UJUE MZUNGUKO WA HEDHI NA SIKU ZA HATARI ZA KUSHIKA MIMBA
Mzunguko wa hedhi ni mpangilio wa mabadiliko yanayotokea katika mwili wa mwanamke kwa lengo la kuandaa mwili kwa hali ya ujauzito unaoweza kutokea. Kila mwezi katika mwili wa mwanamke ovari moja huachilia yai katika mchakato unaoitwa ‘ovulation’.
Kwa wakati huo huo kila mwezi mabadiliko ya homoni huuandaa mfuko wa uzazi ‘uterus’ kutengeneza ukuta mpya ‘endometrium’ kwa ajili ya kujiweka tayari kwa mapokezi ya mimba inayoweza kutungwa.
Kama yai litaachiliwa na kutorutubishwa na mbegu za mwanamme, basi ukuta wa mfuko wa uzazi humeguka na kutoka nje ukiwa pamoja na damu kupitia ukeni. Kitendo hiki cha mzunguko hadi kutoka kwa damu ndicho huitwa hedhi (menstruation) au mzunguko wa hedhi (menstrual cycle).
Mzunguko wa kawaida ni upi?
Mzunguko wa hedhi huanzia siku ya kwanza ya kutoka kwa damu hadi siku ya kwanza tena ya kutoka damu ya mzunguko unaofuata. Japokuwa mzunguko wa hedhi wa kawaida ni siku 28, ni jambo la kawaida kuwa na mzunguko wenye siku pungufu au zaidi ya hizo.
Mzunguko huu huweza kutofautiana kati ya wanawake lakini pia kati ya mzunguko mmoja na mwingine. Mzunguko wa kawaida huwa na siku 21 hadi siku 35 kwa wanawake wakubwa na siku 21 hadi 45 kwa wasichana wadogo walioanza hedhi.
Kwa miaka michache ya awali baada ya msichana kupata hedhi yake ya kwanza (kuvunja ungo), kupata mizunguko mirefu huwa ni jambo la kawaida. Mizunguko huanza kupungua urefu (idadi ya siku) na kuanza kuwa ya kawaida kadri umri unavyosonga na mara nyingi mzunguko huwa kati ya siku 21 hadi 35.
Msichana huanza kupata hedhi (period) wakati gani?
Kwa kawaida, msichana huanza kupata hedhi ya kwanza (menarche) afikapo umri wa miaka 11-14. Hata hivyo, hedhi huweza pia kutokea binti angali na miaka 8 na hali hii huwa ni kawaida pia. Umri wa wastani ni miaka 12 lakini hii haimaanishi kwamba wasichana wote hupata hedhi ya kwanza katika umri sawa.
Mara nyingi hedhi ya kwanza huanza miaka miwili baada matiti ya binti kuanza kutokeza. Iwapo binti hajapata hedhi ya kwanza angali na miaka 15 au ni miaka 2 hadi 3 baada ya kuanza kuota matiti, anapaswa amuone daktari.
Ukomo wa hedhi ni wakati gani?
Mwanamke huanza kupata ukomo wa hedhi (menapause) anapofika umri kati ya miaka 45-55. Wanawake wengine hupata ukomo wa hedhi angali na umri mdogo zaidi kwa sababu mbalimbali ikiwemo kufanyiwa upasuaji au baadhi ya matibabu, kuugua au sababu nyingine.
Katika hali ya kawaida, mwanamake huanza kupata hedhi chache anapofika umri wa miaka 40 ambapo huanza kupata mizunguko mirefu na inayobadilika mara kwa mara. Mizunguko huanza kuwa mirefu na baadaye kukoma kabisa.
Hedhi ya kawaida ni ipi?
Wakati wa hedhi, mwanamke hutokwa na mchanganyiko wa damu pamoja na ukuta wa mfuko wa uzazi uliomeguka kupitia sehemu ya uke. Kiasi cha damu inayotoka (menstual flow) huweza kutofautiana kati ya mizunguko. Kwa wastani mwanamke hutokwa na damu ya hedhi kiasi cha ujazo wa mililita 35 (sawa na vijiko viwili na nusu vya chai).
Hata hivyo, kutokwa na damu inayofikia mililita 10 hadi 80 (kijiko 1 hadi vijiko 6) bado huchukuliwa kama hali ya kawaida.
Wanawake wengi hupata hedhi inayodumu kwa siku 3-5, lakini hedhi yoyote inayodumu siku 2-7 huwa ya kawaida. Kabla ya hedhi kuanza, wanawake wengi hupatwa na dalili mbalimbali.
Dalili zinazowapata zaidi ni pamoja na kutokwa chunusi, matiti kuuma, kuhisi uchovu, kukasirika haraka na kubadilika kwa ukimwa (mood). Hata hivyo, kiwango cha dalili hizi hutofautiana kati ya wanawake na wengine huwa na dalili kali zaidi.
Nini hutokea mwilini wakati wa mzunguko wa hedhi?
Mzunguko wa hedhi huendeshwa na homoni mbalimbali za mwili. Wakati wa mzunguko wa hedhi, sehemu za kwenye ubongo ziitwazo ‘hypothalamus’ na ‘pituitary gland’ hupeleka taarifa za homoni kwenda kwenye ovari na kurudi kwenye ubongo. Taarifa hizi huziweka ovari na mfuko wa uzazi tayari kwa ajili ya kubeba mimba.
Kwanza pituitary gland hutoa homoni iitwayo Follicle Stimulating Hormone-FSH ambayo huenda kusababisha kukomaa kwa yai ndani ya ovari. Baada ya hapo homoni ya estrogen hutolewa ambayo huenda kusaidia ujenzi wa ukuta wa mfuko wa uzazi kwa ajili ya maandalizi ya mimba inayoweza kutokea (kwenye ukuta huu ndipo mimba hujishika, kupata virutubisho na kukua).
Wakati kiwango cha estrogen kimepanda mwilini, hali hii husababisha utolewaji wa homoni nyingine iitwayo Gonadotropin-Releasing Hormaone-GnRH kutoka kwenye sehemu ya ubongo.
Uwepo wa homoni ya GnRH husababisha pituitary gland kusababisha ongezeko la homoni ya lutenizing (LH). Baadaye LH husababisha uachiliwaji wa yai kutoka kwenye ovari, kitendo kinachojulikana kitaalamu kama ‘ovulation’.
Baada ya yai kutolewa kutoka kwenye ovari, husogezwa karibu na mfuko wa uzazi ‘uterus’ kusubiri kuungana na mbegu za mwanamme, na endapo litakutana nazo basi mimba hutungwa. Kama hakutatokea muunganiko kati ya yai na mbegu (kitaalamu huitwa ‘fertilization’) basi yai humeguka na kufa ndani ya masaa 6 hadi 24.
Dalili za yai kutoka/kuachiliwa
Muda mfupi kabla ya yai kuachiliwa kutoka kwenye ovari mwanamke hutokwa na ute katika mlango wa uzazi ambao huwa katika hali ya kuteleza na usio na rangi; ni kama sehemu ya nje ya yai bichi (isiyokuwa kiini).
Ute huu huvutika sana pia. Mwanamke anapokuwa katika hali hii huweza kupata ujauzito iwapo atagusana na mbegu za kiume. Ute huu husaidia kurutubisha mbegu za kiume pindi zinaposafiri kupita mlango wa uzazi ‘cervix’.
Iwapo mwanamke hayupo katika kipindi hiki cha yai kuachiliwa, ute wa kwenye mlango wa uzazi ‘cervical mucus’ huwa na rangi tofauti na katika hali ya tofauti.
Ute huu huweza kuwa unanata, mweupe kama maziwa, ukiwa na muonekano kama losheni ya kujipaka au kuwa na rangi ya njano. Ute huu huwa hauvutiki na huwa na harufu kali kidogo.
Aidha, nafasi ya mlango wa uzazi nayo hubadilika wakati wote wa mzunguko wa hedhi. Wakati wa yai kuachiliwa kutoka kwenye ovari, mlango wa uzazi husogea juu kidogo na njia hutanuka kidogo zaidi. Baadhi ya wanawake huhisi hali ya maumivu wakati wa yai kuachiliwa.
Maumivu haya hutofautiana na huweza kuwa ya kuvuta au ya jumla katika sehemu ya tumbo, au maumivu ya kukata upande mmoja wa tumbo ambao ndio yai huachiliwa.
Ni siku gani yai huachiliwa (ovulation)?
Mara nyingi wanawake huamini kuwa yai huachiliwa katikati ya mzunguko wa hedhi. Ukweli ni kwamba yai huachiliwa siku 12 hadi 16 kabla ya mzunguko unaofuata kuanza.
Kwahiyo, japokuwa kwa mwanamke mwenye mzunguko wa siku 28 yai lake laweza kuachiliwa katikati ya hedhi (kati ya siku ya 12 na 16), mwanamke mwenye mzunguko wa hedhi wenye siku 36 yai lake huachiliwa kati ya siku 20 na 24.
Kwa wanawake wenye mizinguko isiyobadilika sana, njia nzuri ya kukadiria siku ya yai kuachiliwa ni kutoa 16 kutoka kwenye jumla ya siku za mzunguko wake wote na baada ya kupata jibu, ajumlishe jawabu hilo na 4. Hii itampa siku ambayo yai huweza kuachiliwa.
Kwa mfano, mwanamke mwenye mzunguko wenye siku 22 mara nyingi yai lake huachiliwa kati ya siku ya 6 hadi 10 ya mzunguko wake (22-16=6, halafu 6+4=10).
0 comments:
Post a Comment