufanya kazi nje ya mipaka yake ya kisheria kama kuingilia mambo ya ndani ya vyama vya siasa.
Akizungumzia hatua hiyo, Profesa Lipumba alisema mgogoro ndani ya CUF ungeweza kuzungumzwa na kumalizwa ndani ya chama. “Suala la kupeleka mahakamani linachukua muda badala ya kujenga chama.
Mimi sijapata shauri hilo. Kwa hiyo nikirudi Dar tutatoa majibu, lakini kwa kweli ni jambo ambalo linanifehedhesha,” alisema.MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment