KILIMO CHA BANGI SASA CHAUNDIWA MBINU MPYA YA KULIMA, LENGO KUKWEKA POLISI
KUNA mfumko mkubwa wa kilimo cha bangi nchini; na sasa baadhi ya watu wanaendesha kilimo cha dawa hizo za kulevya kwa kutumia teknolojia ya umwagiliaji.
Wengine wanalima bangi katikati ya hifadhi za misitu ya taifa na juu ya milima, ambako ni vigumu kwa usafiri wa gari au pikipiki.
Wakati kilimo cha bangi kinashamiri, pia kumekuwepo na ongezeko la watuhumiwa waliokamatwa kwa tuhuma za kujihusisha na dawa zingine za kulevya kama mirungi, kokeni na heroin. Ongezeko hilo linatokana na kazi inayofanywa na kikosi kazi, kinachoundwa na taasisi mbalimbali kuzidisha msako.
Kikosi kazi hicho kinaundwa na Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya, Polisi, Uhamiaji, Mamlaka ya Mapato, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, Jeshi la Wananchi, Magereza na Takukuru.
Kikosi kazi hicho kinapambana na watuhumiwa wanaojihusisha na uingizaji, usambazaji na utumiaji wa dawa za kulevya.
Akizungumza na gazeti hili jana, Kamanda wa Kikosi cha Dawa za Kulevya nchini, Mihayo Msikhela alisema mwaka huu zimekamatwa kilo 84.183.6 za dawa za kulevya, ukilinganisha na kilo 35,373 zilizokamatwa mwaka jana. Idadi ya watuhumiwa pia imeongezeka kutoka 14,339 mwaka jana hadi kufikia watuhumiwa 18,893 waliokamatwa mwaka huu.
Kilimo cha bangi Akizungumzia kilimo cha bangi, Msikhela alisema kikosi kazi hicho, kimebaini kulimwa zao hilo kwa wingi katika safu za milima mbalimbali nchini, ambako kutokana na jiografia ya huko ni vigumu kufika kwa usafiri wa gari au pikipiki.
“Bangi ni janga la taifa, watu wamegeukia kilimo cha bangi na kuacha kulima mazao mengine katika maeneo mengi nchini. Walimaji wanalima katika maeneo ambako ni ngumu kuyafikia kwa usafiri wa magari au pikipiki,” alisema Msikhela.
Alisema kutokana na msako mkali wa kikosi kazi hiyo, mwaka huu kumekuwa na kesi nyingi na kiasi kikubwa cha bangi iliyokamatwa ukilinganishwa na mwaka jana.
Alisema mwaka huu kumekuwa na kesi 8,159 zilizohusu bangi wakati mwaka jana kulikuwa na kesi 6,752. Ongezeko la kesi za bangi ni 1,407. Kiasi cha bangi ambacho kimekamawa mwaka huu ni kilo 65,804, tofauti na mwaka jana ambako bangi iliyokamatwa ilikuwa ni kilo 20,066.
Idadi ya watuhumiwa wa bangi, pia imeongezeka kutoka watuhumiwa 12,056 hadi kufikia watuhumiwa 15,800. Alisema wamebaini kuwepo kwa kilimo cha umwagiliaji wa zao la bangi katika bonde la mto Ruvu kuelekea wilaya za Kisarawe na Morogoro.
“Bonde lote lile watu wanalima bangi kwa kutumia teknolojia ya umwagiliaji, juzi tu tumegundua kuwepo kwa hekta 30 za mashamba ya bangi kwenye bonde hilo na tukaziteketeza,” alisema.
Pia alisema kikosi kazi hicho, wamebaini kuwepo kwa mashamba mengi ya bangi katika safu za milima ya Udzungwa. Alifafanua kuwa katika maeneo hayo, wakulima wanaenda milimani ambako ni ngumu kufika na huko wanapanda bangi.
“Hivi juzi Polisi tuliendesha operesheni maalumu ya kutokomeza bangi katika baadhi ya maeneo ikiwemo katika milima ya Kikewe na Mgeta, ambapo tulishuhudia bangi hiyo ikiwa imestawi katika ekari 20 za mashamba yaliyoko milimani,” alisema Musikhela.
Anasema licha ya kuteketeza mashamba hayo, lakini walikamata magunia 200 yakiwa yamehifadhiwa kwenye nyumba ambazo zimejengwa maalumu huko milimani kwa ajili ya kuhifadhi bangi. Alitaja kilimo cha bangi ambako kimeshamiri kuwa ni Morogoro, Tarime, Arusha, Iringa, Ruvuma na Simiyu.
“Mikoa hii inaongoza kwa kilimo cha bangi na tumekuwa tunafanya kazi nzito ya kusaka mashamba kwa kuwashirikisha wananchi. Dawa zingine za kulevya Akizungumzia mapambano dhidi ya dawa zingine za kulevya, Msikhela alisema kazi inayofanywa na kikosi kazi imesaidia kupungua kwa dawa za viwandani, zinazoingizwa nchini kutoka Asia na Amerika."
Alitoa mfano kuwa mwaka huu, wamekamatwa watu 250 walioijngiza cocaine nchini, tofauti na mwaka jana walikamatwa watuhumiwa 258. Hata hivyo, alisema kikosi hicho kimekamatwa kilo 18 za dawa hizo, tofauti na mwaka jana walikamata kilo 8.
Lakini, idadi ya kesi pia imeongezeka kutoka kesi 107 hadi kufikia kesi 181 na hivyo kuwepo ongezeko la kesi 74.
Kwa upande wa heroin, idadi ya kesi imeongezeka kutoka 289 hadi kufikia kesi 415 ongezeko likiwa ni kesi 126, idadi ya watuhumiwa waliokamatwa imeongezeka kutoka watuhumiwa 482 hadi kufikia 640 na kilo zilizokamatwa, zimeshuka kutoka kilo 69.3 hadi kufikia kilo 31.7.
Kwa upande wa mirungi, idadi ya kesi imeongezeka kutoka 1,071 hadi kufikia 8,159, hivyo kufanya kuwepo kwa ongezeko la kesi 233, idadi ya watuhumiwa imeongezeka kutoka 1,543 hadi kufikia 2,203 na kiasi cha dawa kilichokamatwa kimeongezeka kutoka kilo 15,229.6 hadi kilo 18,329.8 mwaka huu.
Alisema changamoto kubwa wanayokabiliana nayo ni mipaka ya Bahari ya Hindi kuwa mrefu, jambo ambalo linafanya kuwepo ugumu wa udhibiti wa uingizaji wa dawa za kulevya.
Pia alisema kwa sasa watuhumiwa wengi, wanatumia Mto Ruvuma mpakani na Msumbiji, kuingiza dawa za kulevya kutokana mpaka huo pia kuwa mrefu.habarileo
0 comments:
Post a Comment