Kiongozi wa Vijana wa Kanisa Katoliki la Kristo Mfalme Tabata, jijini Dar es Salaam, John Lekule akiangalia Pango la Mtoto Yesu ambalo ni mfano wa Hori la Ng’ombe alipozaliwa Yesu Kristo katika Mji wa Bethlehemu miaka zaidi ya 2000 iliyopita. (Picha na Mroki Mroki).
WAKATI leo Wakristo duniani kote wanasherehekea Sikukuu ya Krismasi, jana msongamano katika soko la Kariakoo uliongezeka, huku baadhi ya bidhaa zinazotumika kwenye sikukuu, ikiwemo nyama, zikiwa zimepanda bei.
Katika hatua nyingine, Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli imepongezwa kwa kuongoza vyema nchi kwa utulivu na amani kwa kuendelea kuwaunganisha waumini wa dini zote, Waislamu na Wakristo.
Naye Mke wa Waziri Mkuu, Mary Majaliwa ametoa msaada wa vitu mbalimbali kwa makundi ya watoto yatima jijini Dar es Salaam ili kuwawezesha kufurahia sikukuu za mwisho wa mwaka.
Habari Leo lilishuhudia msongamano huo jana katika Soko la Kariakoo, ambapo wateja mbalimbali walifurika kwenye maduka ya nguo za watoto na viatu, pamoja na kujipatia viungo na mboga vinavyotumika katika kipindi hiki.
Msongamano huo ulihusisha watu, bajaji, baiskeli, matoroli, magari ya mizigo na ya watu binafsi, hali iliyosababisha barabara kupitika kwa shida zinazozunguka soko kuu la Kariakoo. Bidhaa kama viazi jana sadolini ilikuwa ikiuzwa Sh. 4,000 hadi Sh 5,000, tofauti na bei iliyozoeleka ya Sh. 3,000 hadi Sh 3,500.
Viungo kama vitunguu saumu viliuzwa kilo Sh. 8,500 na Sh 9,000, karoti Sh. 3,000 na hoho Sh.3,000. Katika mabucha mbalimbali nyama ya kawaida iliongezeka bei kutoka Sh. 5,500 na Sh 6,000 hadi kufikia Sh. 7,000 na Sh 7,500.
Juzi, Meneja Mipango na Biashara wa Shirika la Masoko Kariakoo jijini Dar es Salaam, Mrero Mgheni alisema kuwa mzunguko wa fedha mwaka huu umekuwa mdogo, ndio maana uwezo wa watu wa kununua bidhaa katika kipindi hiki cha kuelekea sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya, umepungua.
Alisema kwa mwaka huu hali ya mzunguko wa fedha imekuwa tofauti, kwani mara nyingi mwishoni mwa mwaka, kunakuwa na mfumuko wa bei katika bidhaa sokoni hapo, hasa zile zinazotumika kwa wingi ikiwemo mchele, viazi mviringo, vitunguu swaumu, vitunguu maji, nyanya, viungo mbalimbali pamoja na nyama.
HabariLeo limeshuhudia umati wa watu katika soko hilo ni wa kawaida, tofauti na miaka mingine kunakuwa na msongamano mkubwa.
Kutokana na mzunguko wa fedha kupungua, watu wengi wamekuwa wakiangalia zaidi mahitaji ya msingi ya shule ikiwemo sare, madaftari, ada na chakula, badala ya kushughulika na maandalizi ya sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya.
Shehe Jalala ampongeza Magufuli
Katika hatua nyingine, serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli imepongezwa kwa kuongoza vyema nchi kwa utulivu na amani kwa kuendelea kuwaunganisha waumini wa dini zote, Waislamu na Wakristo.
Akitoa salamu za Sikukuu ya Krismasi Dar es Salaam jana, Kiongozi Mkuu wa Waislamu wa Dhehebu la Shia, Shehe Hemed Jalala alisema kuwa wanaendelea kuombea amani ya nchi pamoja na viongozi wote ili wapate hekima na busara ya kuendelea kuongoza vyema.
“Ninamuomba Mwenyezi Mungu kupitia Serikali hii awape hekima na busara viongozi wetu ili waendelee kutuongoza kwa salama na amani na vilevile wazidi kuboresha maelewano kati yetu sisi Waislam na ndugu zetu wakristo,” alisema Shehe Jalala.
Pia alisema kuwa mtu yeyote ambaye ana nia ya kuleta chokochoko ya kuvunja amani hiyo, asiweze kuingia katika nchi ya Tanzania ili Taifa lizidi kuwa na amani kwa ajili ya ustawi wake.
Hata hivyo, alisema kuwa salamu hizo kwa wakristo wote nchini na duniani ni kuonesha kwamba Uislam hauna chinja chinja wala ukatili kwa Wakristo, badala yake ni kudumisha amani na maelewano kati yao.
Alifafanua kuwa Waislamu na Wakristo wote ni ndugu, ambao wanaamini kwa Mungu mmoja na kwamba wote wanapaswa kuilinda amani ya Tanzania.
“Sisi Waislamu na Wakristo sote ni Watanzania ni wajibu wetu kuwa na umoja na mshikamano ni makosa makubwa kufungua mwanya wowote wa mvutano kati ya Waislam na Wakristo hapa Tanzania,” alisema.
Alisema ni vyema kuvumiliana kupitia tofauti za itikadi, mitazamo na fikra, ili kuepusha kugawanyika. Alisema Watanzania tukiendelea kuipenda nchi, amani itaimarika.
Aidha, alisisitiza kuwa salamu za Krismasi zinaonesha ishara ya upendo kwa ndugu zao Wakristo, kwa kuwa katika Vitabu Vitakatifu vinahamasisha kupendana kama mtu apendavyo nafsi yake na kwamba hakuna uadui kati ya dini hizo.
“Niwatakie mkono wa pongezi ndugu zetu Wakristo kwa kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Nabii Issa (Yesu Kristo),” alisema.
Mama Majaliwa atoa msaada Wakati huo huo, mke wa Waziri Mkuu, Mary Majaliwa ametoa msaada wa vitu mbalimbali kwa makundi ya watoto yatima jijini Dar es Salaam ili kuwawezesha kufurahia sikukuu za mwisho wa mwaka.
Mama Majaliwa alitoa msaada huo jana katika vituo vitatu vya Chakuwama kilichopo Sinza, Hisani kilichopo Kigamboni na Chamazi kilichopo Mbagala.
Akikabidhi msaada huo ikiwemo mchele, sabuni, mbuzi, juisi na soda, Mama Majaliwa alisema ameona ni vema atoe msaada huo kwa watoto hao ili na wao waweze kufurahia sikukuu za mwisho wa mwaka, kama ilivyo kwa watoto wengine.
Alitoa wito kwa makundi mbalimbali yenye uwezo katika jamii, yawe na moyo wa kusaidia makundi yenye uhitaji. Kwa upande wao, walezi wa vituo vya kulelea watoto yatima vya Chakuwama na Hisani, walimshukuru mke wa Waziri Mkuu kwa msaada huo.
Baadhi ya watoto walisema msaada huo, umewapa faraja kubwa. Mlezi wa Kituo cha Chakuwama, Saida Hassan alishukuru kwa msaada huo na alisema anawaombea kwa Mwenyezi Mungu viongozi wa Serikali ili awape afya na nguvu za kuendelea kuwatumikia vizuri Watanzania.
Mlezi wa Kituo cha Hisani, Hidaya Mutalemwa aliiomba jamii iendelee kuyakumbuka makundi yenye uhitaji, kwani bado yanakabiliwa na changamoto nyingi za kufanikisha ndoto zao, ikiwemo kupata elimu. Imeandikwa na Lucy Ngowi na Francisca Emmanuel
MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment