Na Juma Mtanda, Morogoro.
Tukio la mauaji ya watu wawili na mmoja kujeruhiwa baada ya kupigwa risasi katika kijiji cha Kisaki Stesheni kata ya Kisaka limechukua sura mpya baada ya askari wa jeshi la polisi kutajwa kuhusika moja kwa moja katika tukio hilo mkoani Morogoro.
Akizungumza na waandishi wa habari mkoani hapa, Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro, Urlich Matei alisema kuwa askari wa jeshi hilo ndio waliofyatua risasi na kuwashambulia raia wawili na kupoteza maisha huku mmoja akijeruhiwa na kulazwa hospitali ya rufaa ya mkoa huo.
Kamanda Matei akifafanua juu ya tukio, alisema kuwa jumla ya risasi 22 zilifyatuliwa na jeshi hilo linafanya uchunguzi kwa askari waliokuwa katika tukio hilo.
“Desemba 19 mwaka huu majira ya saa 1 usiku, askari polisi walitumwa kwenda Kisaki kukamata wahalifu wa makosa makubwa na desemba 21 majira ya saa 1 usiku walifanikiwa kukamata watu watatu.”alisema Kamanda Matei.
Aliwataja watuhumiwa waliokamatwa katika tukio hilo kuwa ni Ushindani Salum, Ally Ngohamweru na Mussa Bakari lakini wakati ukamataji unaendelea wananchi walikusanyika na kuwataka askari wawachie watuhumiwa.alisema Kamanda Matei.
“Askari waliwataka wananchi kutawanyika eneo hilo baada ya kujitambulisha na kuonyesha vitambulisho vyao vya kazi lakini baadhi yao waliitikia wito wa kutawanyika kwa amani na wengine walikaidi amri hiyo na baadaye walifunga barabara kwa kuweka magogo.”alisema Kamanda Matei.
Wakati askari hao wakiondoa magogo, wananchi walirusha mawe na kumjeruhi mmoja wa askari hao mguuni na kuvunja kioo cha gari.
Baada ya fujo hizo, Kamanda Matei alisema kuwa askari hao waliwasihi wananchi kuacha fujo ndipo lilipochukuliwa jukumu la kufyatua risasi 22 na kati ya risasi hizo mbili ziliwachambulia watu wawili ambao walifariki dunia.
Aliwataja waliofariki dunia kuwa ni Daud Simon na Ally Said Mtengani huku mtu mmoja, Juma Malekela akijeruhiwa na kulazwa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Morogoro.
“Ni makosa na ni marufuku kwa raia yeyote kumzuia askari kufanya kazi lakini ni kosa la jinai kumshambulia askari kwa vyovyote vile isipokuwa kama ndugu yako amekamatwa njia raisi ni kumfuatilia kituo cha polisi.”alisema Kamanda Matei.
Akizungumza na MTANDA BLOG juu ya tukio hilo, Mwenyekiti mstaafu wa serikali ya kijiji cha Kisaki Stesheni, Ismail Ng’anji (Rage) alisema kuwa juzi (desemba 21) majira ya saa 3 usiku walionekana askari wakiwa kwenye magari matatu katika kijiji hicho.
Ng’anji alisema kuwa askari hao walijitambulisha kama ni askari lakini baadhi yao walikuwa na sare na wengine walivaa kiraia hali iliyozua hofu ya kutowaamini hasa kwa baadhi ya wananchi kuwaamini kama ni kweli askari ama laa.
Kaimu Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Kisaki, Yusuph Jasho alisema kuwa tukio hilo lisingeweza kutokea endapo tu taratibu za kisheria kama zingefuatwa kwa askari kushirikiana na uongozi wa kijiji katika kukamata wahalifu hao ungefanyika.
Jasho alisema kuwa wananchi hawakuwajua watu hao na hawajulikani huku wakiingiwa na mashaka wakati wa ukamataji wa watuhumiwa hao kijiji hapo.
“Maiti tumewazika jana (juzi) majira ya saa 11 jioni katika kijiji cha Kisaki baada ya kufanyiwa uchunguzi na mganga majira ya saa 4:46 asubuhi na mkuu wa upelelezi mkoa wa Morogoro aliruhusi ndugu kuchungua miili ya maiti hao kwenda kuzika”alisema Jasho.
Jasho akielezea juu ya mazingira ya tukio hilo la mauaji hayo, alisema kuwa isingeweza kutokea mauaji kama askari wangekubali ushauri wa wananchi wa kuwataka kwenda ofisi ya kijiji na kuonana na viongozi lakini badala yake askari hao waliwatoroka wananchi hao kwa gari na kuendelea na kamatakama ya watuhumiwa wao.
“Kitendo cha askari kuwatoroka kundi la wananchi wakati wanaelekea ofisi za kijiji kisha kuendelea na zoezi lao, ndio chanzo cha vurugu iliyosababisha askari kufyatua risasi na kuwaua watu wawili na kujeruhi baada ya kuweka magogo barabarani na vurugu wakati askari hao wakirejea Morogoro mjini.”alisema Jasho.
Jana (juzi) Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei alilieleza gazeti hili kuwa mauaji ya watu hao yalitokana na kundi la watu watano wanaovuruga amani katika kijiji hicho.
0 comments:
Post a Comment