MAMA ASILIMULIA NAMNA KUNDI LA KIHARIFU LA BLCK AMERICANS WALIVYOMVAMIA SAA 9: 00 USIKU DAR ES SALAAM
WAKATI Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam likiendelea kusaka wahalifu wa kundi linalojiita Black Americans.
Mmoja wa watu waliokumbwa na mkasa wa kuvunjiwa nyumba na vijana hao, ameeleza jinsi ambavyo waliweza kutumia dakika 15 kupekua kila pembe ya nyumba yake na kutishia kumchinja mwanaye.
Fotunata Mmari, mkazi wa Mtaa wa Mponda uliopo Mbagala jijini Dar es Salaam, alisema tukio hilo lilitokea Septemba 21 majira ya saa 9:25 usiku.
Alisema katika tukio hilo, vijana zaidi ya 10 wakiwa na umri kati ya miaka 15 na 20, walivamia nyumba yake huku wakiwa na kiongozi wao ambaye ana umri wa kati ya miaka 35 na 40.
Alisema vijana hao waliweza kuingia ndani ya nyumba baada ya kuvunja mlango na geti la mlango la chuma kwa kutumia kilipuzi.
“Nadhani walitumia baruti ama kilipuzi kingine ila inaonekana ni wataalamu kwa sababu kupitia huo mlipuko mmoja, waliweza kuvunja mlango na geti lake la chuma wakaingia ndani," alisema na kueleza zaidi:
"Walivyoingia ndani tu, walitawanyika kila mmoja kwenye chumba chake wakaanza kutafuta vitu, waliingia kwenye chumba cha watoto na dada wa kazi wakapekua kila mahali, walipokosa kitu wakachukua simu yake, wakawa wanaingia kwenye chumba kingine wakakutana na bibi anatoka mmoja akauliza ‘huyu ndiye mama’ mwenzake akasema ‘siyo’ wakamsukumia ndani.
"Kule kwenye chumba cha dada walivyochukua simu, walimchukua na kumwambia tuonyeshe chumba cha baba, walivyokuja wakataka kuvunja mimi nikawaambia wasivunje nikaamka na kufungua mlango na kulala chini.
"Wakati wote tu walikuwa wanasema tunataka fedha na sisi hatukuwaambia kwamba hatuna ila tuliwaambia tu chukueni chochote mnachoona kinawafaa, wakaingia kwenye makabati kila mahali walipekua, lakini hawakupata fedha zaidi walichukua 'vihela' kidogo tu na 'laptop' (kompyuta mpakato), simu kama tano hivi.”
Alisema wakati tukio hilo likiendelea ndani ya nyumba kukiwa na vijana hao zaidi ya 10, kundi kubwa zaidi lilikuwa nje ya nyumba huku likionya majirani kutofika kutoa msaada.
"Waliwaambia majirani ole wake mtu atakayethubutu kutoka nje."
Alisema kutokana na kutishiwa huko, walishindwa kutoka hali iliyofanya waliokuwa ndani wazidi kupekua kila kona ya nyumba hiyo.
Alisema wakati wengine wakiwa wanazidi kupekua, mwingine alishika mtoto akawa anatishia kumchinja akidai wazazi hao watoe fedha ili kuokoa maisha ya mtoto wao.
“Wakati hayo yakiendelea majirani walikuwa wameanza kupuliza filimbi kuashiria hatari na nadhani waliokuwa nje walitoa ishara kwa wenzao waliokuwa ndani kwa hiyo wakatoka na kuacha familia bila kumdhuru mtu."
Alisema ingawa yeye siyo mtu anayekaa na fedha ndani, kundi hilo lilipovamia nyumba yake, lilionekana kwamba ni watu waliotarajia kupata kiasi kikubwa cha fedha.
Alisema tangu siku ya tukio, licha ya kutoa ripoti polisi na kuwapa namba maalumu za simu (IMEI) zilizoibiwa ili kuzitumia kusaka wahalifu hao, bado hajataarifiwa kuhusu kukamatwa kwa mtu yeyote kutokana na tukio hilo.
“Wangeamua kutumia hizo IMEI, naamini kabisa wangeweza kujua wako wapi hao wahalifu kwa sababu wapo mtaani na kila siku wanafanya matukio, sasa kwanini hawakamatwi?" Alihoji.
"Kuna sungusungu mtaani na kuna tetesi kwamba wanawafahamu, kwanini hawawakamati?”
Alisema kama viongozi wa mtaa wake wangeamua kufanya mkutano na kuweka mikakati ya ulinzi, jambo hilo lingepatiwa ufumbuzi.
Jumapili iliyopita, kundi la vijana hao lilifanya uhalifu katika mitaa ya Mianzini na Mponda iliyopo Mbagala wilayani Temeke na kutoa damu majeruhi watano kwa mapanga, marungu na visu.
Miongoni mwa waliojeruhiwa katika tukio hilo lililotokea alfajiri ni askari wa Jeshi la Wananchi (JWTZ), Jerald Malilo, ambaye alipata majeraha makubwa kichwani na kulazimika kulazwa kwenye Hospitali ya Lugalo jijini.
Tukio hilo lilitokea alfajiri wakati majeruhi hao wakitoka majumbani kwao kuelekea vituo vya mabasi kuwahi maeneo yao ya kazi.Nipashe
0 comments:
Post a Comment