BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

ALIYECHOMWA MKUKI MDOMONI NA KUTOKEA SHINGONI AANZA KUONGEA NA KUNYWA UJI MORO


Juma Mtanda, Morogoro.
Augostino Mtitu (42) aliyenusurika kifo baada ya kuchomwa mkuki mdomoni na kutokea nyuma ya shingo ameanza kupata nafuu na kuongea kwa mara ya kwanza tangu kukumbwa na mkasa huo katika tukio lililotokea sikukuu ya krismasi mwaka huu mkoani Morogoro.

Moja ya sababu ya mkulima huyo kunusurika kifo imelezwa kuwa mkuki huo haukuweza kugusa mishipa mikuu mitatu inayopitisha damu kutoka kwenye moyo kwenye kichwani, ubongo, uti wa mgongo na endapo mishipa hiyo ingeguswa damu ingevuja ngingi na kupelekea kifo.

Tukio hilo lilitokea katika kitongoji cha Upangwani kijiji cha Dodoma-Isanga kata ya Masanze wilaya ya Kilosa majira ya saa 5 asubuhi baada ya kuzuka ugomvi unaodaiwa kuanzishwa na wafugaji dhidi ya wakulima kwa kuingiza mifugo katika shamba lenye mazao.

Akizungumza kwa taabu kutokana na maumivu ya majeraha ya mdomo hospitali ya rufaa ya mkoa wa Morogoro alikolazwa, Augostino Mtitu alisema anawashukuru madaktari waliowezesha kumfanyia upasuaji na kuutoa mkuki salama na sasa ameanza kupata nafuu ikiwemo kuongea na kunywa uji.

Mtitu alisema kuwa afya yake imeanza kuimarika tofauti na siku ya tukio na baada ya kufanyiwa upasuaji ulionusuru maisha yake.

“Baada ya chomwa mkuki na yule mfugaji sikuweza hata kumeza mate katika mdomo wangu kutokana na maumivu lakini hata baada ya kufanyiwa upasuaji bado mdomo ulikuwa umevimba kutokana na majeraha ya kuchomwa na mkuki na hawa madaktari nawashukuru sana kwa kazi yao kubwa ya kiutatibu.”alisema Mtitu.

Mtitu aliongeza kwa kusema kuwa, leo asubuhi (jana) alianza kunywa uji na kuongea japo kwa taabu lakini anamshukuru mwenyeji mungu kwa hatua hiyo ambayo ilikuwa kipindi kigumu kwake kumtokea katika maisha yake kutokana na tukio hilo lililojaa majonzi.

Akielezea namna tukio hilo lilivyomkuta, Mtitu alisema kuwa siku ya tukio alisikia sauti ya mtu kuomba msaada ambapo alitoka nyumbani kwake na kuifuata sauti ilikokuwa inatoka mita chache tu kutoka eneo la tukio.

“Baada ya kuisikia ile sauti nilitoka nyumbani na kwenda kwenye shamba ambalo lipo jirani na nyumba yangu na kumkuta mkazi mwenzangu akishambuliwa na wafugaji wakati wakimpiga kwa fimbo na sime, mimi na wenzangu tulifanikiwa kumuokoa katika kundi lile la wafugaji.”alisema Mtitu.

Mtitu alisema kuwa baada ya zoezi la kumuokoa mwenzao, yeye alianza kukimbia huku akikwepa mawe manne yaliyokuwa yakirushwa na wafugaji hao lakini alizidiwa ujanja na kuchomwa mkuki baada ya kumzingira katika vurugu hizo na watu walipokusanyika wengi walitimua mbio na kuacha mifugo yao.

Mganga Mfawidhi hospitali ya rufaa mkoa wa Morogoro, Dk Francis Semwene alisema kuwa Augustino Mtitu alichomwa mkuki katikati ya pua na mdomo juu na kutoboa chini ya ngozi ya nyuma ya shingo yake.

Dk Semwene alisema kuwa mkuki huo haukuweza kugusa mishipa mikuu mitatu inayopitisha damu kutoka kwenye moyo kwenye kichwani ambapo hali hiyo iliwapa matumaini madaktari kufanya kazi ya upasuaji wa kuutoa mkuki huo kiurahisi.

“Unajua awali tulidhani ule mkuki ulikuwa umegusa moja ya mishipa mikuu mitatu inayopitisha damu kutoka kwenye moyo kwenda kichwani na katika ubongo lakini baada ya uchunguzi wa kina tukadundua kuwa umetoboa chini ya pua na mdogo wa juu na kupita eneo la wazi ndani ya mdomo kisha kutokea kwenye chini ya ngozi ya nyuma ya shingo”.alisema Semwene.

Mishipa hiyo ni ile inayopita eneo la nyuma ya shingo, ikipitisha damu katika mshipa wa fahamu, mshipa wa damu chafu na ule mshipa wa damu safi na endapo mkuki huo ungegusa kati ya mishipa hiyo, damu nyingi ingevuja na ingesababisha kifo kwa mgonjwa. Dk Semwene.

Chanzo cha ugomvi huo kinadaiwa kuanzishwa na wafugaji kuingiza mifugo shamba la Dotto Mfaume ambapo, Yohana Wisa aliyekuwa jirani aliweza kuziona na kwenda kuziondoa ili isiharibu mazao.

Kitendo cha, Yohana Wisa kutoa mifugo hiyo shambani ndicho kilichowakasirisha wafugaji waliokuwa eneo hilo na kumshambulia kwa sime na fimbo na kuvunja mkono wa kulia kabla kuchomwa kwa mkuki mdomoni, Augostino Mtitu.

Kutokana na ugomvi huo kati ya wafugaji na wakulima watu tisa walijeruhiwa na kukimbizwa katika hospitali ya wilaya ya Kilosa katika tukio hilo huku baadhi ya viongozi wa kitongoji cha Upangwani na kijiji cha Dodoma-Isanga katika kata ya Masanze mkoani Morogoro wakijeruhiwa.

Wilaya ya Kilosa ni miongoni mwa wilaya za mkoa wa Morogoro zenye migogoro mingi ya wafugaji na wakulimu na inayopelekea watu kupoteza maisha na kupata ulemavu wa kudumu ambapo mpaka sasa bado ufumbuzi wa kudumu haujapatiwa kukomesha vitendo hivyo.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: