BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

MAKAMU MWENYEKITI AFURAHISHWA CCM KUFUKUZA WANACHAMA 100

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Philip Mangula, amefurahishwa na uamuzi wa chama hicho mkoani Mwanza kuwafukuza wanachama 100 wakidaiwa kukisaliti chama hicho wakati wa uchaguzi mkuu uliopita.

Alisema huwezi kujiita mwanachama wa CCM ambaye badala ya kuonesha uzalendo wao katika chama ili kishinde vita ya kushika dola, wao wanakisaliti jambo ambalo haliwezi kuwafanya waitwe wanchama bali ni jeshi la kukodiwa.


Mangula aliyasema hayo jana, wakati akizungumza na vijana wanaosoma na waliohitimu vyuo vikuu 20, ambao wameweka kambi ya kufyatua matofali kwa ajli ya ujenzi wa mabweni na nyumba za walimu katika Shule ya Sekondari Nasabagani, Mkuranga, mkoani Pwani.


“Taarifa ya CCM kuwafukuza uanachama 100 kule Mwanza imenifurahisha sana, naamini hatua kama hizi zitaendelea kuchukuliwa kila mahala nchini kwa wasaliti wote.


“Hivi ni mchezaji gani anayempiga ngwara mchezaji wa timu yake wakati wa mechi ya kutafuta ubingwa halafu akaachwa aendelee kuwa katika timu,” alihoji Mangula kwa mshangao.


Aliongeza kuwa, wakati mikoa itaendelea kuchukua hatua, ngazi ya Taifa nao wataendelea kuchukua hatua dhidi ya wasaliti wote na kukata majina yao kama wataomba kugombea nafasi za uongozi kwenye uchaguzi wa chama mwaka 2017.


Aliwataka vijana nchini kote hasa wasomi, kuepuka kutumiwa vibaya na wanachama wanaosaka uongozi katika Uchaguzi Mkuu wa CCM na kijana yeyote ambaye atabainika kutumiwa vibaya atakuwa amekisaliti chama hivyo, hafai kuwa mwanachama.


“Hili la kutumiwa vibaya hasa vijana, nawaasa mliepuke hili ni jambo baya si kwa chama pekee hata kwa wewe uliyekubali kutumika maana utatumiwa kama ngazi.


“Mgombea aliyekutumia akipita, hatakuwa na manufaa kwako na Taifa maana atakuwa mvurugaji tu badala ya kushiriki kuleta maendeleo ya chama na Taifa,” alisisitiza.


Alisema vijana 53 waliojitolea kufyatua matofali kwa ajili ya ujenzi wa mabweni na nyumba za walimu, wameonesha moyo mkubwa wa uzalendo kwa nchi yao na ndiyo uzalendo wa kweli unaopaswa kuoneshwa na kila mwananchi hasa viongozi katika ngazi mbalimbali.


Mangula alisema vijana hao wameonesha mwamko uliokuwa umejengwa na Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, ambao umetoweka kwa vijana wengi baada ya mfumo wa vyama vingi vya siasa.


Aliongeza kuwa, umefikia wakati kipimo cha kwanza kwa yeyote kupata uongozi kiwe uzalendo wake na utayari wa kufanya kazi za kujitolea katika jamii badala ya kutazama uwezo wa kuzungumza na kumwaga hotuba nzuri majukwaani.


“Sifa za mtu kupewa uongozi isiwe ukasuku wa kutoa talalila za hotuba nzuri za kisiasa majukwaani, atazamwe kama amekuwa akitoa mchango gani kwa jamii, kufanya kazi za kujitolea ili kusukuma maendeleo ya Taifa kama ilivyokuwa wakati wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere,” alisema.


Awali Katibu wa Kambi ya vijana hao, Daniel Sarungi, alisema, tangu walipoanza kambi ya kufyatua matofali Septemba 29, mwaka huu, wamefanikiwa kufyatua tofali zaidi ya 30,000, lengo ni kufyatua tofali 45,000 na kazi hiyo wataikamilisha leo.


Alisema wamejikusanya kutoka vyuo vikuu 20, vitatu kutoka nje ya nchi na kushirikiana vizuri katika kazi ya kusomba mchanga, kufyatua tofali, kujipikia chakula, kufundisha wanafunzi wa kidato cha tano na sita katika shule hiyo, kutoa huduma ya afya, kushiriki michezo mbalimbali na kufanya semina na mijadala ya kukuza uwezo wa kuleta maendeleo ya jamii.


Sarungi alisema vijana hao ambao baadhi wamehitimu masomo na wengine wakiendelea kusomea taaluma mbalimbali, wameamua kusaidia ujenzi wa mabweni na nyumba za walimu baada ya kuguswa na adha ya wanafunzi wa kidato cha tano na sita kulala chini katika shule hiyo, walimu wakiwa hawana nyumba za kutosha kwa ajili ya makazi.


“Wakati wanafunzi waliopo sasa wanalala chini katika chumba cha maabara, nyumba moja yenye vyumba vitatu inatumiwa na walimu saba kuishi, hali ambayo hairidhishi,” alisema.


Mangula alishiriki kufyatua matofali akiwaunga mkono vijana hao baada ya kusikia taarifa zao kwenye vyombo vya habari baada ya kuhamasishwa na Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Filberto Sanga ambaye naye amekuwa akishiriki kufyatua matofali hayo.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: