BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

MIKOSI NDANI YA CUF YAENDELEA KUMWANDAMA PROF LIPUMBA, SASA YAHAMIA MIKOA YA LINDI NA MTWARA

 
CHAMA cha Wananchi (CUF) Kanda ya Kusini inayojumuisha mikoa ya Lindi na Mtwara kupitia wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi Taifa, kimesema hakimtambui Profesa Ibrahim Lipumba, kama kiongozi halali wa chama hicho.

Msimamo huo ulitolewa na wajumbe hao pamoja na baadhi ya wadhamini wa chama hicho walipokuwa wanazungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kumalizika kwa kikao cha Kamati ya Utendaji ya kanda hiyo kilichofanyika katika ofisi ya CUF iliyopo Mtaa wa Msonobarini Manispaa ya Lindi juzi.

Katika kikao hicho kilijumuisha Mdhamini wa chama hicho, Abdallah Khatau, kutoka Wilaya ya Masasi, wabunge wa majimbo ya Tandahimba na Kilwa Kusini, Ahamad Khatani na Selemani Said Bungara (Bwege), Mwenyekiti wa CUF Wilaya ya Lindi Mjini, Salum Bar’wani na viongozi wengine mbalimbali.

Akiwasilisha tamko hilo kwa niaba ya wajumbe wenzake mbele ya waandishi wa habari, Mwenyekiti wa CUF mkoani Lindi, Bar’wani alitaja sababu mbalimbali zilizowafanya wachukue jukumu la kutomtambua Profesa Lipumba kuwa ni kutokana na kitendo chake cha kujiondoa kwenye nafasi yake wakati wakiwa katika mapambano ya uchaguzi.

Sababu nyingine zilizotajwa ni pamoja na kutekeleza na kuheshimu maamuzi halali yaliyotolewa na uongozi wa Baraza Kuu la chama hicho yaliyofanyika Zanzibar hivi karibuni.

“Profesa Lupumba alituacha tukiwa kwenye mazingira magumu tena ya uchaguzi, wanachama na wazee wakamsihi asichukue uamuzi wa kujiuzulu, lakini hakukubali. Tumevuka safari yetu salama sasa anataka kurejea. Tunasema hatupo tayari kufanya kazi na yeye, aende chama chochote lakini siyo CUF,” alisisitiza Bar’wani.

Aidha, wajumbe hao wamekanusha tamko lililotolewa na baadhi ya watu wanaojiita viongozi kwamba wanamuunga mkono Profesa Lipumba.

Wajumbe wa chama hicho Kanda ya Kusini, wamesema wanaungana na viongozi wenzao kupinga msimamo wa ushauri wa Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi akisema ushauri dhidi ya kumrejesha na kumtambua Profesa Lipumba kuwa ni kiongozi, ni kwenda kinyume cha katiba ya chama hicho.

Bar’wani alisema kwa mujibu wa Katiba ya CUF, Ibara ya (65) kifungu kidogo cha kwanza, Kamati ya Utendaji za wilaya kwa nchi nzima, ni pamoja na kusimamia maamuzi yanayotolewa na mikutano na vikao mbalimbali ikiwamo Kamati Utendaji Taifa, Baraza Kuu, uongozi taifa na mkutano mkuu taifa.

Aidha, tamko hilo limewataka watendaji wa wilaya Kanda ya Kusini Lindi na Mtwara, kutomuunga mkono Profesa Lipumba kwa kuwa si kiongozi anayeitakia mema CUF. 


Pia wamewaomba wanachama na wakereketwa kuwa na subira wakati viongozi wa kitaifa wakiendelea kushughulikia mgogoro unaoendelea kufukuta ndani ya chama chao.Nipashe
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: