POLISI WAPEWA KAZI YA KUWATIMUA HARAKA MAKAHABA
MEYA wa Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi, Willy Mbogo, ameliagiza Jeshi la Polisi wilayani humu, kwenda kwenye machimbo ya dhahabu kuwatimua madada poa waliovamia eneo hilo kwa lengo la kufanya biashara ya ukahaba.
Madada poa hao awali walikuwa wakifanya biashara hiyo katika Mtaa wa Fisi mjini hapa.
Mbogo alitoa agizo hilo kwa Jeshi la Polisi wilayani Mpanda wakati akifunga kikao cha Baraza la Madiwani wa manispaa hiyo kilichofanyika jana.
Alisema pamoja na jitihada kubwa zilizofanywa na Jeshi la Polisi wilayani hapa la kuwaondoa kinadada poa waliokuwa wakifanya biashara ya kuuza miili yao akina dada hao wamebuni mbinu mpya tofauti na ile ya awali iliyokuwa imezoeleka.
Alisema badala ya kufanya biashara hiyo kwenye maeneo ya baa na kumbi za starehe, madada poa hao sasa wamehamia kwenye machimbo ya dhahabu ya Dilifu, Sikitiko na Kapanda.
Mbogo alilitaka Jeshi la Polisi kufika kwenye maeneo hayo na kufanya utaratibu wa kuwaondoa kama walivyowaondoa katika Mtaa wa Fisi.
Alieleza kuwa endapo madada poa hao wataachwa kuendelea na biashara hiyo, yawezekana wakati wa mavuno wakahama kwenye machimbo na kuhamia wanakovuna mazao na hasa mpunga.
Hata hivyo, Meya Mbogo alilieleza baraza hilo kuwa kitendo hicho cha kufanyika kwa biashara ya kuuza miili yao kimepokelewa kwa furaha miongoni mwa vijana na wazee wanaofanya kazi kwenye machimbo hayo ambao walilazimika kuwafuata mjini.
Alisema watu hao hufurahia kwa madai kwamba hatua ya dada poa kuhamia kwenye machimbo, kumewapunguzia gharama ya kukodi bodaboda kwani awali walilazimika kuwafuata mjini Mtaa wa Fisi.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi wilayani Mpanda, Veno Malesa, ambaye alikuwapo kwenye kikao hicho, alisema baraza hilo la madiwani kuwa watalifanyia kazi suala hilo mapema iwezekanavyo.
Mwaka jana, aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Paza Mwamlima, aliwashauri madada poa waliokuwa wanafanya biashara ya kuuza mili yao katika Mtaa wa Fisi wafike ofisini kwake awapatie wataalamu wa kuwapa elimu ya ujasiriamali ili waondokane na biashara hiyo.
0 comments:
Post a Comment