RAIS mstaafu wa awamu ya pili, Ally Hassan Mwinyi na Rais mstaafu wa Zanzibar, Dk. Salmin Amour Juma, ni miongoni mwa vigogo wanaotajwa kuwamo katika orodha ya zaidi ya wakazi 10,000 wanaotakiwa kuhama kwenye vijiji vinne vilivyoko Mkuranga mkoani Pwani kabla hawajaondolewa kwa nguvu.
Mbali na Mwinyi, maarufu kama Mzee Ruksa na Dk. Salmin “Komandoo”, wengine wanaotajwa kuwamo katika orodha hiyo, ni Waziri Mkuu wa zamani aliyewahi pia kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU sasa Umoja wa Afrika) , Dk. Salim Ahmed Salim; Mbunge wa Jimbo la Mkuranga na Katibu wa Wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdallah Ulega, na aliyekuwa Naibu Waziri wa Fedha katika serikali ya awamu ya nne, Adam Malima.
Wengine ni Dk. Ramadhani Dau, mmoja wa watoto (anayedaiwa wa kike mkubwa) wa Waziri Mkuu wa zamani katika Serikali ya awamu ya kwanza, Rashidi Kawawa na majaji wastaafu.
Vigogo hao, pamoja na wakazi wa vijiji vinne vya Kata ya Mwanambaya, wanatakiwa kuondoka ndani ya siku 21 ili kupisha eneo hilo kuingizwa katika mpango wa upimaji wa mji.
Taarifa zilizotolewa katikati ya wiki kwenye katika mkutano uliofanyika katika kijiji cha Mwanambaya na kuhusisha wananchi wa vijiji vyote vinne, zilieleza kuwa wakazi hao wanatakiwa kuondoka kuanzia Desemba 20, 2016, ambayo ni siku iliyotolewa notisi ya kutakiwa wafanye hivyo.
Vijiji vinavyotajwa katika mpango huo ni Mwanambaya, Mwanadiratu, Mlamlemi na Mizandu, ambavyo maeneo yake yote yanadaiwa kumilikiwa na wanandugu wawili wenye asilia ya Kiasia, Karim Manji na Ahmed Manji.
Akizungumza kwenye mkutano huo wa hadhara, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mwanambaya, Leila Chaduma, alisema ililetwa barua katika ofisi yao kutoka kampuni ya APL, ikiwataka wakazi wote wa vijiji vyao vinne kuondoka ndani ya siku 21 ili kupisha eneo hilo linalodaiwa kuwa la kina Manji.
"Nilipoipokea hiyo barua niliwaita wenzangu, tukashaurina na tukaamua kutoa kopi (nakala) na tukazitawanya maeneo mbalimbali ili wanakijiji wote wazisome,'' alisema.
Pamoja na kusambaza nakala hizo, alisema aliandaa mkutano kwa wanakijiji ili wajadili notisi hiyo na kisha kupeleka nakala kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya, Mshamu Munde, ili aione na kupata ufafanuzi wake.
Chaduma alisema katika kata hiyo, wananchi wamekuwapo kwa miaka mingi, tangu Tanzania Bara haijapata uhuru mwaka 1961 na kwamba baadaye maeneo hayo yalihalalishwa kwao baada ya kupewa na hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, kwa mujibu wa wazee wao ambao wameshatangulia mbele za haki.
Alisema wanashangaa kuona Desemba 19, mwaka huu, wakipewa notisi ya siku 21 kuanzia Desemba 20, kutakiwa kuondoka wakati eneo hilo ni lao na wanaishi kwa miaka mingi.
Alisema jitihada mojawapo wanayoichukua ni kuunda timu maalumu ya kuwawakilisha ili waende kumwona Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, kumtaka awasaidie wasiporwe maeneo yao.
Mmoja wa wananchi aliyechangia kwenye mkutano huo, Omary Kisigalile, alisema hawakubaliani na notisi hiyo, hivyo watafuata sheria ili wapate haki yao.
Alisema kwa kiasi kikubwa, eneo lote linalotajwa lilikuwa pori, lakini wameliendeleza na kujenga shule za msingi, sekondari na kituo cha afya, hivyo anashangaa kusikia wakiambiwa kuwa ni wavamizi.
Aliongeza kuwa katika notisi hiyo wanaambiwa maeneo hayo yalianza kumilikiwa na kina Manji tangu mwaka 1951 na hadi sasa bado wanalipa kodi ya ardhi na kwamba taarifa hiyo inawashangaza kwa sababu miaka yote hawajawahi kuonekana wanaodaiwa kuwa wamiliki halali.
"Kama wanadai hilo ni eneo lao kihalali toka mwaka 1951, mbona kipindi cha operesheni vijiji mwaka 1974 maeneo hayo yalipotolewa hawakujitokeza? Na kwa nini wanajitokeza mwaka huu baada ya kusikia Mkuranga kuna wawekezaji wengi wamekuja kuwekeza,” alihoji Kisigalile.
Mwananchi mwingine, Idd Madenge, alisema hayuko tayari kuhama kwa namna yoyote katika eneo lake na kusisitiza kuwa hilo lilikuwa shamba la mkonge na baada ya wenyewe kushindwa kuliendeleza, serikali iliwapatia na hadi sasa hati wanazo walizopewa enzi za utawala wa awamu ya kwanza chini ya Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere.
Alisema serikali ilichukuwa shamba hilo na kuwapa wanakijiji baada ya kuona haliendelezwi.
Amina Ndombole alisema yeye na wenzake wengi kijijini hapo wamekosa amani na hivi sasa wanakaa roho juu kutokana na kuiona hiyo notisi, hivyo hatua zinapaswa kuchukuliwa sasa ili kuwaondolea hofu iliyopo sasa.
MAJINA YA VIGOGO
Akizungumza na Nipashe, Chaduma alisema wana matumaini makubwa kuwa dhuluma ya aina yoyote haitapata nafasi kwa sababu ya umoja wao na kuwapo kwa baadhi ya wamiliki wa ardhi katika vijiji hivyo waliowahi kushika nafasi za juu za uongozi.
Chaduma alipowataja baadhi ya vigogo wanaohusishwa na maeneo hayo na kuathiriwa na maelekezo ya notisi ya APL kuwa ni Rais mstaafu Mwinyi; Dk. Salmin, Dk. Salim; Balozi wa Tanzania nchini Malaysia, Dk. Ramadhani Dau; Jaji mstaafu Hamis Msumi; Malima; Ulega na mtoto mmoja mkubwa wa Mzee Kawawa.
Mwenyekiti huyo alisema baada ya kutoa nakala za notisi hiyo, waliisambaza pia kwa vigogo hao, hasa kupitia kwa watu wanaowaangalizia maeneo yao.
Hata hivyo, Nipashe haikuthibitisha kupitia vyanzo huru kuwa ni kweli, majina ya vigogo wote waliotajwa ni miongoni mwa wamiliki wa ardhi kwenye vijiji hivyo. Malima, UIega na msaidizi wa Dk. Salmin, ndio waliopatikana na kukiri kuwa wana maeneo Mkuranga.
WALICHOKISEMA MALIMA, ULEGA
Akizungumza na Nipashe juzi, Malima alikiri kuwa ni miongoni mwa watu wanaomiliki mashamba Mwanambaya, lakini alikuwa bado hajapokea notisi hiyo ya kutakiwa kuhama.
Alisema ukweli kama ardhi hiyo ni mali ya wanakijiji au ya wanaodai kuwa ni yao utajulikana kupitia uamuzi wa kisheria.
"Hivi hao watu, miaka yote walikuwa wapi hadi leo ndiyo wanajitokeza na kudai hilo eneo ni lao? Sheria zipo na tutaona haki inakuwa ya wanakijiji au yao… ngoja tuone,''alisema Malima, aliyewahi kuwa Mbunge wa Mkuranga katika serikali ya awamu ya nne.
Naye Ulega alisema ni kweli anamiliki ardhi katika eneo hilo na kuhoji hao watu waliojitokeza sasa walikuwa wapi miaka yote.
Alisema anamiliki eneo hilo tangu mwaka 2012 na anayo hati ya kuhalalisha umiliki wake, hivyo anajua sheria ndiyo itakayoamua hatima ya jambo hilo.
Akizungumzia kupokea notisi ya kuwataka waondoke ndani ya siku 21, Ulega alisema ameipata, lakini anawaunga mkono watu wa Mwanambaya wa kutokubali kuhama.
Naye mtoto wa Dk. Salmin Amour, Amin Amour, alikiri kuwa ni kweli wana eneo Mkuranga, lakini hawajapata notisi yoyote ya kuwataka wahame.
"Baba ana maeneo ya mashamba Mkuranga, lakini notisi hatujapata. Ila naomba uwasiliane na Katibu wa Mzee (Dk. Salmin) ambaye anaweza kukueleza kila kitu kuhusu hayo mashamba ya Mkuranga,''alisema.
Alipoulizwa, katibu huyo wa Dk. Salmin alisema kuwa ni kweli ana shamba Mkuranga, lakini ni katika kijiji cha Kiguza na si Mwanambaya.
"Tuna mashamba kijiji cha Kiguza na si Mwanambaya. Wengi wanafikiri tuna mashamba Mwanambaya kwa sababu ya kuwapo kwa viongozi wengi kumiliki maeneo kwenye eneo hilo la Mwanambaya,” alisema.
Diwani wa Mwanambaya, Athumani Kiwike, alikanusha taarifa za watu wa kutoka ardhi kuwa walishafanya mkutano na wanakijiji kwa ajili ya kuwapo mpango wa kukuza mji katika hivyo vijiji vinne.
Alisema watu hao wa ardhi waliwahi kufika katika ofisi yake na kumweleza juu ya kufanya mkutano na wanakijiji, na kwamba lengo la mkutano huo ni kuviweka vijiji vinne katika mipango miji.
"Mkutano huo pamoja na kwamba unakuwa wa mipango miji, lakini agenda kuu ilikuwa kuwataka wanakijiji waondoke katika hayo maeneo kwa sababu wenyewe wanataka wayafanye yawe sehemu ya utekelezaji wa mipango miji,'' alisema.
Hata hivyo, alisema aliwaambia kuwa kama wanataka kufanya maeneo hayo yawe ya mipango miji wanakubali, lakini suala la kuwaondoa hawakubali ndipo walipotaka kuonana na hao watu (kina Manji) wanaodai kuwa hayo ni maeneo yao.
Alisema baada ya hapo, mkutano haukufanyika kutokana na ukweli kuwa wahusika walishindwa kuwapeleka hao watu wanaodai kumiliki maeneo hayo; lakini wakashangaa kuona Desemba 20, mwaka huu wakiletewa notisi ya kutakiwa wahame ndani ya siku 21.
Alisema wao hawapo tayari kutoka katika hayo maeneo kwa sababu wanaishi kihalali.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mkuranga, Juma Abeid, alisema kadri wanavyofahamu, eneo la shamba likitelekezwa kwa muda mrefu bila kuhudumiwa, mmiliki hupoteza haki ya kuwa nalo.
MKURUGENZI MTENDAJI
Alipoulizwa kuhusiana na notisi hiyo ya kuwataka zaidi ya wananchi 10,000 wa vijiji vinne kuhama, Munde, alisema ni kweli kuwa taarifa hizo anazo.
Alisema ofisi ya mwanasheria wa halmashauri yao inafuatilia undani wa suala hilo ili kubaini sheria zinasemaje na mmiliki halali ni nani kati ya pande hizo mbili; yaani hao kina Manji na wananchi wa vijiji vinne.
Akieleza zaidi, Munde alisema taarifa alizo nazo ni kwamba, eneo hilo lilikuwa ni shamba la mkonge linalomilikiwa na wazungu tangu mwaka 1931, lakini mwaka 1981 likachukuliwa na wafanyabiashara wenye asili ya Kiasia na miaka yote tangu wakati huo wamekuwa wakililipia kodi kwa ukamilifu hadi kufikia sasa.
Alisema suluhu ya jambo hilo itapatikana kwa kuangalia sheria inasemaje na upande unaostahili haki utaipata.
Akizungumzia kuwapo kwa vigogo wanaomiliki maeneo hayo hivi sasa, Munde alisema sheria haitaangalia ukubwa wa cheo cha mtu bali vifungu vya sheria ndivyo vitatumika kuamua.
Aidha, Munde alisema hadi sasa, Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga haijatoa notisi ya kufutwa kwa umiliki wa eneo hilo kwa kuwa jambo hilo hupaswa kutekelezwa na Ofisi ya Rais.
WANAODAI KUMILIKI ENEO
Akizungumza na Nipashe, Luziga Bundara, mwakilishi wa kampuni ya Ardhi Plan Ltd (APL) ambao wanawasimamia wamiliki (kina Manji), alisema wanawasimamia wateja wao ambao wana eneo Mwanambaya la ekari 2,472 na lina hati namba 8291.
Alisema wamekuwa wakililipia kodi toka walipolichukua mwaka 1952 hadi sasa.
Alisema wateja wao walianza kumiliki eneo hilo mwaka 1952 wakati wanalima mkonge, lakini mwaka 1987 walishindwa kuliendeleza shamba hilo kutokana na biashara ya mkonge kushuka bei.
"Wamiliki wa eneo hili, baada ya kuona hakuna tena biashara ya mkonge, waliamua hayo maeneo wayapime ili yawe katika mpango wa mji ambao utakuwa wa kisasa na baadhi ya fedha zitakazo patikana ziingizwe katika mfuko wa halmashauri kwa ajili ya kutumika kufanikisha miradi ya maendeleo,''alisema.
Aliongeza kuwa, waliwaelimisha wananchi katika mkutano uliofanyika mwaka huu, kwenye baadhi ya vijiji, juu ya kuwapo kwa mpango wa upimaji wa mradi wa viwanja; ambapo baadhi ya wananchi walikubali na wengine waliukataa.
Alisema katika mkutano wa Novemba 27, mwaka huu, walikutana tena na wanakijiji kujadili kuhusu kuwaondoa katika hayo maeneo na ndipo Desemba 20 ikatolewa notisi ya siku 21 ya kuwataka wahame wenyewe.
Alisema zikipita siku 21 halafu bado wanavijiji hao watakuwa bado hawajahama, utaratibu wa kuwaondoa kupitia mahakama utafanyika.
WIZARA YA ARDHI
Alipoulizwa kuhusu mvutano uliopo Mkuranga kwenye eneo la Mwanambaya, Kamishna wa Ardhi, Mary Makonda, alisema mambo ya ardhi yanahitaji uthibitisho mkubwa unaoonyesha kuonyesha nani ni mmiliki halali.
Alisema suala la Mwanambaya ambalo wakazi wake wanasema lilitelekezwa kwa kipindi kirefu bila ya kuendelezwa na hali hiyo kuwapa nafasi wananchi kumiliki, linapaswa kuthibitishwa kuona kama na hao wananchi wanalimiliki kihalali.
Alisema wapo watu ambao hupeana ardhi, lakini hata hati za kumiliki hawana na hilo nalo ni tatizo ambalo limekuwa likitokea katika sekta ya ardhi na kusababisha kuibuka kwa migogoro.
"Sheria zipo wazi. Kama mtu akitelekeza shamba kwa kipindi kirefu bila ya kuliendeleza linatakiwa lifutwe… hivyo ndivyo sheria inavyosema,''alisema.
Aliongeza kuwa, kama shamba lililopo katika halmashauri husika likatelekezwa, inabidi Mkurugenzi atoe notisi ya kufutwa kwa shamba hilo; jambo ambalo yeye (wakati akizungumza na Nipashe) hakuwa na uhakika nalo kama lilifanyika au la.
MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO
Home / kitaifa /
slider
/ RAIS MSTAAFU ALLY HASSAN MWINYI YUMO KATIKA ORODHA YA WANAKIJIJI WATAKAONDOLEWA KWA NGUVU MKURANGA0
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment