ASKARI WA USALAMA BARABARANI WASHAURIWA KULA MATUNDA ILI WAONE VIZURI
ASKARI wa Usalama Barabarani mkoani Singida wameagizwa kupanda miti ya matunda na kula matunda yake ili wakabiliane na tatizo la uoni hafifu linalowakabili hivi sasa.
Mwito huo ulitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk Rehema Nchimbi kwenye mkutano wa hadhara katika kijiji cha Iguguno wilayani hapa.
Alisema utumiaji wa matunda mara kwa mara unaboresha uoni hafifu hivyo ni jambo jema kwa askari hao kupanda miti ya matunda ili waweze kujipatia matunda ya kutosha na hivyo kuweza kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
Alilazimika kutoa mwito huo kutokana na vitendo vya mara kwa mara vya askari hao kumsimamisha barabarani kwa kudhania ni gari ya mtu wasiyemjua kisha kumwomba radhi wakidai hawakujua kuwa ni yeye.
“Yapo matukio yanayonikera. Askari wa usalama barabarani anajitokeza barabarani na kusimamisha gari langu. Baada ya kusimama tu ananiomba radhi na kuniruhusu niendelee nasafari. Eti anajitetea hakujua kuwa ni Mkuu wa mkoa anapita,” alisema Dk Nchimbi na kuongeza: “Unamuuliza hata kama hukufahamu gari lina kiongozi, Je hata bendera hujaiona.
Anabaki kukuangalia tu. Kutokana na vitendo hivi, nahisi askari hawa wana uoni hafifu. Naagiza wapande miti ya matunda ili waweze kukabiliana na tatizo hilo.”
Alisema jicho ni kiungo muhimu kwa askari wa usalama barabarani ili aone vizuri kutoka mbali; hivyo ni lazima wale matunda kwa wingi.
“Nitaanzia kukagua agizo langu hili kwa askari wa usalama barabarani kisha kwa askari wengine wote, watumishi wa ofisi yangu, wakuu wa wilaya, viongozi wote wa serikali na wananchi kwa ujumla,” alisisitiza mkuu huyo wa mkoa.
0 comments:
Post a Comment